domingo, 7 de maio de 2017

MCHUNGAJI WA KWELI NDIYE YULE ANAYELIJUA KUNDI LAKE NA KULITUNZA


Matendo 2, 14a.36-41; 1Pt 2,20b-25; Yoh 10,1-10


        Tunaadhimisha Jumapili ya Mchungaji mwema na Jumapili ya miito. Jumapili hii ni mwaliko kumshukuru Mungu kwa zawadi kuu ya wito na kumwomba ili aendelee kulibariki Kanisa lake kwa miito mingi. Pendekezo la Jumapili hili linatoka kwa baba mtakatifu Paulo wa VI. Yeye alilialika Kanisa zima kuchukua ahadi kwa ajili ya wito. Maombi kwa ajili ya miito ni pia utiifu kwa mwaliko wa Yesu ili tuombe kwa mwenye mavuno ili atume wafanyakazi kwa mavuno yake kwa sababu mavuno ni makubwa, lakini wafanyakazi ni wachache (cf. Mt 10, 37-38). Wito ni zawadi ya Mungu. Tena ahadi ya kuiombea miito ni zawadi yake. Huu ndio utekelezaji wa ubatizo wetu. Kilimo cha wito huanza katika familia na yule anayealika hutarajia jibu kwa ukarimu kutoka kwa wanaoalikwa.    

      Katika somo la kwanza mitume wanatangaza kwa shauku fumbo la pasaka ya Kristo kwa nguvu wa Mungu, kama mwaliko wa mabadiliko ya maisha. Nguvu ya maneno yao yalitoka kwa Roho Mtakatifu akitenda maishani mwao na kusababisha kutubu. Kwao kila kipindi kilikuwa nafasi mpya ya kushuhudia maisha mapya aliyotoa Yesu kwa wote hata “kwa ajili ya wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake”. Ndiye Kristo ukamilifu wa ahadi za Mungu na kupitia yeye watu wana uhakika wa kupata wokovu. Yeye ametufanya kuwa watoto wa Mungu na kutualika kuwa na uhusiano mwema na Mungu kama wana kondoo na mchungaji wao. Tukiufuata mfano wake tunaweza kuwatenda wengine mema na kuishi kama wamoja.

       Yesu ndiye Mchungaji Mwema kwa sababu anawapenda wana kondoo wake naye yuko tayari kufa kwa ajili yao. Anawajua wana kondoo wake na kuwaalika kuisikiliza sauti yake ambayo yanawaongoza kupata ukamilifu wa maisha yao. Uhusiano wa upendo kati ya Mwana na Baba ndio rejeo la uhusiano kati ya Yesu na kundi lake. Uhuru wa Yesu wa kutoa uhai wake kwa ajili ya kundi lake ni maonyesho ya upendo wake. Akitumia mfano huu Yesu anataka kuongelea uhusiano kati yake na wanafunzi wake. Msingi wa uhusiano huu ni imani, upendo, upole nao unasababisha maisha kamili kwa wafuasi wake. Kama yeye anawajua wana kondoo wake, anatarajia kwamba wako tayari kumjua na kuyafuata mafundisho yake. Kosa la kujua njia na sauti ya mchungaji ni hatari kwa sababu linaweza kusababisha mgawanyiko wa kundi na hasara ya utambulisho wa mfuasi. Njia ya Yesu ya kuongoza na kutunza ni kipimo cha walio na jukumu la kuwaongoza watu.

       Yesu ni mlango wa uhusiano mwema kati ya watu na Mungu. Mlango huu unamaanisha vipengele vitatu. Cha kwanza, Yesu ndiye njia inayotuongoza kwa Baba; uwepo wake unatuhakikishia mkutano na Mungu. Cha pili, Yesu ndiye ukweli wa Mungu kwa binadamu na ukweli wote wa binadamu kwa Mungu; “kila mtu wa ukweli humsikiliza” (Yoh 18,37) na kuruhusu kuongozwa naye kwa ajili ya kupata ukweli kamili. Yesu ndiye uhai unaotolewa kwa hiari ili kundi lake lipate maisha mengi. Katika Yesu aliye Mchungaji Mwema, Mungu anaonyesha ulinzi na utunzaji wake kwa ajili ya watu wake. Upinzani dhidi ya sauti ya Yesu ni upinzani wa kuifanya mapenzi ya Mungu na kuishi uhusiano wa upendo naye. Jibu yeye analotarajia kwa mwaliko wake siku hizi ndio uangalifu kwa msukumo wake ili tuweze kutenda kwa hekima katika mazingira yote.


      Yesu ni mchungaji mwema kwa sababu anayajua mahitaji ya wana kondoo wake na jinsi ya kuwatunza. Hakuna jambo lingine ambalo anatarajia kwa kundi lake isipokuwa maisha mengi na kamili. Wito wetu unapata mafanikio yake wakati tunaweza kutambua sauti ya Bwana kati ya sauti nyingi zinazojaribu kutuongoza. Kupitia neno lake, sakramenti na mafundisho ya wachungaji wetu Mchungaji Mwema Yesu anaendelea kuwaongoza na kuimarisha kundi lake. Tunaalikwa kuruhusu kuongozwa katika roho ya upole na ushirika. Hata sisi pia kupitia ubatizo tuko na jukumu la kuwaongoza wengine kwa kuwasaidia wachungaji wetu wafanye kazi yao vizuri. Tunaalikwa kutenda kama wanafunzi wa kwanza, ambao waliuchukua wito kwa furaha na kwa hamu kwa manufaa ya Watu wa Mungu ndilo kundi la Yesu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: