sábado, 2 de junho de 2018

KUWA ‘EKARISTI’ ILI KULISHA ULIMWENGU



Kutafakari kuhusu Kutoka 24: 3-8; Ebr 9: 11-15; Mk 14: 12-16, 22-26


         Siku ya leo tunaalikwa kuadhimisha sikukuu ya Mwili na Damu ya Kristo, lililo fumbo la imani yetu. Hii ni nafasi maalum kuonyesha shukrani yetu na upendo wetu kwa zawadi kuu ya Ekaristi takatifu. Hii ni siku ya kutafakari kuhusu uwepo wa kweli wa Kristo katika ishara za mkate na divai. Ekaristi takatifu ni fumbo la kujisalimisha kwake kwa upendo kwa wokovu wa ulimwengu. Ekaristi ni adhimisho la fumbo la Mungu ambaye anawatumikia watu wake, yupo karibu nasi na ndani yetu. Hilo ni fumbo la ushirika ambao tunahusishwa kama washirika katika uhai wake. Ekaristi ni sakramenti ya Agano jipya na milele kupitia hilo Kristo anatuunganisha naye na miongoni mwetu wenyewe kama wana wa watu wapya wa Mungu lililo Kanisa.

      Masomo ya leo yanaongea kuhusu hali hii. Kulingana na somo la kwanza, agano ambalo Mungu alianzisha na watu wake lina kama msingi Neno lake ambalo watu alikubali kama mwongozo ili waweze kuishi kulingana na matarajio yake Mungu. Katika mwendo huu ni muhimu uwepo wa Musa kama mpatanishi mwema ili maneno ya Mungu yatangazwe kwa watu kikamilifu. Damu ya wanyama waliotoa kwa Mungu ikanyunyizwa juu ya watu ikithibitisha ahadi kati ya Mungu na watu wake. Somo la pili linaongea kwamba Kristo ndiye mpatanishi wa kipekee wa agano jipya na milele. Ukuhani wake ni mkubwa kuliko ukuhani wa agano la kale  kwa sababu una asili ya Mungu. Yeye hakuhitaji kumtolea Mungu damu ya sadaka ambayo inatoka kwa wanyama, bali alijitoa kama sadaka kamili na kupitia damu yake wanadamu wote walipata wokovu.

          Injili inasimulia tukio la Karamu ambayo Yesu akitumia ibada ya Wayahudi, alianzisha Ekaristi takatifu. Fumbo la usiku ule lilifunua hamu ya kiini ya moyo wa Yesu. Kweli Yeye alitaka kusherehekea pasaka na wanafunzi wake kwa sababu alikuwa na jambo muhimu la mwisho la kudhihirisha kwao. Aliwapa mafundisho yake ya mwisho akiwaalika kubaki kuungana naye kwa ajili ya mafanikio ya kazi yao: “Bila mimi hamwezi kufanya chochote”. Basi, kwa kutarajia, akihisi mwenye uhuru kabisa kwa kujitolea mwenyewe kwa ajili ya wale ambao aliwapenda mpaka upeo, "alitwaa mkate na kikombe, akashukuru, akawapa, akasema: twaeni huu ndio mwili wangu na hii ndiyo damu yangu. Vitendo hivi vya Yesu na wanafunzi wake vilivyofanyika katika hali ya kifamilia na amini ya kubadilishana kama mwaliko wa kuchukua ahadi pamoja.

          Mkataba kati ya Mungu na watu wake katika agano la Sinai ulikuta maana yake kamili na Yesu ambaye alifanya mkataba mpya, akianzisha Agano jipya kati ya Mungu na Watu wake wapya. Akitumia Ibada ya Wayahudi, Yesu alianzisha Ibada mpya, yaani Mlo wa Ekaristi, akitangaza kwa Wafuasi wake ukombozi kamili ambao ulikuwa ukija na kwamba alitamani kwa shauku kushiriki na marafiki zake. Katika karamu hii ya mwisho, Yesu alijitoa kama chakula na kinywaji, akionyesha maana ya kujisalimisha kwake kwa hiari msalabani. Kujisalimisha kwake kwa upendo na hiari kunakuwa tabia kamili na sharti kwa yeyote anayetaka kumfuata. Wanafunzi wake wakati watakaposherehekea Kuumega Mkate wataendelea mwendo huu kama ushiriki katika kujisalimisha kwa mwalimu Yesu wakipokea nguvu ili kujitolea wenyewe kama yeye alivyo.

     Huu ndio msingi wa misa takatifu yote. Hili ni maana ya imani yetu. Tunaalikwa kuadhimisha fumbo la Mwili na Damu ya Kristo kwa upendo na ahadi sawa Kristo alikuwa nayo aliposherehekea pamoja na wanafunzi wake. Yeye alianzisha Ekaristi akiutoa mwili na damu yake katika ibada, akiandaa wanafunzi wake kwa kujisalimisha kwake msalabani. Katika sakramenti hii Kanisa linaukuta utambulisho wake wa kweli kwa sababu linafanya upya ahadi yake na Yule aliye kichwa chake. Katika kila Ekaristi takatifu Kanisa linahisi moja na Kristo ili kuleta uzima wake duniani kote. Hii ndiyo Sakramenti inayolifanya Kanisa; hii ndiyo msingi na lengo la kazi yake.
    Katika Ekaristi uwepo wa Yesu ni hai na ufanisi. Yeye mwenyewe katika kila maadhimisho ya Ekaristi anatufanya kuona mabadiliko ambayo tunahitaji ili kuwa mashahidi wenye furaha wa ufufuko wake. Tunapoadhimisha Ekaristi tunabadilishwa kuwa kama Yule ambaye tunamsherekea kwa kukubali ukweli wa Fumbo hili kama “Pasaka ya Kristo katika pasaka yetu na pasaka yetu katika Pasaka ya Kristo”. Hivyo, baada ya kila adhimisho ya Ekaristi tuna changamoto ya kurudia shughuli za kila siku kama mashahidi wa Kristo anayetoa maisha yake kwa upendo ili wote wawe na maisha kamili. Basi, tumshukuru Mungu kwa uzoefu wa udugu tunaoishi katika kila misa takatifu tunayoadhimisha. Neema yake itusaidie kuishi uhusiano wa ndani na Yesu ili maisha yetu yawe kama vile yake, ‘ekaristi’ ili kulisha ulimwengu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: