domingo, 28 de maio de 2017

KUWA MWANAFUNZI ILI KUFANYA WANAFUNZI WAPYA


Mtdo 1, 1-11; Waef 1, 17-23; Mt 28, 16-20



         Maandiko haya yanaongea kuhusu fumbo la uwepo wa Yesu. Yesu hakumwacha Baba alipokuja kwetu na hakutuacha alipomrudia Baba. Kupaa kwake Yesu kunaongea kuhusu njia mpya ya uwepo wake miongoni mwetu kwa kutangaza hatua mpya ya kazi yake. Huu ni wakati wa Kanisa, jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Ujumbe muhimu kuhusu hayo ni wazi sana katika maandiko mawili ya Luka, yaani, Injili na Matendo ya Mitume. Katika Injili yeye anajulisha vitendo vya Yesu, na andiko la Matendo ya Mitume anajulisha vitendo vya wanafunzi wake waliosaidiwa na Roho wake, aliye nguvu ya juu atauhakikisha uwepo wa Yesu miongoni mwao.   

           Mizimu ya Yesu kwa baadhi ya muda iliwaimarisha wanafunzi wake kugundua tena maana na furaha ya kuwa wanafunzi. Uzoefu huo wa kuona Yesu Mfufuka ulikuwa mpya sana kwao naye Yesu alifahamu kwamba alipaswa kuwa na uvumilivu kwa sababu ya imani yao haba. Kulingana na andiko la injili, baadhi yao waliona shaka bado. Hakika shaka hili halikuwa kuhusu hali ya ufufuko wa Yesu bali ni kuhusu uwezo wao wenyewe wa kuutangaza ukweli huu. Walikuwa kumi na mmoja kwa sababu Yuda hakuwa tena kikundini, lakini namba hii inaweza kuwa pia ya mfano, yaani kama kumi na wawili ni makabila ya Israeli, kumi na mmoja ni namba ya wanafunzi Yesu aliwatumia kwa watu wote. Walitumwa kueneza injili kwa ulimwengu kote.

        Kulingana na somo la kwanza, katika maneno ya mwisho kwao, Yesu aliwasaidia kufahamu uhusiano kati ya kila kitu alichotenda na kufundisha na hali ya Ufalme wa Mungu. Hali ya Ufalme huu ilidhihirishwa kwa ishara za Yesu na kuendeleza kwa matendo ya Kanisa mpaka miisho ya ardhi. Kabla ya kuanza kazi hii kwa dunia nzima, wanafunzi waliipokea nguvu kutoka juu. Kwa nguvu hii waliweka tayari kuwa vyombo vya wokovu wa Mungu wakifanya wanafunzi wapya kwa ajili ya Kristo. Roho mmoja aliyekuwepo mwanzoni mwa uumbaji na mwanzoni mwa kazi ya Yesu ataiongoza kazi ya jumuiya ya wanafunzi wake.

         Wanafunzi waliitwa na Yesu kuenda pamoja kwenye mahali fulani huko Galilaya. Kutoka mahali  huko walitumwa pamoja tena kuinjilisha kwa sababu ushahidi wa kwanza wa jumuiya ya wanafunzi wa Yesu ni umoja utakaohakikishwa na Roho yake. Kila mtu anaitwa kuweka juhudi kwa ajili ya kuusaidia umoja huu kama maana ya utambulisho. Tumezipokea zawadi kutoka kwa Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi na kuendeleza kuujenga mwili mmoja, ambao ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake. Hivyo, uwepo wa Yesu ni muhimu sana kwa ajili ya nguvu na ufanisi wa wanafunzi wake, kwa maana mwili bila kichwa unakufa. Siku moja alisema, “Bila mimi hamuwezi kufanya chochote”.

         Ndiye Yesu peke yake na mamlaka aliyopokea kutoka kwa Baba ya kudhihirisha mpango wake wa wokovu. Alishiriki mamlaka haya na wanafunzi wake kwa ajili ya kufanya wanafunzi wapya miongoni mwa watu. Wanafunzi  walitumwa kama wajumbe wa habari njema kwa wanadamu wote kwa sababu injili haina mipaka. Yesu aliwaahidi kuandamana nao mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa mwili hauonekani tena, Roho wake anahakikisha ukaribu wake katika safari yao kwa sababu kama Yesu alitenda pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, vivyo hivyo Roho huyo anatenda pamoja na Yesu na Baba. Ikiwa wanafunzi wanaruhusu kuongozwa na Roho huyo wanaweza kuwashirikisha wengi katika mpango wa Yesu ulio mpango wa Utatu Mtakatifu. Kuwa mwanafunzi wa Yesu ni kuwa makao ya Utatu Mtakatifu.

          Malaika wawili waliwaambia wanafunzi wa kwanza na wanatuambia siku ya leo: “mbona mmesimama mkitazama mbinguni?” Hakika kama Wakristo tunahitaji kuelekeza mtazamo wetu kwa Yesu, mfano wetu na kichwa chetu ili tuendeleze kazi yake kwa uaminifu, lakini hatuwezi Kukaa kusimamishwa kutazama mbinguni. Kama wanafunzi wake tunaitwa kuendeleza kazi yake kwa kuandaa kurudi kwake katika mwisho wa nyakati. Bwana anatutaka wenye uangalifu na fanifu kwa sababu “Wabarikiwa watumishi wale ambao watakuwa wakitumikia Bwana wao atakaporudi”. Ahadi ya Kikristo kuhusu maisha ya kibinadamu kwa kusaidia amani na upatanisho kati ya watu ni ishara ya maandalizi yetu kwa kurudi huku.

           Basi, “Maisha ya Kikristo ni njia; siyo njia ya huzuni bali ni njia ya furaha” kwa sababu pamoja na Kristo, sisi tuko katika mwendo wa kupaa mbinguni, bali kwa miguu imara katika nchi hii ya utume. Maisha ya Kikristu ni tafakari na kitendo, imani na matendo. Ishara za uwepo wa Yesu ulimwenguni zinatambuliwa kwa mapendo ya wale wanaomwamini na wanayofuata nyayo yake. Kwa ajili ya hayo tuko na msaada wa Roho Mtakatifu ambaye sio anakaa ndani yetu tu, bali anatenda pia ili atufanye kuwa kulingana na jina letu, yaani Wakristo, “Kristo mwingine”. Kwa hivyo tuseme, Uje Roho Mtakatifu!



Fr Ndega

Nenhum comentário: