sábado, 30 de junho de 2018

YESU ANAWEZA KUURUDISHA UZIMA KWA SABABU YA IMANI



Kutafakari kutoka Hek 1,13-15;2,23-24; Mk 5, 21-43


Mauti yako duniani lakini hayatoki kwa Mungu kwa sababu yeye ndiye uzima na kutuumba kwa uzima. Mungu hataki mauti ya watoto wake lakini hazuii watende dhidi ya mapenzi yake kwa sababu anaheshimu uhuru wao wa uamuzi. Huu ndio ujumbe wa kifungu cha Kitabu cha Hekima. Andiko hili linachukua tena tukio la uumbaji na kuonyesha nia ya Mungu alipoumba viumbe vyote. Ingawa ndiye binadamu anayefanyika kwa mfano na kwa sura ya Mungu, viumbe vingine pia vinaonyesha uzuri wa nafsi ya Mungu na kuongelea yeye. Hivyo, binadamu anaitwa kuishi kwa maelewano na viumbe vyote kwa sababu yeye na vingine vina asili sawa. Mambo yote binadamu anayepanga kufanya kwa ajili ya viumbe vingine yanaleta matokeo kwa maisha yake mwenyewe.    
Baada ya kufukuza pepo wachafu kutoka mtu fulani, Yesu aliendelea anahubiri habari njema na kutenda mambo mema mengi. Watu wakastaajabu. Kweli Yesu alikuwa mtu maarufu na mahali popote ambapo alifika mara makutano makuu yalikusanika yakimsongasonga ili kusikiliza neno la Mungu. Kulingana na andiko la leo Yesu alivuka ziwa la Galilaya na kubaki kando ya bahari. Tena umati wa watu ulikusanika kumsikiliza. Kwa upande wa Yesu, yeye alipatikana kwa ajili ya kujifunza watu na kuwasaidia katika mahitaji yao. Kwa upande wa watu, imani ndiyo kipengele msingi.
Alipozungumza, mtu mmoja aliye mkuu wa sinagoga aliyeitwa Yairo alimwendea kumwomba aponye binti yake aliyekuwa mgonjwa na mara Yesu alienda pamoja naye na wanafunzi watatu. Lakini wakati wa safari mtoto alikufa. Yesu alimwambia Yairo: “uwe na imani tu!” kweli, kwa sababu ya imani ya Yairo na mke wake mtoto alifufuliwa. Kabla ya Yesu kwenda kwenye nyumba ya Yairo, mkutano mkuu waliomfuata wakisongasonga. Miongoni mwao alikuwako mwanamke fulani aliyekuwa mgonjwa wa kutoka damu. Yeye alimgusa Yesu kwa imani kubwa na mara akapata kuponywa. Yesu alimwambia: “binti, imani yako imekuokoa”.
Katika matukio hayo mawili ndiyo imani kipengele cha msingi ili Yesu atende muujiza. “Imani ndiyo msingi, kama Marko asemavyo kwamba, Yesu hakuweza kufanya miujiza Nazareti kwa sababu watu walikosa imani (Mk 6, 1-6).” Miujiza siyo uchawi ili mtu aseme: “utuonyeshe kitu nasi tutasadiki!”, bali ni mwaliko wa kutusaidia kuzikuza imani yetu. Katika miujiza mingi ya Yesu, imani ndicho kipengele cha msingi. “Hata iwapo siyo imani kutoka kwa mgonjwa mwenyewe moja kwa moja, kwa mfano binti Yairo, imani ya jumuiya ni muhimu (Mk 2,5).” Tukumbuke tena wakati Yesu alipokuwa ndani ya nyumba fulani iliyojaa watu. Kikundi kimoja cha watu ambacho kilimbeba mtu mgonjwa, kilifanya shimo katika dari ya nyumba na kupata kumuweka mtu mgonjwa mbele ya Yesu. Kwa sababu ya imani yao, Yesu alimponya mtu mgonjwa. 
Ndilo jambo la ajabu inayoonekana katika matukio mawili, yaani mwanamke fulani alikuwa mgonjwa kwa miaka kumi na miwili na mtoto alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Nambari hii yaani kumi na miwili ndiyo ishara muhimu katika biblia na kumaanisha Watu wa Israeli na ubinadamu mzima. Wote yaani mwanamke na mtoto wanahitaji uzima kwa sababu ya ugonjwa. Ndiye Yesu peke yake anayeweza kuwapatia uzima kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye uzima wa milele. “Mwanamke mgonjwa wa kutokwa damu, alikuwa na imani iliyosukuma amguse Yesu na hivyo akaweza kuponywa.”  Kulingana na Agano la Kale, kugusa mavazi ni kugusa mtu mwenyewe. Tukumbuke kwamba ilitosha kupata mavazi ya Elijah ili Elisha apokee roho yake. “Tendo la kugusa ni ishara ya upendo, kama vile mtu anapomgusa mgonjwa, ni ishara kwamba anampenda na kumjali katika hali yake yote.” Ingawa hali ya mwanamke ilikuwa uchafu na yeyote aliyekutana naye alikuwa mchafu, Yesu aliruhusu kuguswa naye na kubadilisha hali iliyotarajiwa na wote, yaani badala ya kuwa mchafu yeye alisababisha usafi mwilini mwa mwanamke.
 “Usiogope; amini tu...” yalikuwa maneno ya Yesu kwa Yairo alimpoteza mtoto wake. Maneno ya Yesu ni maonyesho ya upendo na huruma yake kwa ajili ya walioteseka. Tumejifunza na kuhisi kwamba “moyo wa Yesu ni chemchemi ya huruma” na Maandiko yenyewe yashuhudia kwamba “Kwa upande wake tumepokea neema juu ya neema”. Habari hii inaiimarisha imani yetu na kulifufua tumaini letu. Nasi kama Yairo na watu wengine twapewa changamoto ya kuamini kuwa Yesu anaweza kurudisha  uzima. Kilichotokea katika maisha ya Yesu kilikuwa kimelenga katika kuwaelimisha wale wenye imani kuwa wao pia watapata uzima kwa sababu, kulingana na mapenzi ya Mungu maisha yetu yanafaa kupata ukamilifu kwa kufufuka kama Mwanawe. Uzima kwa mwenye imani wawezekana kutokana na ufufuko wa Kristo. Tujaribu kumwamini Kristo na matendo yetu yawe tangazo la uzima uliomo ndani yetu ambao yeye mwenyewe anatuhakikishia. 

Fr Ndega

Nenhum comentário: