domingo, 17 de setembro de 2017

MSAMAHA BILA KIPIMO WALA MPAKA


Kutafakari kuhusu Mt 18: 21-35



      Akiwaita wanafunzi ili wamfuate Yesu alikuwa akianzisha jumuiya. Akijua moyo wa kibinadamu na kukiri kwamba kuna hali ambazo zinaweza kuijenga ama kuharibu jumuiya, yeye alionyesha njia kamili ili mahusiano kati ya wanafunzi wake yawe ya kweli na kuzaa matunda mazuri. Njia ambayo Yesu alionyesha ilikuwa njia ya mazungumzo, ya msamaha na ya upatanisho. Kama hatua ya kwanza ya marekebisho ya kidugu nilipaswa kumwita ndugu aliyekosa kwa mazungumzo kati yake na mimi peke yetu. Ikiwa hatua hii haipati mafanikio inawezekana kuuomba msaada wa jumuiya. Kwa Yesu, ndugu anayekosa anaendelea kuwa ni ndugu naye anastahili kufikiriwa kama ndugu. Hali ya maisha ya ndugu fulani anayehudhuria pamoja nasi katika maisha ya kijumuiya ni jukumu letu. Tunaalikwa kutumia juhudi zote, pamoja na Yesu, ili ndugu huyo asipotee bali aokolewe.   

     Tukiendelea kwa ujumbe huu wa upatanisho, tunataka kutafakari kwa kina juu ya thamani ya msamaha kwa maisha ya jumuiya zetu. Petro alimjia Yesu na kumwuliza, akisema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Yesu alimjibu, akisema “saba mara sabini.” Yesu alitumia swali la Petro ili kuongea kuhusu mahitaji ya kusameheana bila kipimo wala mpaka kama sharti kwa kuingia katika Ufalme na pia kama njia kamili ya uhusiano mwema kati ya watu. Kama kawaida, Yesu anajulisha tabia ya Baba yake kama kipimo. Katika mfano huu, bwana wa mtumishi mbaya sana ni kama Mungu Baba. Yeye alimwonea huruma, akimsamehe lile deni na kumwacha aende. Bila shaka mtumishi huyo hastahili, lakini huruma ya bwana huyo ni kubwa zaidi kuliko hali mbaya ya mtumishi huyo wala haimtegemei. Na kama hitimisho, Yesu anawaalika wasikilizaji wake wawe na huruma kama Baba Yake alivyo, yaani, wasamehe kwa mioyo yao yote.

        Mungu anasamehe bila kipimo kwa sababu hii ni tabia yake. Akitenda hivyo, anatarajia wanadamu wawe na uhusiano mwema naye na tena kati yao. Kwa Yesu, rejeo la kutenda ni Baba daima kwa sababu angalia kwa kina lile ambalo linatokea ndani ya binadamu. Yeyote ambaye anaweza kuona ndani tena anaweza kuona vizuri. Ingawa binadamu ana udhaifu mwingi na kutenda mbaya, mtazamo wa Mungu kwake ndio wa upendo, yaani ndio mtazamo ambao anatoa nafasi ya kutenda tofauti na kuwa mwema. Kwa sababu ya mtazamo huu binadamu sio mpotevu bali ndiye mtu wa tumaini. Kulingana na Mtakatifu Yohane Calabria, “tunapaswa kuyachukia makosa bali kuwapenda waliokosa kwa maana ndio ndugu zetu.” Hata wakati wanapotukosea mara nyingi, kulingana na swali la Petro, tunaalikwa kuwapenda.

       Basi, andiko hili ni mwaliko wa kuifuata tabia ya Baba anayesamehe daima bila kufikiria aina ama kiasi cha dhambi zetu. Msamaha ni maana ya sikukuu na furaha kwa sababu unasababisha uzoefu wa ukombozi kwa mtu ambaye anamkosea mwingine na kutubu, na pia kwa yule anapomsamehe. Mtu ambaye anasamehe ni chombo cha huruma ya Mungu na mtoto wake wa kweli, kwa sababu, kulingana na Baba Mt. Francisco, “Yesu anasisitiza kwamba huruma si tendo la Baba peke yake, bali inakuwa kipimo cha kuthibitisha nani kweli ni watoto wake. Kwa kifupi, tumeitwa kuonyesha huruma kwa sababu huruma imeonyeshwa kwetu kwanza.”


        Lakini tuwe macho kwa sababu hatuwezi kufikiri kwamba maneno ya Yesu ya “saba mara sabini” ni mwaliko ili tuendeleze kukosa na kutarajia kwamba wengine wapatikane kutusamehe daima. Huu ndio mwaliko ili tuache njia ya dhambi, kwa sababu matokeo ya uzoefu wa kweli wa huruma ya Mungu, hasa kupitia Sakramenti ya Kitubio ndiyo mabadiliko ya maisha. Kupitia sakramenti hii, anasema tena Baba Mt. Francisco, “Mungu anakuja kutusaidia katika udhaifu wetu... tukiguswa na huruma yake, tunaweza pia kuwa na huruma kwa wengine”. Tunaalikwa kuishi kama tulioguswa na huruma, yaani tuliosamehewa kwanza. Msamehe ni zawadi ya Mungu. Wakati tunaposamehe tunaonekana na Mungu na kupata kufikia matarajio yake ya Baba Mwema.   

Fr Ndega

Nenhum comentário: