sexta-feira, 1 de setembro de 2017

MWANAFUNZI WA KWELI NDIYE YULE ANAYEJITOA KAMA MWALIMU WAKE ALIVYO


Kutafakari kutoka Yer 20, 7-9; Mt 16, 21-27


          Ujumbe wa masomo haya unatuimarisha sana kwa sababu ingawa sio rahisi kufanya kazi kwa ajili ya watu wa Mungu, lakini ndiyo nzuri. Uaminifu wa Mungu ndio maana ya uvumilivu wetu tulio watumishi wake. Ikiwa tunapata kufanya mapenzi yake tuko na uhakika kwamba tutakuwa washindi wakati wa mazingira magumu katika safari yetu. Huu ndio uzoefu wa Yeremia. Yeye ndiye nabii aliyeteseka kwa sababu ya uaminifu wake kwa Yule aliyemwita awe nabii. Yeye aliishi wakati wa mgogoro katika kazi yake kwa sababu ya upinzani dhidi ya maneno yake na hatari kwa maisha yake. Alikuwa karibu ya kukata tamaa kwa sababu ilionekana kwamba alifanya kazi bure, yaani bila maana, lakini uhusiano alioishi na Mungu ulimwimarisha kusimama mwaminifu na mshindi. Upendo wa Mungu kwa Yeremia ndio kama moto inayochoma ndani yake na kuizaa hamu kwa ajili ya Mungu.

      Andiko la injili ni mwendelezo wa lile ambalo Yesu aliwauliza wanafunzi kuhusu utambulisho wake kulingana na mtazamo wa watu. Majibu yalikuwa ishara ya kwamba mawazo kuhusu Yesu hayakuwa wazi sana kwa upande wa watu. Lakini Yesu alitaka kujua jambo hili kwa upande wa wanafunzi wake, kwa sababu kwa Yesu si muhimu yale ambayo watu wanafikiri, bali muhimu ni kukiri kwa wafuasi wake. Petro alisema yale ambayo wanafunzi wengine kumi na mmoja walijua pia, yaani Yesu ni Masiya wa Mungu. Lakini yeye aliwakataza ili watangaze habari hii kwa sababu ya kutokuwa na maana kamili. Yesu alitambua kwamba wafuasi wake wakahitaji ufunuo zaidi na kujifunza vizuri maana ya Masihi yake na masharti kwa kumfuata kwa kweli.

            Ni jambo la ajabu kwamba yule Simoni aliyeruhusu kuongozwa na msukumo wa Mungu na kuwa Petro aliye mfano wa umoja wa Kanisa, tena kwa haraka aliruhusu kuongozwa na shetani. Hilo linamaanisha kwamba ingawa wanafunzi wa Yesu wanaongozwa na Mungu, kuna nguvu za ndani ambazo zinawaongoza kumpinga Mungu. Kweli mawazo ya wafuasi wa Yesu kuhusu Masiya yalifuata matarajio ya Wayahudi wengine, yaani, masiya wa kisiasa atakayetumia nguvu zake za kimungu ili kuwakomboa Wayahudi toka ukoloni wa Warumi. Bila shaka Yesu aliyakanusha mawazo hayo akionyesha njia tofauti ya kutimiza ujumbe wake wa Masiya, yaani kupitia mateso, kifo na kufufuka. Uamuzi wa Yesu ni kulingana na mpango wa upendo wa Baba yake aliyeupenda ulimwengu mno hata alimtoa Mwana wa pekee ili kila mtu asipotee bali awe na uzima wa milele. Basi, kumfuata Yesu kupitia njia aliyochagua ni kutenda kulingana na mapenzi ya Mungu.

        Wanafunzi wa kwanza walihitaji mwendo mrefu ili kujifunza kumhusu Yesu na kuyafahamu mapendekezo yake sawasawa. Kidogo kidogo walitambua kwamba kwa kujitoa kama Yesu alivyo, walipaswa kuzifuata hatua tatu, yaani, kujikana wenyewe, kuichukua misalaba yao na kumfuata Yesu. Kwa maneno mengine, walipaswa kubadilisha njia yao ya kuishi na kufikiri. Hivyo, wale ambao hukutana na Yesu hawabaki walivyo wala hawawezi kumdai Yesu atende kulingana na njia yao ya kufikiri. Mwendo unapaswa kuwa tofauti. Mawazo ya Yesu ni tofauti na mwelekeo wa ulimwengu, yaani mtu anayetaka kuwa wa kwanza anapaswa kuwa wa mwisho; tena ikiwa anataka kuwa mkubwa anapaswa kuwa mtumishi wa wote; tena ikiwa anataka kuiokoa nafsi yake anapaswa kujitoa kwa ajili ya Kristo na injili. Kwa maneno mengine, kulingana na Yesu, ni lazima kufa kwa kuishi.

          Basi, ili tuwe wanafunzi wa kweli tunapaswa kupitia kwa mwendo wa kufa kwa nafsi yetu kila siku. Kwa kumfuata Yesu kwa kweli tunapaswa kupatikana kwa kila kitu katika jumuiya zetu. Tunapaswa kufanana maisha yetu kulingana na njia ya Yesu ya kuishi. Hali hii haileti upendeleo au hadhi, bali mateso na kujisalimisha kwa ajili yake. Yeyote anayetaka kuishi bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Mtu anayetamani kumfuata Kristo bila msalaba hatamfuata kweli kamwe. Tujiulize kidogo, Je, ni Kristo gani tumemfuata? Mawazo au kitu gani tunahitaji kujinyima bado ili tuweze kumfuata Yesu kabisa? Ujumbe huu utuimarishe kumfuata Yesu kwa uaminifu, yaani kulingana na njia aliyochagua ili mapenzi ya Mungu yafanyike.

Fr Ndega

Nenhum comentário: