Kutafakari kutoka Yoe 2, 12-18; 2Kor 5, 20-6:2 Mt 6, 1-6; 16-18
Kwaresima ni siku arobaini
za maandalizi kwa adhimisho la fumbo la Pasaka ya Kristo. Wakati huu
unatukumbusha siku arobaini ambazo Musa alibaki milimani Sinai; pia miaka
arobaini ya Wana wa Israeli jangwani; tena siku arobaini za Eliya akitembea
mpaka milima Horebi na siku arobaini za Yesu jangwani aliyeongozwa na Roho
Mtakatifu. Wakati wa kwaresima unalenga kuwa uzoefu wa jangwa. Kwa upande wa
viongozi wengi katika biblia jangwa palikuwa mahali pa mkutano na Mungu kwa
hamu na uzoefu wa utakaso. Walitafuta mahali huko kabla ya matukio muhimu
maishani mwao ili waweze kuchukua ahadi kwa nguvu na uaminifu. Vivyo hivyo, ni
Kwaresma kama maandalizi kwa tukio muhimu sana la imani yetu, yaani Ufufuko wa
Yesu.
Ni wakati kwa kutafakari kwa njia ya ndani
kuhusu huruma ya Mungu na hali yetu ya wenye dhambi. Hasa katika Mwaka huu wa Jubilei, kutafakari kwetu kuhusu huruma ya Mungu
kunatuongoza kuishi katika mwanga wa maneno ya Bwana: “Muwe na huruma kama Baba
yenu alivyo na huruma (Lk 6, 36).” Dhamiri
kuhusu matokeo ya dhambi katika maisha yetu inatuongoza kumwomba Mungu
kulingana na somo la kwanza, yaani “Wahurumie watu wako ee Bwana!” nasi tunajua
kwamba Mungu anawahurumia watu wake sio kwa sababu wanastahili, lakini kwa
sababu hii ni tabia yake ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa
hasira, bali ni mwingi wa rehema. Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha
kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye
kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima.” Kwa hivyo tunaalikuwa kumrudia yeye kwa imani na
kuutumainia wokovu wake. Kama mwendelezo, somo la pili linaongea kuhusu
mahitaji ya upatanisho na Mungu kwa sababu yeye mwenyewe anatupa nafasi ya
kufanya hivyo kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Huu ni wakati wa neema, nasi
hatuwezi kuipokea neema ya Mungu bure. Wakati wa mabadiliko na wa wokovu ndio
sasa.
Katika dini ya kiyahudi,
kuna hatua tatu muhimu sana ambazo zinadhihirisha utambulisho wa myahudi wa
kweli, yaani sala, sadaka (itolewayo kwa maskini) na kufunga. Hasa wakati huu wa
kwaresima tunaalikwa kuchukua hali hizi kama ishara ya toba yetu. Yesu
alipopendekeza hatua hizi tatu, yeye aliwakumbusha wafuasi wake kuhusu maana na
roho ambayo lazima kuimarisha hatua hizi. Wakati wa Yesu, kufunga kulikuwa
shughuli ya kawaida, naye pia alifunga kwa wakati wa siku arobaini jangwani
kabla ya kuanza ujumbe wake kwa umma. Yesu alitaka kwamba wanafunzi watende kwa
tabia ya kweli sio kama ile ya baadhi ya watu (wanafiki) ambao walipofunga wakaonyesha
huzuni; hao walikunja nyuso zao wapate kuonekana kwa watu kuwa wanafunga. Yesu aliihakiki tabia hii na akasema
kwamba wamekwisha pata tuzo lao. Kwa Yesu kufunga kuzuri ni kujinyima baadhi ya
chakula kwa mshikamano na maskini. Tunaweza kueneza ujumbe huu kwa kufunga
baadhi ya maneno, ya matendo na ya mawazo ambayo si mazuri katika uhusiano wetu
na wengine. Kwa hivyo kanisa katoliki linapendekeza hayo hasa wakati huu ambao
ni kipindi maalum cha toba na mabadiliko ya maisha.
Kuhusu sala,
ni vizuri pia kuufuata mfano wa Bwana wetu. Yeye alikuwa mtu wa sala na
aliijulisha sala kama njia ya uaminifu kwa mpango wa Mungu. Sala yake ilikuwa maonyesho
wa uhusiano wake na Baba na mwaliko kwa wanafunzi wake wafanye vivyo hivyo kama
utambulisho naye. Kwaresima ni wakati wa sala kwa hamu zaidi, kufungua akili zetu
na mioyo yetu kwa tendo la wokovu wa Mungu. Huu ni wakati pia wa kutenda
matendo ya huruma kwa wenzetu, kuonyesha juhudi yetu ya kubadili hali yetu na
kandokando yetu. Majivu usoni ni ishara ya hali yetu ya ndani na kwamba
tunakubali mwaliko wa Kanisa wa toba kwa sababu wakati wa kuukaribisha wokovu
wa Mungu na kuiamini injili ndio sasa.
Fr Ndega
Mapitio: Sara
Nenhum comentário:
Postar um comentário