sábado, 10 de setembro de 2016

MUNGU ANAFURAHI SANA TUNAPOMRUDIA YEYE


Kutafakari kuhusu Lk 15, 1-32

Sura ya kumi na tano ya toleo la Luka ni maarufu miongoni mwa mifano ya Yesu. Hii inaitwa sura ya Mifano ya huruma. Tuko na mifano mitatu (Kondoo aliyepotea: 4-7; Sarafu iliyopotea: 8-10; Mwana mpotevu: 11-32). Mifano hii inaonyesha tabia ya huruma ya Mungu kuhusu wenye dhambi na furaha ya kukutana tena na yule ambaye alipotea. Kwa kufahamu nia ya Yesu alipoisimulia mifano hii tunahitaji kutafakari kwanza kuhusu mazingira ambayo Yesu aliishi. Katika muktadha huo, baadhi ya watu walijiona waliostahili wokovu wa Mungu kwa sababu ya uaminifu wao kwa Sheria. Walichukua mamlaka ya kuwatenganisha watu, wakiwapanga kama wema au wabaya. Mamlaka haya hayatoki kwa Mungu kwa sababu kipimo ni ubaguzi. Walisahau kwamba mbele ya Mungu watu wote ni sawa. katika njia yake ya kupenda Mungu hambagui yeyote. Kwa upande wake watoza ushuru na wenye dhambi ni watoto wake kama vile ndio Mafarisayo na Waandishi. Ikiwa hao wanaweza kuzaa undugu, tena wataweza kuishi katika ushirika na Mungu, anayekaribisha kila mtu ili awaokoe wote.

          Ingawa yako matukio mengi katika Agano la Kale, ambayo yanaonyesha njia maalum ya Mungu ya kutenda, ni “katika Yesu Kristo kwamba huruma ya Mungu imepata kuwa hai na yenye kuonekana, na hata ilifikia kilele chake katika Yeye... Yesu ni uso wa huruma ya Baba. Kila kitu ndani yake kinaongelea huruma. Hakuna chochote kwake kinachopungukiwa na huruma (Baba Mt Francisco).”  Kama alama ya huruma ya Mungu, Yesu ana chaguo wazi sana, yaani, “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao”. Maneno haya yalisemwa na wale waliompinga Yesu. Kwa kweli, Yesu alikuwa na njia maalum ya kuongelea huruma ya Mungu, yaani katika Yesu jambo la huruma lilionyeshwa “kwa neno lake, matendo yake na kwa nafsi yake yote.” Yeye alitumia ishara nyingi za makaribisho, akithibitisha lengo la ujumbe wake na ukweli wa mafundisho yake. Kwa kweli, watozaushuru wengi, makahaba na wengine waliokataliwa na jamii, walijiona kukaribishwa na Yesu na tena kubadilishwa kwa sababu ya mkutano na huruma ya Mungu.

          Katika mfano wa mwana mpotevu, ingawa tuko na tukio la kijana mdogo na hisia za kijana mkubwa, macho yetu yamlenga baba wa vijana hawa wawili ndiye aliye mhusika mkuu wakati wote. Uhusiano wake wa mapendo kwa vijana wake, ambao wote ni wapotevu kwa njia tofauti ndio umuhimu wa tukio hili. Kulingana na Yesu, baba huyo ni kama Mungu ambaye ana watoto tofauti na kushiriki nao zawadi zake kwa njia sawa. Yeye anawapenda wote na kutaka watu wote wajione wakiwa katika familia, kushiriki kwa furaha yake kama Baba. Katika familia hii anautoa utunzaji na ulinzi ili wawe na maana nzuri ili kubaki naye daima. Wakati yeyote anapoamua kutenda kinyume naye na kubaki mbali sana naye, sio kwa maana mtu huyo hajihisi kupendwa, bali ni kwa sababu anajiona mwenye uhuru. Kama huu ni uzoefu wa upendo wa Baba: huu ni wa hiari na kuuzaa uhuru. Sisi pia tunahisi mbali sana na Mungu wakati sisi hutenda kinyume naye, yaani, tunapomkosea. Yeye anajihisi ameachwa na kusalitiwa, lakini haachi kutupenda. Kama yule baba, Mungu anashughulika sana na maisha yetu. Anakuja kututafuta ili kutupa sisi ulinzi na utunzaji wake. Kwa hivyo tunahisi majuto na kivutio cha kuishi tena uzoefu wa ushirika tumeopoteza. Ingawa mara nyingi tunakataa utambulisho wetu wa wana, kwa dhambi zetu, Mungu haukatai utambulisho wake wa Baba kamwe.

         Katika mfano huu yuko pia mwana mkubwa ambaye hajihisi mwana, kwa sababu anajiona kuwa ni mfanyakazi, wala hajihisi ndugu, kwa sababu anamkataa ndugu yake mdogo. Tabia ya huyo mwana mkubwa inaizuia furaha kamili ya Baba na ukamilifu wa sikukuu. Kumrudia Mungu ni maana ya furaha kubwa kwake. Lakini furaha yake haiwezekani kuwa kabisa ikiwa hatushiriki katika hisia zake kuhusu wengine. Hataki kwamba tuwe na wivu kuhusu njia yake ya kupenda; anataka kwamba tutende kama yeye alivyo. Kwa hivyo Yesu alisema, “Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo.” Upatanisho na wengine ni kipimo ili uhusiano wetu na Mungu uwe kweli. Hii ni njia ya kweli ya toba iliyo mwendo wa muda mrefu na huanza mioyoni mwetu. Kupitia Ekaristi hii, turuhusu kuguswa na huruma ya Mungu ili tuweze kuwa vyombo vya huruma hii kwa wale wanaohitaji msamaha wetu.

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Serah

Nenhum comentário: