Kutafakari kutoka Is 50:5-9; Mk 8:27-35
Yesu alikuwa
anatembea pamoja na wanafunzi wake na karibu na Kaisarea Filipi anawauliza
maswali kuhusu utambulisho wake kulingana na mtazamo wa watu. Majibu yalikuwa ishara
ya kwamba wazo kuhusu Yesu halikuwa wazi sana kwa upande wa watu. Ingawa halikuwa
wazi kwa watu, kwa wafuasi wa Yesu lazima kuwe tofauti, kwa sababu kwa Yesu si
muhimu sana yale ambayo watu wanafikiri, bali kukiri kwa wafuasi wake. Petro
anadhihirisha yale ambayo wanafunzi wengine kumi na mmoja wanajua pia: Yesu ni
masiya wa Mungu. Lakini hawawezi kutangaza habari hii kwa sababu ya kutokuwa na
maana kamili. Yesu alitambua kwamba wafuasi wake walihitaji ufunuo zaidi na
kujifunza vizuri maana ya umasiha wake na masharti kwa uanafunzi wa kweli.
Mawazo ya
wafuasi wa Yesu kuhusu masiya yalifuata matarajio ya wayahudi wengine, yaani,
masiya wa kisiasa atakayetumia nguvu zake za kimungu ili kuwakomboa Wayahudi
toka ukoloni wa Warumi. Bila shaka kwamba yesu anayakanusha mawazo hayo kwa
kuonyesha njia tofauti ya kutimiza ujumbe wake wa masiya, ni kwamba, kupitia
mateso, kifo na kufufuka. Umasiha ulichaguliwa na Yesu ni umasiha wa mtumishi
mwema kulingana na Somo la kwanza. Utambulisho wa Mtumishi huyo ni kuwa makini
kwa sauti ya Mungu ili aweze kufanya mapenzi yake kutumikia kabisa. Kwa kufanya
mapenzi ya Mungu mtumishi huyo anapaswa kuteseka na kufa, lakini alisimama
upande wa Mungu ambaye alimsaidia akimfanya mshindi. Pamoja na wazo wa wongo
kuhusu umasiha wa Kristo, itikio la Petro lilidhihirisha pia baadhi ya upinzani
dhidi ya njia ya maisha ambayo Yesu alichagua ili atimize mapenzi ya Mungu. Uamuzi
wa Yesu ulikuwa katika ushirika na Baba yake na upinzani dhidi ya njia hii ni
upinzani dhidi ya mapenzi ya Mungu.
Wanafunzi
wa kwanza walihitaji mwendo mrefu ili kujifunza kumhusu Yesu na kuyafahamu
mapendekezo yake sawasawa. Wakati Yesu alimkemea Petro na kumwalika afuate
mtazamo wa Mungu, alihitajika rejea za nguvu kwa uanafunzi wa kweli. Kidogo
kidogo walitambua kwamba kwa kujitoa kama Yesu alivyo, walipaswa kuzifuata
hatua tatu, yaani, kujikana wenyewe, kuichukwa misalaba yao na kumfuata Yesu.
Kwa maneno mengine, walipaswa kuyabadilisha maisha yao kwa jumla. Kama hii ni lazima
kuwa kwa sisi sote. Wale ambao hukutana na Yesu hawakubaki walivyo na hawawezi
kumdai Yesu atende kulingana na mapendekezo yao. Mwendo lazima kuwa tofauti.
Kwa kumfuata Yesu kweli tunapaswa kupatikana kwa kila kitu na kuweka ndani ya
maisha yetu mapendekezo ya Yesu. Tunapaswa kufanya maisha yetu kulingana na
njia ya Yesu ya kuishi na kuchukua
msalaba kama yeye alivyo.
Injili ya Marko katika kifungu hiki inatusaidia kutafakari kuhusu njia ambayo tumechagua ili kumfuata Yesu. Je,
hii ni njia ya kweli? Tunatambua kwamba Kumfuata Yesu hakuuleti upendeleo au
hadhi, bali mateso na kujisalimisha kwa ajili ya injili. Basi, yeyote ambaye
anataka kuishi shwari na bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Yeyote ambaye
anatamani kumfuata Kristu bila msalaba hatamfuata Kristo kweli kamwe. Kupitia
mambo hayo tunaweza kujiuliza maswali: Je, Kristu gani tumemfuata? Mawazo au kitu
gani tunahitaji kujinyima bado ili tuweze kumfuata Yesu kikamilifu? Maisha yetu
ya kawaida ni ishara ya kwamba tumekuta hazina yetu ya kweli? Ili Ekaristi hii
takatifu itusaidie kuishi wito wetu wa wanafunzi wa Yesu kwa shauku na furaha. Ili
ujumbe wa liturujia ya siku ya leo uiimarishe imani yetu na kutuhamasishe kumfuata
Yesu kwa uaminifu na tayari kwa kila kitu kwa ajili ya injili, kwa ajili ya
ufalme wa Mungu.
Fr Ndega
Mapitio: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário