domingo, 6 de setembro de 2015

AMEFANYA MAMBO YOTE VEMA


Kutafakari kutoka Isaya 35:4-7; Yak 2:1-5; Mk 7: 31-37

       Kulingana na somo la kwanza, Watu wa Israeli walikuwa wafungwa katika Babiloni na nabii Isaya aliwatangaza wakati mpya, wakati wa ukombozi na furaha. Kulingana na nabii Watu hawa ni kama vipofu ambao wanaishi gizani mwa Babiloni na hawapati kuona njia ya kurudi nyumbani; tena wao ni kama walemavu ambao hawawezi kutumia miguu yenyewe ili kuacha mahali ambapo walikuwapo; pia wao ni kama viziwi na bubu kwa sababu waliyafunga masikio kwa Neno la Mungu. Hata hivyo Mungu atakuja kuwaokoa kwa sababu watu hawa ni mali yake na awapenda. Tendo hili la ajabu ambayo Mungu atatenda kwa ajili wa Watu wa Israeli yatachukuliwa na Yesu kwa watu wote kwa sababu yeye ni wokovu wa Mungu kwa wote. Katika somo la pili Yakobu anawaalika wakristo kushinda tabia ya ubaguzi katika jumuiya na kuthamini uwepo wa kila mtu zaidi kuliko hali au uwezo wake.

       Katika injili, matendo ya Yesu yanatambuliwa na watu ambao walitangaza, “amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema”. Uwepo wa Yesu umeleta wakati mpya ulimwenguni. Katika Yeye ufalme wa Mungu umekuwa hali halisi, ukiwaalika wote washiriki. Wakati aliutangaza ujumbe wake katika sunagogi ya Nazareti, mahali alipolelewa, alikataliwa. Lakini alikaribishwa sana katika upande wa ziwa Galilaya, mahali panapoitwa Dekapoli - yaani miji kumi. Kulingana na toleo la Mathayo, Galilaya ilifikiriwa “nchi ya watu wa mataifa”. Uwepo wa Yesu unawafanya watu waliokaa “gizani” waone mwanga mkubwa. Basi, ingawa watu hawa walikuwa na lugha na desturi tofauti kwa ushusiano na wayahudi wa Yudea, walimtarajia Masiya kwa hamu sana. Tunapata kufahamu hali hii kwa sababu Injili ya Marko iliandikwa kwa wakristu wa huko Roma na lengo la injili hii yote ni kujibu kwa swali “Yesu ni nani?”. Jibu kwa swali hili tunakuta katika wakati wa mwisho wa maisha ya Yesu kutoka midomo ya jemadari mmoja wa Roma: “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

      Kama Mwana wa Mungu, lengo la Yesu ni kutangaza wokovu wa Mungu si kwa watu fulani tu, bali kwa wote. Yesu alikuwa myahudi, bali hakawa mali ya Wayahudi. Ishara zilizotumiwa na Yesu zilidhihirisha kwamba wokovu wa Mungu si mpango kwa wakati ujao tu, bali unaanza katika historia na upo kwa wote. Wakati tunaongea kuhusu “watu waliochaguliwa” tunamaanisha mpango wa hekma ya Mungu ambaye anatumia baadhi ya watu ili kufikia wengine kwa urahisi. Kama hii, kutoka Waisraeli Yesu na washirika wake walifikia wasio na Wayahudi pia wakitangaza habari njema ya injili. Mtu yule aliletewa kwa Yesu alikuwa na matatizo mawili, yaani, alikuwa bubu na kiziwi. Aliteseka sana na mara nyingi alikuwa mpweke kwa sababu hakuweza kuwasiliana na wenzake kila alichofikiri au kutamani, na wao pia hawakueza kuzungumza naye. Alitamani kukutana na Yesu na kupitia maisha mapya ili kufanya uhusiano mwema na wengine. Kabla ya kufanya mwujiza Yesu anatazama juu mbinguni kwa maana ni Mungu peke aliyemwezesha kumponya Bubu kiziwi.


       Kama wafuasi wa Yesu tunahamasishwa na uamuzi na ishara zake. Ujumbe wetu ni mwendelezo wa ujumbe wake na kama yeye tunaalikwa kufanya mambo yote vema. Mtu bubu na kiziwi ni ishara ya ugumu wetu wa kusikiliza Neno la Mungu na kulitangaza kwa uaminifu. Lakini kupitia sisi hata kwa udhaifu wetu Yesu anaendelea kufanya mambo makuu maishani mwa watu wengi. Injili haina mpaka; vivyo hivyo ni matendo mema ya wakristo. Tunaalikwa kushinda vikwazo ambazo vinatuzuia kuwakaribisha wengine na kuwa na unyeti mbele ya mahitaji yao. Kama watu waliona mwujiza wa Yesu na kutangaza bila kuchoka, vivyo hivyo tunapaswa kutangaza makuu ya Mungu ili watu wengine wapate  maisha mapya.

Fr Ndega
Mapitio: Sara

Nenhum comentário: