domingo, 6 de agosto de 2017

“KUPANDA MLIMANI” KWA KUGEUKA SURA KATIKA MAISHA YA KILA SIKU


Tafakari ya Mt 17, 1-9


         Siku sita baada ya kuwasilisha masharti ya kumfuata, Yesu aliwaalika wanafunzi wake kupanda mlimani. Jambo la Mlima ni muhimu sana katika Injili ya Mathayo. Mwinjilisti huyo anaandika kwa Wayahudi na kwa hivyo, nia yake ni daima kumjulisha Yesu kama Musa mpya. Mlima katika Biblia ni mahali pazuri kwa ajili ya uzoefu wa Mungu. Hasa katika injili hii mlima unatajwa sana kwa sababu ni rejeo katika matukio makubwa ya maisha na utume wa Yesu. Tangu mwanzo wa maisha ya umma mpaka kupaa kwake, Mathayo anaongea kuhusu milima 7. Namba 7 inatusaidia kuelewa umuhimu wa mahali huko katika uzoefu wa ufunuo wa Yesu kama Mwana mpendwa wa Mungu.

      Tunataka kwa kifupi kukumbuka kidogo matukio ya milima hii 7 kwa kusisitiza yale ambayo tumesema, yaani Mlima wa majaribu - wakati wa majaribu, Yesu aliletwa kwenye mlima juu sana ambapo yeye alithibitisha uaminifu wake kwa mpango wa Baba (Mt 4,8s). Mlima wa Heri nane – Yesu alienda mlimani wakati alipotangaza kwa mara ya kwanza Ufalme wa Mungu (Mt 5). Mlima ya maombi - baada ya kuzidisha mikate na samaki kwa mara ya kwanza, yeye alipanda mlimani peke yake ili kusali (14:23). Mlima vya kuzidisha mikate – hali hii inatukumbusha tukio la Heri, yaani, Yesu alipanda mlimani na huko aliketi; umati mkubwa ukakusanyika karibu naye (15,29s). Mlima wa Golgotha (27), Mlima wa kupaa mbinguni (28) na katika sura ya 17 tuko na Mlima wa Kugeuka sura.

         Kisha, Yesu aliamua kuchukua baadhi ya wanafunzi na kwenda pamoja kwenye mlima mrefu. Kulingana na desturi ya Kikristo, mlima huu unaitwa Tabor. Huko mlimani Yesu aligeuka sura mbele yao. Hakika Yeye alikuwa kama kawaida lakini uzoefu huu ulibadilisha mtazamo wao kuhusu mwalimu. Yesu aliwaonyesha kidogo utukufu wake na hali ijayo ya maisha ya wale wanaomfuata kwa uaminifu. Yesu aliwaalika kwa uzoefu wa juu ili waone kwa mtazamo wa juu na kuweza kuona vizuri hali ya kujisalimisha kwake na hali wanayoalikwa kuichukua kama ahadi na Mwalimu wao.

        Uwepo wa Musa na Elia unaeleza kuhusu rejeo la ufunuo katika Agano la Kale. Wote wawili waliongea na Yesu wakionyesha kwamba hakuna kupasuka kati ya mafundisho yao na yale ya Yesu, bali uhusiano na mwendelezo. Lakini kulingana na sauti iliyosikika kutoka kwenye wingu ndiye yeye kwa uwezo wa kufundisha na kutafsiri kamili yale yaliyosemwa na mababu wa zamani. Baba alishuhudia kuhusu Mwana wake, akimweka kama rejeo la maisha yetu, yaani, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni”. Wote wanaalikwa kumsikiliza. Kusikiliza katika Biblia ni kitenzi chenye nguvu sana. Hii ni tabia kamili ya Myahudi mbele ya Neno la Mungu, akifanya mazoezi kuhusu yale aliyosikia. Basi, kusikiliza kuna uhusiano wa ndani na kushika/kutenda.

       Yesu ni ufunuo wa kipekee wa Mungu. Hakuna mwingine ambaye aweze kumdhihirisha Mungu kama Yesu alivyo. Kweli Mungu aliongea wakati wa zamani kwa mababu zetu. Lakini “siku hizi” mambo yote Mungu anayoendelea kudhihirisha kwa watu anafanya kwa Mwanawe Yesu. Hata wale ambao hawamjui Yesu wanapokea ufunuo wa Mungu kwa njia yake. Katika kila ndugu ambaye wanamsaidia wanaweza kukutana na Kristo ambaye alijitambulisha na walio na mahitaji mengi (cf. Mt 25,31-46). Kipimo ni upendo/huruma. Matendo yao ya huruma yanaongelea Kristo.


   Wanafunzi “wanatamani kubaki mlimani, lakini sauti inatoka mbinguni ikiwaalika kumsikiliza na kumtii Yesu.” Mara nyingi Mungu anatualika kufanya uzoefu wa uwepo wake kama ilivyotokea kwa wale kwenye mlima, mfano, wakati tunaposhiriki katika sherehe fulani ama siku za maombi na kadhalika. Uzoefu kama huu unaiimarisha imani yetu na hamu yetu kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kwa kawaida tunataka uzoefu huu uwe wa muda mrefu. Lakini safari yetu yapaswa kutendeka kati ya “kupanda mlimani” (mfano wa uzoefu wa Mungu wa kibinafsi) na “kushuka milimani” (mfano wa changamoto za undugu na kazi). Kila siku tunaalikwa kufanya uzoefu wa “kugeuka sura” kwa kusikiliza Neno la Yesu na kufanya mazoezi kuhusu Neno hili. Uzoefu huu unatusaidia kutambua nyuso za baadhi ya ndugu wengi kandokando yetu na kuona hisia na tabia za Kristo kwa ajili yao. “Kusikiliza neno lake kunatupatia nguvu ya kumfuata mpaka mwisho.” Hii ni njia kamili ili tuwe pia “wana wapendwa” wa Mungu.

Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: