segunda-feira, 11 de abril de 2016

ANATUONYESHA NJIA BORA YA KUTENDA, KUTUTUMIKIA NA KUTUALIKA KUMFUATA


Kutafakari kuhusu Mdo 5,27-32.40-41; Ufu 5, 11-14; Yoh 21, 1-19

         Huu ni mwaliko wa kukutana na Bwana Mfufuka na kumtambua kama upendo ambao unaitoa maana kwa maisha. Ishara anazoonyesha Bwana huyo ni alama ya kwamba yeye anaijua hali yetu na kunampendeza kushiriki katika shughuli zetu za kila siku. Yeye anatuonyesha njia bora ya kutenda, kututumikia na kutualika kumfuata kwa upendo ambao ulionyeshwa kupitia utumishi wa ndugu. Somo la kwanza linatuambia kwamba ni lazima kupatikana na hatia kwa kumtii Mungu kuliko wanadamu, kulingana na ushuhuda wa Petro na wafuasi wengine. Ni Roho Mtakatifu ambaye aliwaimarisha wafuasi wa kwanza wakubali kuaibishwa na kuteseka kwa ajili ya jina la Yesu. Tumepokea Roho huyo kwa kumtii Mungu na kuyatangaza mambo makuu yake bila hofu, kupitia maisha yetu. Kulingana na somo la pili, Yesu yu Mwanaa-Kondoo aliyechinjwa na kuishi milele. Yeye anastahili sifa na heshima ya pekee kwa sababu kujitolea kwake kwa ajili yetu kulitufanya kushiriki katika utukufu wake na heri ya milele.

     Katika injili Yesu anatokea tena kwa wanafunzi wake. Baadhi ya walimu wa Kanisa wanasema kwamba sura hii ya ishirini na moja iliongezeka baada ya hitimisho la injili, kwa sababu, baada ya kupokea kutembelea kwa Kristo, wanafunzi kumi na mmoja waliimarishwa sana ili waendelee safari yao kama mashahidi wa Bwana mfufuka. Lakini, kulingana na andiko la siku ya leo, nambari ya wanafunzi ni saba. Ingawa namba saba katika Biblia inamaanisha ukamilifu, hali hiyo ya kikundi cha wanafunzi wa Yesu haikuwa kamili. Kikundi chao kimevunjika na kukosa lengo. Hakuna kitu kingine cha kufanya ila kuvua samaki bila mpango kama walivyofanya kabla ya kukutana na Kristo. Inaonekana kwamba kupita kwa Yesu katika maisha yao hakusababisha mabadiliko yoyote. Walitenda wakati wa usiku bila kupata kitu.  Kwa kweli walitenda bila Kristo na matokeo ni kukatisha tamaa. Asubuhi inawaletea zawadi kubwa, yaani, uwepo wa bwana Mfufuka. Bwana huyo aliwasalimia kama rafiki aliyejulikana sana, lakini wanafunzi hawamtambui kwa sababu ya kuchoka kwa kazi bila mafanikio. Tena aliwaalika kuibadili njia ya kuvua samaki, yaani, kuubadilisha mwelekeo wa maisha yao. Baada ya kuona tendo la ajabu, mwanafunzi aliyependwa anatambua kwamba hakuna mwinigine aweze kupendekeza jambo kama hili ila Bwana Yesu.

     Wanafunzi walitambua kwamba ni lazima kuwa macho kuhusu ishara za uwepo wa Bwana wao na kusikiliza tena yale anayosema kama mwongozo kwa mafanikio katika kazi yao. Mfano wa mwanafunzi aliyependwa na Yesu unatuhakikishia kwamba uzoefu wa upendo unafanya kuona mbele. Wakati wengine walimwona mtu mgeni tu ambaye aliwapendekezea mabadiliko ya upande wa mashua, yule aliyependwa aliona mbele na kutambua uwepo wa Bwana. Ni uzoefu wa upendo ambao unasaidia kuona tofauti na vizuri. Kujiona kupendwa ni kufanya uzoefu wa uwepo wa mtu, yaani uwepo ambao hauwaachi waliopendwa. Upendo ndio unajua, unakuja, unajali na kutumikia. Upendo ni mwaliko wa kubadilisha mawazo, tabia, mwelekeo, njia, kila kitu. Hii ndiyo maana ya kuvua samaki tofauti. Utayari wa kuvua samaki ulionyeshwa na Petro ambaye ni wa kwanza wa kujifunga vazi na kujitupa baharini, yaani alijifunga pendekezo la Kristo na kuchukua kazi kwa shauku na ujasiri kukabili upinzani wa kibinafsi na changamoto nyingi za uinjilishaji.


      “Je, unanipenda?” Petro alikiri mara tatu upendo wake kwa Yesu licha udhaifu wake. Kama ilivyotekea na Petro, hivyo Yesu anatuuliza swali sawa na kutarajia upendo wa kweli kutoka kwetu. Kwa upande wa Yesu ni muhimu utayari wetu kwa utumishi wake kwa uaminifu mpaka upeo. Upendo ndio maana ya utume wetu. Upendo tu unatusaidia kuona mbele na kumtambua Bwana katika hali isiyotarajiwa. Ikiwa huu ni haba hautatuongoza kwa kujitolea kabisa kama mwalimu wetu Yesu alivyo. Yeye amefufuka ili atuonyeshe kwamba kujisalimisha kwa upendo ni njia ambayo inamtukuza Mungu na kuendeleza kazi ya mwanawe. Kujitolea kwa upendo wa kweli kunaitoa maana kwa kazi yetu na vitu tu ambavyo vinafanyika kwa upendo vinadumu milele.    

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah

Nenhum comentário: