sábado, 16 de junho de 2018

UFALME WA MUNGU NDIO KAMA MBEGU



Kutafakari kuhusu  Ezekieli 17: 22-24; 2Wakorinto 5: 6-10; Marko 4: 26-34


         Kiini ya liturjia hii ni uwepo wa kimya na ufanisi wa ufalme wa Mungu miongoni mwetu. Mungu anafanya mambo yote kwa wema wetu na kutarajia tumwamini yeye kuliko nguvu zetu.

       Somo la kwanza linaongea kuhusu hali ya utumwa wa Babeli katika mwaka wa 597 K.K. na kumjulisha Ezekieli kama mmoja wa manabii aliyeandamana na watu wa Israeli katika kipindi hiki kigumu. Watu waliishi hali ya kuchanganyikiwa katika maisha yao bila matarajio ya mabadiliko. Lakini pamoja mwao alikuwako Ezekieli aliyewaimarisha kama mjumbe wa Mungu. Kulingana na nabii huyo, Mungu hakuwasahau; yeye yupo miongoni mwao na kuwaokoa, akiwaletea maisha mapya na kuwafanya kuwa rejeo kwa ajili ya kutangaza wema wake kwa mataifa yote. Katika mwendo huu wa ukombozi watu walinganishwa kama mmea mdogo utakaokuwa mti mkubwa. Basi, Mungu atachukua watu wake waliodhulumiwa na kuaibishwa, atawainua kama chombo cha wokovu wake. Njia hii ya Mungu ya kutenda inakumbukika katika wimbo wa Bikira Maria: “Bwana amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, na akawakweza wanyenyekevu”.

       Kulingana na Mtakatifu Paulo, sisi ni kama wageni, watu waliohamishwa ulimwenguni huu, mbali sana kutoka makao yetu. Sisi ni wa Mungu nasi hatuwezi kuridhishwa kwa ulimwengu huu, kwa sababu zawadi kuu ya imani ambayo tumepokea kutoka kwake inautoa mwelekeo kamili kwa maisha yetu ili tufikie marudio salama katika Mungu mwenyewe. Zawadi ya imani inatuimarisha kuchukua utambulisho wetu wa Kikristo kwa kutenda pamoja na Kristo ambaye anatungojea ili kututuza kulingana na chaguzi ambazo tumefanya katika dunia hii. Sisi sote tunaalikwa kwa maisha mapya ambayo Mungu anatupatia kwa neema yake, lakini bila kutenda kulingana na mapenzi yake, maisha mapya hayawezekani.

        Katika injili Yesu anaongea kwa watu kwa kutumia mifano ili kutueleza kuhusu nguvu ya Ufalme wa Mungu. Mfano wa kwanza ni kuhusu mbegu ambao unaota na kukua kwa nguvu yake mwenyewe; ushiriki wa binadamu ni kuupanda tu na kusubiri wakati wa mavuno ili kukusanya matunda. Wa pili ni kuhusu udogo wa kipimo cha mbegu ya haradali na ukuu wa matokeo yake. Kwa nini Yesu aliongelea watu akiitumia mifano? Chaguo la Yesu kwa njia hii ya kuongea ni kwa sababu yeye alijitambulisha na hali ya watu wanyenyekevu na tena akitumia vipengele vya hali hii ilikuwa ni halisi ili watu wafahamu ujumbe wake. Hivyo, kwa njia ya Yesu ya kuongea, mafumbo makubwa ya Ufalme wa Mungu yalipatikana kwa watu walio wadogo na wanyenyekevu.

     Katika ujumbe wake, Yesu hakujitangaza mwenyewe; yeye aliutangaza Ufalme wa Mungu. Ufalme ni kiini ya ujumbe wake. Kulingana na Yesu, hali na nguvu ya Ufalme wa Mungu haitegemei juhudi za binadamu, bali hiki ni tendo la neema ya Mungu inayotolewa kwa hiari. Kila mtu anaalikwa kutoa uwezo wake ili kusaidia kuujenga kwa Ufalme wa Mungu duniani, lakini ufalme huu ni kwanza tendo la Mungu nao unamtegemea yeye sio binadamu. Kwa upande wetu ni vizuri kutenda kama Mt. Yohana Calabria aliyechukua kama ahadi kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake kupitia imani na kujisalimisha kabisa kwa riziki ya Mungu Baba. Mfano wake unatusaidia kufahamu kwamba hakuna kipaumbele kingine katika maisha yetu ili tuweze kupata furaha kamili.

      Watu wengi miongoni mwetu ni wakulima na mifano hii pamoja na kuwa mafundisho kuhusu hali ya Ufalme wa Mungu, tena ndiyo msaada ili waendelee kwa shughuli zao za kila siku kwa uvumilivu na imani katika tendo la Mungu. Mifano hii inatualika kuangalia mwendo wa ongezeko la mashamba katika uwanja, hasa kuhusu mahindi na maharagwe. Sisi sote tunajua kwamba baada ya kazi ya kwanza ya kupanda tunaitegemea mvua na nguvu ndani ya mbegu. Hiki ni kitendo cha Mungu anayethamini juhudi ya binadamu kama ushiriki katika uumbaji na kutubariki kwa mavuno mengi. Tumshukuru Mungu kwa nguvu ambayo anatupa ili kufanya kazi kwa uaminifu naye aendelee kutupatia Baraka zake kwa manufaa ya familia zetu.

Fr Ndega



Nenhum comentário: