domingo, 28 de agosto de 2016

UNYENYEKEVU NA UKARIMU KAMA VIPIMO VYA UHUSIANO WETU


Kutafakari kutoka Luka 14,1.7-14

        Yesu alialikwa kula chakula nyumbani mwa Mfarisayo mmoja na, kwanza kabisa, yeye alisababisha usumbufu kwa sababu alimponya mtu mmoja siku ya Sabato. Sheria ya Wayahudi inakataza hali hii, lakini Yesu anapendelea kuwajali watu kuliko kuifuata sheria ambayo haikufuata tena nia ya Mungu ya asili. Akitarajia waweze kufikiri kama yeye aliwauliza swali: “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini wao wakakaa kimya. Tukumbuke kwamba Mafarisayo na Waandishi waliondoa maana ya kinabii ya sheria, wakitafsiri kulingana na mawazo yao ya upungufu. Hao wanapenda sana kujiinua na kupendezwa. Mara nyingi Yesu alipokutana nao hakufikia mafanikio kuhusu mapendekezo yake ya maisha mapya kwa sababu wao ni wanafiki na wanapendelea kumjaribu Yesu kuliko kubadilisha mawazo yao kulingana na matarajio ya Yesu. Kwa hivyo mkutano wa Yesu nao ni maana ya mapambano/mfarakano daima.

     Yesu yupo mloni, karamuni. Injili ya Luka inaonyesha kwamba kushiriki katika milo mbalimbali kulikuwa muhimu sana kwa Yesu aliyetumia vipindi hivi kama nafasi ya kuwafundisha watu. Karamu miongoni mwa Wayahudi inathamini sana. Pamoja na maana ya uzoefu wa familia, kielelezo cha urafiki, mshikamano na hamu ya kukuwa pamoja, karamu pia ni mfano wa uhusiano wa upendo kati ya Mungu na watu wake (Hos 2:1-23, Isa 54:4-8, Eze 16:7-8). Katika mafundisho ya Agano la Kale, kushiriki katika Ufalme wa Mungu, mara nyingi hulinganishwa na kushiriki katika karamu (Isa 34:5-7, Zek 9:15,1 Nya 12:38, Zek 14:15-24). “Karamu za namna hiyo mara nyingi zilikuwa na ujumbe wa kimasiha. Zilisherehekea ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu (Isa 25: 6-8), zikaimarisha uhusiano kati ya Mungu na watu wake, na kuwaunganisha watu kati yao.” Huu ni kweli, mfano kwenye karamu ya arusi. “Upendo wa Mungu ni kama ule wa Bwana arusi, jinsi alivyolipenda na kulichagua Taifa la Israeli kama mali yake mwenyewe. Wakristo wa kwanza, walifikiria pia juu ya uhusiano wao na Kristo kama mfano (Yoh 3:39, 2Kor 11:2, Efe 5:23-32).”

         Basi, katika injili ya leo, Yesu alishangaa kwa sababu ya mashindano ya watu kwa ajili ya mahali pa kwanza katika karamu naye aliwapendekezea tabia tofauti. Kulingana na Yesu tabia ya ukarimu wao kwa ajili ya maskini na wasiojiweza ni njia ya kuonyesha kuwa upendo wa Mungu unatolewa kwa hiari kwa ajili ya watu wote. Kwa maneno mengine, karamu zinapaswa kutafakari upendo wa Mungu kwa wote. Katika karamu ya arusi mbinguni, yeye atawakaribisha wale wanaomwelekea. Katika jamii, kwa kawaida, kutafuta mahali pa kwanza, msimamo, upendeleo, umaarufu, na kadhalika huongezeka sana. Hali hii husababisha mapambano/mfarakano, chuki na ukatili. Hata katika Kanisa na jumuiya zetu tunaweza kukuta hali kama hii. Yesu alikwisha ameonya kuhusu hatari za hali hii na kufundisha unyenyekevu kama njia kamili. Unyenyekevu ni fadhila ambayo inampendeza Mungu na watu. Kuwa mnyenyekevu ni kuchukua hali ya udhaifu ya kibinafsi kushinda mwelekeo wa kuwa bora kuliko wengine. Inamaanisha kuweka vipaji vya kibinafsi kuwatumikia wengine kwa ukarimu na upendo.


        Lengo la Yesu ni kuzaa ubinadamu mpya na aina mpya ya uhusiano miongoni mwa watu. Msingi wa ubinadamu mpya ni unyenyekevu na upendo. Thamani hizi zinapaswa kusaidiwa zaidi miongoni mwetu. Kupitia utumishi wa kindugu na wa kinyenyekevu tunaweza kufikia lengo la Yesu ambaye ana mawazo tofauti na yale ya jamii. Kwake Yesu, mtu ni mkuu ikiwa yeye ni mdogo; tena mtu ni wa kwanza ikiwa yeye ni wa mwisho; pia mtu anakwezwa ikiwa yeye anajishusha. Katika jumuiya zetu za wafuasi wa Yesu muhimu sio uhusiano wa biashara bali upendo wa hiari na ukarimu, kutumikia wenzetu kama Mwalimu Yesu ambaye alikuja kutumikia na sio kutumikiwa. Maisha yake ya utumishi ni kipimo chetu. Hatuhitaji mahali pa kwanza, bali kutumikia kwanza kwa njia ya unyenyekevu na ukarimu. Tujifunze kutoka kwa Kristo aliyefahamika kama Mtumishi wa Bwana kwa namna ya kipekee, ili utumishi wetu uweze kumpendeza Mungu.   

Fr Ndega

Nenhum comentário: