domingo, 27 de agosto de 2017

TUMEJENGWA JUU YA MSINGI WA MITUME


Tafakari kutoka Is 22, 19-23; Rom 11,33-36; Mt 16, 13-20



       Kama Wakristo, tumejengwa juu ya msingi wa mitume, yaani imani yetu ilianza kwa kukiri kwa imani ya mitume. Ingawa sisi tu tofauti, utambulisho wetu ni kuwa wamoja. Ndio ubatizo wetu umetuunganisha na Kristo kwa ajili ya kujenga mwili mmoja na kuishi kwa uaminifu Agano ambalo Mungu alifanya nasi tulio watu wake.

     Katika somo la kwanza, kwa sababu ya kosa la uaminifu wa Shebna, Mungu atamchagua Eliakimu na kumpa mamlaka ya kuwatawala watu wake. Kulingana na mpango wa Mungu kwa watu wake, kiongozi huyo atakuwa  kama baba aliye na ufunguo wa mti kwa ajili ya kuwatunza watu na kuzaa hali ya utulivu na kuamini. Kupitia watumishi wema na wanyenyekevu Mungu anaendelea kuwaongoza na kuwatunza watu wake. Kulingana na somo la pili, Mungu anafanya mema yale anayofanya kwa sababu anatenda kwa hekima na upendo. Kwa upande wetu, ni lazima kufungua moyo kwa kupokea msukumo wake ili tutende kama yeye alivyo.  

        Yesu alikuwa anatembea pamoja na wanafunzi wake na walipofika eneo la Kaisarea Filipi yeye aliwauliza maswali kuhusu utambulisho wake kulingana na mtazamo wa watu. Hii ilikuwa nafasi nzuri ya kuwafundisha vizuri kuhusu utambulisho wake wa Masiha wa Mungu. Jibu la kwanza linadhihirisha kwamba watu hawakuwa na wazo kamili kuhusu Yesu na walifikiri kwamba ilitosha kumlinganisha na manabii wa zamani. Kwa maneno mengine walikuwako mbali na matarajio ya Yesu. “Kumwita Yesu nabii ni nusu tu ya ukweli wote. Manabii huandaa njia kwa ajili ya mtu mwingine. Lakini Yesu pekee ndiye ambaye njia yake iliandaliwa na manabii wengine wote.” Ingawa kwa watu mawazo kuhusu Yesu hayakuwa wazi, kwa mitume yapaswa kuwa tofauti, maana kwa Yesu si muhimu yale ambayo watu wanafikiri, bali kukiri kwa wafuasi wake.

      Kwa hivyo, Yeye aliwauliza akisema, “Na ninyi, Je, mnasema mimi ni nani?” Jibu la Petro alidhihirisha yale ambayo wanafunzi wengine kumi na mmoja walijua pia: Yesu ni Masiya wa Mungu. Lakini hawawezi kutangaza habari hii kwa sababu ya kutokuwa na maana kamili. Mawazo yao kuhusu Masiya yalifuata matarajio ya Wayahudi wengine, yaani, Masiya wa kisiasa atakayetumia nguvu zake za kimungu ili kuwakomboa Wayahudi toka ukoloni wa Warumi. Bila shaka kwamba Yesu aliyakanusha mawazo hayo akionyesha njia tofauti ya kutimiza ujumbe wake wa Masiya. Masihi ambayo Yesu alichagua ni ile ya mtumishi wa Bwana aliye makini kwa sauti ya Mungu na kufanya mapenzi yake kwa njia ya mateso, kufa na kufufuka.

      Ingawa jibu la Petro lilikosa maana kamili, Yesu aliutambua ufunguzi wa Petro kwa msukumo wa Mungu. Msukumo huu ulimsaidia Yesu ili kumpa Petro nafasi ya uongozi kati ya mitume. “Yeye ni sawa na wenzake lakini ana tofauti fulani. Kukutana na Kristo kumbadilisha Petro sana mpaka anapewa kazi hii maalumu. Hasemi kwamba yeye ni tofauti na wenzake. Tena atamkana Yesu (Mt 26:33) lakini anatubu (Mt 26:69-75) na anarudishwa tena kwa kazi yake hiyo (Yoh 21:1-19).” Hivyo, Petro alipokea kazi hii sio kwa sababu alistahili, bali kwa imani yake thabiti na imara ndiyo mwamba. Imani ya Petro na ya mitume wengine ni maonyesho ya uamuzi wa kuyatoa maisha yao kwa ajili ya Kristo. Imani hii ndiyo msingi wa imani yetu kama Wakristo.


    Jukumu la Petro na mitume wengine limerithiwa na Baba Mtakatifu Francisco na maaskofu wote. Kama Yesu alitambua mkono wa Baba na tendo la Roho Mtakatifu katika Petro, tena anatambua tendo hili katika waandamizi wao wote na kuandamana nao ili kazi yao ionyeshe utunzaji na upendo wa Mungu kwa watu wake. Ingawa wana jukumu la kuliongoza kundi la Yesu, wanashiriki pamoja nasi katika kundi moja. Imani yao thabiti na imara inathibitisha imani yetu na kutuhakikishia umoja yetu katika Kristo. Kwa upande wetu ni lazima usikivu na ushirika na wachungaji wetu kwa ajili ya manufaa ya Kanisa zima. Utume wa upendo na wa unyenyekevu wa wachungaji pamoja na utiifu wa wana kondoo uwe daima maonyesho ya Kanisa la kweli la Kristo.

Fr Ndega

Nenhum comentário: