domingo, 5 de abril de 2020

MAANA YA MATESO YA KIBINADAMU



kutafakari juu ya Mt 21,1-11; Is 50,4-7; Waf 2,6-11; Mc 14,1-15,47



       Tunaingia katika wiki muhimu sana kwa Jumuiya za Kikristo. Hii ni wiki inayojumuisha matukio makuu ya imani yetu, ikieleza kwa ishara nyingi na kwa kina vipindi vya mwisho vya maisha ya Yesu ya kibinadamu hapa duniani na kutualika kwa kimya na kutafakari. Hii ni pia nafasi ya kufanya upya ahadi yetu kama wafuasi wa Yesu na kujiruhusu kuimarishwa na mfano wake wa uaminifu na uamuzi.

       Tunaalikwa kumfuata Yesu anayeingia kama mshindi katika Yerusalemu ili kukamilisha kazi yake ya upendo. Kweli, hakuja juu ya farasi kwa kiburi na kwa jeshi yenye nguvu kama walivyofanya majenerali wakiingia mijini, lakini amepanda punda, na kuja kwa wema na rehema kama imetokea wakati wa maisha yake yote. Yesu anajua sana nini itatokea nawe, hata hivyo hakukata tamaa. Kinyume, anaonyesha uhuru wa Mwana mpendwa aliyetumwa kuwaokoa wanadamu. Pamoja na kukumbuka kuingia kwake katika “Mji wa amani”, tunakumbuka pia mateso na kifo chake katika mji huu ulio na mazoea ya kutenda kwa ukatili dhidi ya wajumbe wa Mungu. Hivyo, kifo chake sio hatima, bali ndicho matokeo ya kazi ya kinabii aliyeishi kwa uaminifu hadi upeo.

       Kama tunavyojua, nabii Isaya anatoa nyimbo nne ili kuongea juu ya utambulisho na kazi ya Watu wa Mungu, wanaoitwa pia “Mtumishi wa Mungu.” Nyimbo hizi ziliandikwa wakati wa utumwa wa Babeli nasi tunaweza kuzipata katika sehemu ya pili ya Kitabu cha Isaya. Andiko tunalotumia hapo unafahamika kama ‘wimbo wa tatu’ na kulingana na wimbo huu, mtumishi anaishi wito wake kama zawadi inayotoka kwa Mungu kwa ajili ya kutoa maisha mapya kwa ndugu zake. Kwa sababu ya uaminifu wake, aliaibishwa, alikataliwa na kuteseka sana, lakini hakukata tamaa kwa sababu aliona ukaribu na utunzaji wa Mungu kuyahusu maisha yake.

     Kulingana na Jumuiya za Kikristu Mtumishi huyo ni mfano wa Yesu. Mtakatifu Paulo asema kwamba kwa ajili ya kujiambulisha mwenyewe na hali ya binadamu, Yesu Kristo alijinyenyekeza, akaaibishwa, akateseka na kuuawa maana ya uaminifu wake kwa Mungu. Amini yake ya mwana katika Mungu ndiyo maana ya uaminifu wake. Kwa njia ya kujifanya upole aliupata utukufu. Njia ya unyenyekevu, ya ishara ndogo na ya kuchagua kinachoonekana bila maana kwa jamii ndizo tabia za wale wanaoendelea kazi yake.

      Kulingana na masimulizi ya Marko, Yesu anafikiria kuwa kukamatwa kwake, mateso yake na kifo chake kitakuwa kashfa kwa wanafunzi wake, maana bado walikuwa na mawazo ya Masihi mwenye nguvu na umaarufu. Hata hivyo, aliendelea akisema kuhusu ufufuko wake na baadaye mkutano nao kwenye mahali ambapo yote yalianza, yaani kutoka Galilaya. Kwa Yesu hakuna maonyesho ya upendo kubwa kuliko kutoa maisha yake kwa ajili ya marafiki zake, hata wakati wao wametoroka (isipokuwa wanawake na mwanafunzi mpendwa, kulingana na injili ya Yohane).

     Katika kilio chake, yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?”, yeye alionyesha uchungu aliohisi kweli kama mwanadamu, yaani, uchungu wa kuachwa, uchungu wa vitendo viovu, uchungu wa dhambi za binadamu, n.k. Ghafla, wakati yote yalionekana yamefanyika bila mafanikio, tuko na tangazo kubwa la imani kutoka kwa watu wasiotarajiwa, yaani yule akida pamoja na walioandamana naye: “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

      Yesu aliachwa na marafiki zake, lakini yeye hakuwako peke yake msalabani wala wakati wa kazi yake. Maneno yake mwenyewe yanashuhudia kuhusu hayo, yaani “Yule aliyenituma yuko pamoja nami, hakuniacha peke yangu, kwa maana mimi nafanya yanayompenda yeye (Yoh 8.29).” Hivyo “kilio” ambacho Mathayo anaweka mdomoni mwa Yesu kinapaswa kufahamika kwa uhusiano na kujisalimisha kwake mikononi mwa Baba, kulingana na toleo la Luka, iliyo tabia yake daima, yaani “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu (Lk 23,46).” Vinginevyo, tungekuwa kukana sio tu ushirika wake na Baba bali pia uaminifu wa Baba huyo.

      Fumbo la mateso na kifo cha Yesu halionyeshi uchungu kama jambo la kwanza kwa kutafakari bali upendo wake mkubwa hadi upeo. Kifo hakikuwa kulazimishwa kwa Yesu, bali jambo ambalo yeye alikubali kwa hiari. Yesu alijua kwamba alikuwa akifanya jambo sahihi na hivyo mateso yake ni mwanzo wa ushindi wake juu ya mauti na ya dhambi, akifufua matumaini yote ya maskini na ya wanadamu wote.

     Mateso ya Mwana wa Mungu yanatualika kutafakari kuhusu hali ngumu ya mateso ya binadamu. Kama Mungu alijibu kwa ufufuko mbele ya kifo cha Mwanawe, tunaweza kuhitimisha kwamba Mungu hataki mateso na uchungu wa watu. Yeye hawaachi wale wanaoteseka wala hanyamazi mbele ya mateso yao. Kristo alichukua kwa nafsi yake uchungu wa watu wote wa nyakati zote. Yeye anaendelea kuteseka wakati sisi tunahisi maumivu na majaribio katika safari yetu. Mfano wake unatuimarisha tuwe na kuwepo ufanisi maishani mwa watu wanaoteseka zaidi kuliko sisi. Misalaba ya mshikamano na huruma tunayoitwa kuchukua kila siku kama yeye alivyo inafanya kwamba kujitolea kwetu kuwe ishara ya upendo pia kama ushiriki katika mateso yake kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

Fr Ndega

Nenhum comentário: