quinta-feira, 18 de agosto de 2016

MOYO WETU UKO WAPI?


Kutafakari kuhusu Hek 18, 6-9; Wab 11, 1-2. 8-19; Lk 12, 32-48

Liturgia ya siku ya leo ni mwaliko wa kumwamini Mungu kwa kweli. Kwa kufanya hivyo, tuna Ibrahimu kama mfano na mwaliko wa Yesu ili wanafunzi wake wakeshe na kujiweka tayari kwa ujio wake. Somo la kwanza linaongea kuhusu usiku ule maarufu ambao Waisraeli waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui. Uhakika kuhusu uwepo na tendo la ajabu la Mungu katika safari yao uliwaimarisha watu kukesha na kungoja ukombozi wao kutoka utumwani Misri. Huu ni mwaliko wa tuwe tayari kumtambua Bwana Yesu miongoni mwetu na kumkaribisha katika nyakati zote.  Kulingana na somo la pili, katika imani sisi tu warithi wa ahadi za Mungu kwa Ibrahimu; nasi, pamoja naye, tu wasafiri na wageni juu ya nchi. Kupitia imani tunatamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Ndiye Mungu mwenyewe aliyetutengenezea mji kwa sababu hana haya ya kuitwa Mungu wetu. Pamoja na Ibrahimu na wenye haki wengine tunaalikwa kuziamini ahadi za Mungu kwa sababu ni mwaminifu yule aliyeahidi.
Katika njili Yesu aliwaita wanafunzi wake kama kundi dogo ambalo lilikuwa limepewa ufalme kutokana na ukarimu wa Mungu Baba. Katika mazingira yale, watu walioacha kila kitu na kumfuata Yesu, walikuwa wachache na hawakuwa matajiri au watu wenye uwezo. Hata hivyo, Yesu aliwaalika kuuza mali yao na kutoa sadaka kwa ajili ya walio na mahitaji zaidi. Katika njia hii wanaweza kujitajirisha wenyewe kwa Mungu kupitia uhuru wa moyo kama vile mwalimu wao alivyo. Mali yao haina maana tena kwa sababu Kristo ndiye hazina yao. Kristo mwenyewe anataka kuwatumikia kwa kushiriki nao furaha sawa anayoona katika ushirika wake na Baba. Yeye anaweka wazi kwamba kumtumainia Mungu na wala siyo mali, ni wajibu wa kila mfuasi wake wa kundi dogo, ambalo mwishowe wanaunda Kanisa lake. Mwinjili Luka alipoiandika Injili yake, Kanisa lilikuwa bado dogo, la wanyonge wasiokuwa na uwezo na hawakujulikana.
Mwaliko wa Yesu kwa kundi lake, lililo sisi sote, ni kufanya tofauti na tabia ya kutafuta usalama katika mali nyingi ama ulinzi katika wenye nguvu. “Ni hatari kwa Kanisa na viongozi wake kutafuta umaarufu na nguvu, kama vile kuwa na uwezo wa kisiasa na kuweka vitega uchumi. Wakati wote katika historia, ambapo Wakristo walitegemea serikali, wanasiasa, na faida kubwa katika biashara, Kanisa lilikuwa dhaifu na kuporomoka.” Basi, Yesu anatuangalisha tena kuhusu hatari ya mali na anatushauri tuwafadhili fukara. Tumepewa ufalme na Baba kwa sababu sisi tu kweli wake, katika Yesu. Kutokana na hii zawadi ya Mungu, tunakuta hazina yetu ya kweli na kwa hivyo ni halali kumtegemea Mungu katika mambo yote; hayo ni matarajio yake. Wakati Mungu anakuwa hazina ya kweli katika maisha yetu, na mioyo yetu ikamtukuza yeye, uhusiano mpya utaanza na kukua. Moyo wetu uko wapi? Mungu alitukabidhi ufalme wake nasi tunaalikwa kujikabidhi mikononi mwake. Huu ni ukabidhi wa makubaliano. Hii ni hali inayotupasa kuwa na imani, yaani, ile imani ya Ibrahimu na wenye haki wengine wa Biblia.

kulingana na uzoefu wa Ibrahimu, haitoshi kuamini; ni lazima kutii, kumwachia Mungu na kuruhusu kuongozwa naye hadi palipompendeza. Kuhusu uzoefu huu wa Ibrahimu, waraka wa Waebrania unatuletea ushuhuda mzuri sana, yaani, “Kwa njia ya imani Ibrahimu alitii alipoitwa ahamie nchi ambayo angepewa kuwa mali yake. Alihama bila kujua anakokwenda” (Waebrania 11:8). Kumwachia Mungu ni kuwa na imani ya Ibrahimu. Ni imani ya kumwacha Mungu aitwe  Mungu aliye Baba na Mtoaji. “Matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano na ubaba wake” (Mt. Yohane Calabria). Haya ni matarajio ya Yesu kwa maisha ya sisi sote tulio wanafunzi wake wapya na warithi wa utume wake. Yeye anakuja daima kukutana nasi na kutarajia kukaribishwa vizuri kupitia uaminifu na utayari wetu. Kama anavyoona furaha kwa kushiriki nasi ufalme wa Baba yake vile vile ataona furaha kubwa zaidi atakapokutana na wale ambao watakuwa tayari kwa ujio wake. Tukumbuke kwamba “furaha ya Bwana ni nguvu yetu.”

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Serah

Nenhum comentário: