sábado, 26 de maio de 2018

KUWA MWANAFUNZI WA YESU KUNAMAANISHA KUWA MAKAO YA UTATU MTAKATIFU



Kum 4, 32-34.39-40; War 8, 14-17; Mt 28, 16-20


       Tunaalikwa kutafakari kuhusu fumbo la Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ni fumbo la Mungu aliye ushirika wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Yeye yu ushirika wa upendo kwa maana Mungu ni upendo. Upendo ni tabia ya Mungu. Hivyo, “Mungu ni Utatu kwa sababu ndiye upendo” (L. C. Susin). Mungu yu wa kipekee lakini haishi peke yake kwa sababu alitaka kuwa na kuishi kwa ushirika. Uumbaji wote ni uenezi wa nafsi na wa fumbo lake. Viumbe vyote vinaitwa kuingia katika mwendo huu wa upendo na kuwa maonyesho ya wema wake. Tumsifu Mungu kwa ushirika wake wa upendo, atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu... 

       Tunapofanya ishara ya msalaba, yaani, “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu”, tunaonyesha hisia yetu ya kuwa miliki ya Mungu na tena tunaongea kuhusu ukweli wa Mungu, ambaye yupo hapa na katika kila mahali. Yeye yu upendo aliye juu ya vyote na ndani ya vyote. Hivyo, anapatikana kwa wote lakini yeye ni fumbo daima kwa sababu hakuna lolote ambalo liweze kuweka mipaka kwako. Kulingana na Mtakatifu Agustino, “Mungu ni wa milele mno hata wakati yeye anapopatikana kuna yote ya kupatikana bado.” Kuna hadithi fulani ya Mtakatifu huyo ambayo inatusaidia kutafakari fumbo la Utatu Mtakatifu kama fumbo si la kufahamiwa bali la kukaribishwa. Ikiwa tunajifungua zaidi kwa fumbo hili tunaweza kuhisi zaidi tendo lake ndani yetu.

    “Siku moja Mtakatifu Agustino, aliye mchungaji na mwalimu wa kanisa, alikuwa akitembea katika pwani ya bahari, akijiuliza swali kuhusu fumbo la Utatu Mtakatifu, akisema, “inawezekanaje Mungu kuwako kama Mmoja na Utatu wakati huo huo?” Ghafla, alimwona mtoto mdogo aliyefanya shimo katika mchanga na kukimbia kwenye bahari, akachukua maji kidogo na kuyaweka shimoni. Baada ya kuangalia mchezo huu wa mtoto mdogo kwa mara nyingi, Agustino aliamua kumwuliza maana ya mchezo huo. Mtoto mdogo akamjibu akisema: “Najaribu kuweka maji yale yote ndani ya shimo hii”. Ameshangaa sana, Agustino akasema: “Hutapata kufanya hivyo kamwe!” Kisha, mtoto mdogo akamwambia akisema: “ni rahisi kwangu kuyaweka maji yale yote shimoni kuliko wewe upate kufahamu fumbo la Utatu Mtakatifu kwa akili yako. Mwishowe, mtoto mdogo alitoweka na Mtakatifu Agustino akajiambia: “Labda mtoto huyo angeweza kuwa ni malaika!”

         Ujumbe wa masomo ya siku ya leo unatusaidia kujifungua kwa fumbo hili. Kwa mfano, somo la kwanza linaongelea Mungu aliye karibu, ambaye anajifunua katika hali yetu ya kawaida kwa ishara ndizo halisi sana. Kuwa naye uhusiano wa mwana na imani ndiyo njia kamili ya kupata furaha na maisha mengi. Somo la pili linachukua tena hali ambayo tulitafakari wiki iliyopita, yaani tumepokea Roho ambaye anatufanya kuwa wana. Tendo la Roho ndani yetu anathibitisha kwamba sisi tu wana wa Mungu, na Yesu “hana aibu ya kuwafikiria kama ndugu wale ambao aliwatakasa”. Utakaso huu unamaanisha kuhusishwa katika ushirika mmoja ambao yeye anaishi pamoja na Baba, ushirika wa Mungu ambaye hajui kufanya jambo lingine isipokuwa kupenda.   

       Wanafunzi waliitwa na Yesu kuenda pamoja kwenye mahali fulani huko Galilaya. Kutoka mahali  huko walitumwa pamoja tena kuinjilisha kwa sababu ushahidi wa kwanza wa jumuiya ya wanafunzi wa Yesu ni umoja utakaohakikishwa na Roho yake. Kila mtu anaitwa kuweka juhudi kwa ajili ya kuusaidia umoja huu kama maana ya utambulisho. Tumezipokea zawadi kutoka kwa Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi na kuendeleza kuujenga mwili mmoja, ambao ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake. Hivyo, uwepo wa Yesu ni muhimu sana kwa ajili ya nguvu na ufanisi wa wanafunzi wake, kwa maana mwili bila kichwa unakufa. Siku moja alisema, “Bila mimi hamuwezi kufanya chochote”.

      Ndiye Yesu peke yake na mamlaka aliyopokea kutoka kwa Baba ya kudhihirisha mpango wake wa wokovu. Alishiriki mamlaka haya na wanafunzi wake kwa ajili ya kufanya wanafunzi wapya miongoni mwa watu. Wanafunzi  walitumwa kama wajumbe wa habari njema kwa wanadamu wote kwa sababu injili haina mipaka. Yesu aliwaahidi kuandamana nao mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa mwili hauonekani tena, Roho wake anahakikisha ukaribu wake katika safari yao kwa sababu kama Yesu alitenda pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, vivyo hivyo Roho huyo anatenda pamoja na Yesu na Baba. Ikiwa wanafunzi wanaruhusu kuongozwa na Roho huyo wanaweza kuwashirikisha wengi katika mpango wa Yesu ulio mpango wa Utatu Mtakatifu. Kuwa mwanafunzi wa Yesu ni kuwa makao ya Utatu Mtakatifu.

       Ujumbe wa uhusiano wa Utatu Mtakatifu ni msaada mkubwa ambao Ukristu unatoa kwa jamii yetu ambayo inaongozwa kwa njia ya ubinafsi na mashindano. Yesu alitukabidhi ujumbe wa upendo kama maana ya mambo yote. Tunaweza kuonyesha ukweli wa ujumbe huu ikiwa tunaishi kuungana naye (na  Utatu). Siku moja alisema “wote wawe na umoja; kama wewe Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kusadiki.” Tunapoishi kwa uhusiano wa ndani na Yesu vivyo hivyo tunahisi ndani yetu tendo la Baba na Roho wake. Uzoefu wetu wa Yesu katika Ekaristi ni tena uzoefu wa Utatu Mtakatifu. Kulingana na fumbo hili, Mungu anatumikia, yeye yupo kati yetu na tena ndani yetu. Ndiye yeye mwenyewe anayetuunganisha naye na miongoni mwetu. Anafanya hivyo kwa sababu anataka tuwe washiriki katika uhai wake mwenyewe. Kwa hivyo, tuombe “Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mt...

Fr Ndega


Nenhum comentário: