domingo, 4 de setembro de 2016

KUMFUATA KRISTO KWA KUPANGA MAMBO YA KESHO


Kutafakari kuhusu Lk 14: 25-33

     Umati wa watu waliandamana na Yesu, lakini sio wote waliokubaliana naye. Alipoitambua hali ya kutokuwa na ahadi na makubaliano, aligeuka, akiwakazia macho na kuzungumza nao. Maneno yake yalikuwa nafasi ya kutafakari kwa kweli maana ya safari yao. Ingawa Yesu alikuwa maarufu, kwa sababu ya mambo mema kwa ajili ya watu, utume ambao Yesu alichukua kutimiza mapenzi ya Mungu hauleti umaarufu. Watu walichanganyikiwa kuhusu Yesu kwa sababu hawakumjua bado na kumfuata kwa njia yoyote. Kama Yesu hakuwa na nia ya kumdanganya yeyote, aliongea nao kwa uwazi sana kuhusu maana ya kumfuata na matokeo ya uamuzi huu. Kusema hivyo kulikuwa tabia yake ya kawaida kama alivyofanya kwa ajili ya wale kumi na wawili, yaani aliwajulisha masharti ili wawe wanafunzi wake wa kweli. Kutoka kwao, Yesu hakutarajia werevu ama upumbavu, bali kupatikana na hatia. Hawawezi kumfuata Yesu kwa sababu walipokea habari tu ya kuwa ni vizuri kufanya hivyo. Yesu anatarajia zaidi, mabadiliko ya ndani.

           Andiko hili ni mwaliko wa kuchukua ahadi ya kumfuata Kristo kwa kupanga mambo ya kesho, yaani kuwa na uwezo wa kuona mbele ili kutenda vizuri ama Kuwa na utoaji ili kuepuka kufaragua. Ni vizuri kuota ndoto lakini ndoto hii inapaswa kuihusu hali halisi mtu anayoishi, vinginevyo itakuwa udanganyifu tu. Yesu anataka kuepuka kwamba safari ya wafuasi wake iwe pasipo maana ama udanganyifu. Ni lazima utambuzi, hekima, kupanga na uamuzi. Mungu mwenyewe anatupa mfano wa kuwa na mipango ya muda mrefu ili tupate mafanikio katika safari yetu kama wafuasi wa Yesu. Yeye Mungu alipanga kumtuma mkombozi ndiyo maana miaka ilihesabiwa kwa kurudi nyuma maneno kabla ya Kristo (K.K) kuzaliwa yakitumika. “... wakati maalum ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke... ili apate kuwakomboa waliokuwa chini ya sheria.” (Wagalatia 4: 4-5). “Hata baadhi ya wakulima hutegemea mvua inyeshe hata kama hawajaandaa shamba mahali pa kupanda mbegu kama za mahindi au maharagwe.” Kupanga mambo ya kesho ni muhimu.

         Yesu alisema, “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Kama ilivyotekea katika vifungu vingine, Yesu aliwapendekezea watu mpango wa maisha nao mpango huu unajumuisha kujinyima, kwa sababu yeyote anayekutana na Yesu kwa kweli amekwisha pata hazina ya kweli kwa maisha yake wala hawezi kubaki alivyo, yaani mambo mengine hayana maana tena. Kwa maneno mengine, Yesu anataka kuwa kipaumbele maishani mwa wanaoamua kumfuata. Hakuna jambo lingine ambalo liweze kuitoa maana ya kweli kwa maisha yao ila Yesu mwenyewe. Wanafunzi wa Yesu wa kweli walimtegemea Mungu katika mambo yote kama Yesu alivyo. Yeye alishiriki na wanafunzi wake ufalme wa mbinguni na kuwajulisha njia ya msalaba ili waweze kufanya mapenzi ya Baba yake. Kupitia njia hii, tunatambua kwamba Kumfuata Yesu hakuuleti upendeleo au hadhi, bali mateso na kujisalimisha kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Basi, yeyote ambaye anataka kuishi shwari na bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Tena yeyote ambaye anatamani kumfuata Kristo bila msalaba hatamfuata Yeye kwa kweli kamwe.

         Kupitia njia ya unyenyekevu na utupu Yesu alipata utukufu. Kupitia njia hii utambulisho wa wanafunzi na mwalimu Yesu unatokea. Kwa upande wa Kristo msalaba ulikuwa sehemu muhimu katika mwendo wa kufanya mapenzi ya Mungu na kudhihirisha mpango wa upendo wake. Kwa upande wetu kama wanafunzi, kuchukua msalaba ni ishara ya utayari wetu kwa kuruhusu kuongozwa na Mungu na kuyakaribisha mapenzi yake kwa maisha yetu. Kwa kufikia lengo hili tunapaswa kujikana nafsi yetu, yaani kujisahau sisi wenyewe ili wengine waweze kukumbukwe. Tunapaswa kujikana ili Mungu aweze kujifunua kwa nguvu yote ya upendo wake. Kujiondoka kutoka katikati/mahali muhimu ili wengine waweze kuwa na nafasi zaidi. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuwafikiria wengine kuwa wamuhimu zaidi kuliko sisi wenyewe. Kama haiwezekani kumfuata Kristo bila msalaba, mfano wake wa uaminifu kwa mpango wa Mungu utuimarishe ili tuchukue msalaba wetu wa kila siku, kumfuata kwa uaminifu na kufanya mapenzi ya Mungu.

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Serah

Nenhum comentário: