domingo, 14 de junho de 2020

UWEPO HAI NA KWELI


Kutafakari kutoka Kum 8,2-3.14b-16a; 1Wak 10,16-17; Yoh 6, 51-58



 

      Tunasherehekea sikukuu ya Mwili na Damu Ya Kristo kilicho chakula kinachodumu milele, yaani Ekaristi takatifu. Hii ni sakramenti ya uwepo hai wa Yesu kati yetu. Asili ya sherehe hii ni Karamu ya mwisho katika Alhamisi Takatifu lakini hali ya ukimya na tafakari kwa sababu ya Ijumaa Kuu inatuzuia  kusherehekea sikukuu ya Ekaristi kwa furaha kubwa. Kwa hivyo Baba Mtakatifu Urbano wa IV katika karne ya 13 alianzisha sherehe hii ya Mwili na Damu ya Kristo. Katika sikukuu hii tunaweza kutangaza hadharani imani na upendo wetu kwa Ekaristi Takatifu na kujiona kuungana na Kristo anayefanya upya ishara yake ya upendo kwa ajili ya wokovu wetu na kutualika kwenye karamu ili tuweze kushiriki furaha yake kubwa na uzima wa milele.

     Somo la kwanza ni uthibitisho kwamba ndiye Mungu mwenyewe anayewalisha watu wake. Muda ambao Watu wa Israeli waliishi jangwani ulikuwa nafasi ya kumjua Mungu kama Mtoaji ambaye aliwapatia chakula tofauti na kile cha Misri. Walipokea Mana kutokana na ukarimu wa Mungu kwa ajili ya kufanya upya nguvu zao za kimwili na kuwaimarisha kumshukuru Mungu aliyekuwepo miongoni mwao daima.

   Kulingana na somo la pili, Mtakatifu Paulo anasema kwamba chakula ambacho Mungu anawapatia watu wake wapya ndiye Mwanawe. Yeye anatualika sote tule mwili na kunywa damu yake ili tuwe wamoja naye. Ingawa sisi ni wengi tumefanyika mwili mmoja kwa sababu ya Mkate mmoja tunaoumega ulio Kristo mwenyewe. Ndio umoja kati yetu na ahadi ya kindugu ambayo inaufanyisha ujumbe na ushuhuda wetu uwe wa kweli.    

     Katika injili Kristo aliwaalika wasikilizaji wake kuukaribisha ufunuo juu ya utambulisho wake kama chakula kilichoshuka kutoka mbinguni si kwa binadamu tu bali kwa ajili ya uhai wa ulimwengu wote. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata alimtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele (Jo 3, 16)”. Mwana anajitoa kama chakula kinachodumu hadi uzima wa milele kwa sababu ya mapenzi ya Baba aliye chemchemi ya uzima. Yeye ndiye anayesababisha uzima ndani ya kila mtu anayempokea Mwanawe.

    Tunaongea hapa kuhusu kiini cha mafundisho ya Yesu kama mwokozi na mkombozi wa ulimwengu, lakini wasikilizaji wa Yesu hawakuweza kuelewa kwa sababu walijua hali ya Yesu ya kibinadamu. Waliwajua wazazi wake, yaani Yusufu na Maria na kushiriki pamoja naye katika shule moja. Hakika hawakuweza kukubali kwamba mwenzao huyu alishuka mbinguni. Zaidi ya hayo kulingana na mawazo ya Kiyahudi mwili ni mfano wa udhaifu wa kibinadamu. Lakini ugumu wao wa kufahamu fumbo hilo haukumzuia Yesu kufunua njia yenye maana kamili kwa maisha yao.

    Yesu anaongea kuhusu uzima bila mwisho unaopatikana kwa wote. Inawezekana kuupokea uzima huu kwa kuula mwili wake na kuinywa damu yake, kwa sababu yeye ndiye uhai na huishi ndani ya wale wanaompokea. Yesu anatenda ishara hii ya upendo kwa uhuru kabisa na kulenga kukaa miongoni mwa wanadamu na ndani ya kila mtu. Hiki ndicho kipimo cha kupata uzima. Hilo ndilo fumbo la Ekaristi takatifu. Ndiyo zawadi kutoka kwa Mungu ambaye hataki kuishi mbali na binadamu.

      Ekaristi ni hazina ya kanisa na kiini cha uzoefu wake. Ekaristi inalifanya Kanisa na Kanisa linaishi kwa sababu ya Ekaristi. Kulingana na Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa pili, “matendo yote ya Kanisa yatoka kwa Ekaristi na kulenga Ekaristi”. Ndivyo hivyo kwa sote tunaoumega mkate mmoja na kunywa kikombe kimoja. Uzoefu huu ni ukamilifu wa ushirika wetu na Mungu na msukumo kwa ahadi yetu ya kindugu.

     Yesu ndiye chakula ambacho Mungu alitupa na kuendelea kutupa ili tuwe na maisha kamili. Kutoka Umwilisho wa Neno mpaka msalaba na Ufufuko, maisha ya Yesu yalikuwa kujitolea daima kama chakula cha Mungu kwa ajili ya maisha ya watu wake. Ekaristi takatifu tunayosherehekea inatuhakikishia kwamba ukarimu wa Mungu haumaliziki, kweli utaendelea hata milele. Kila siku Kristo hufanya upya ishara yake ya upendo kwa ajili ya wokovu wetu.

      Ndiye Yesu mwenyewe ambaye anatualika kwa karamu ya uzima, akijitoa kama chakula na kututumikia kama Yule ya pekee ambaye anaweza kujaza moyo wetu unaomtamani Mungu na uhai wake sawa. Lengo la Ekaristi ni kufananisha maisha yetu kidogo kidogo kulingana na maisha ya Yule tunayepokea.

      “Tunapokula chakula cha kawaida mwili wetu unaingiza chakula hiki ili uwe na afya nzuri. Hivyo, chakula kinaingizwa na mwili wetu. Kuhusu Ekaristi, chakula cha uzima, matokeo ni tofauti: wakati tunampokea Yesu, ni sisi tunaoingizwa naye”. Kwa maneno mengine, Yesu anatuingiza, anatuchukua kwake ili tuishi naye na kwa sababu yake. Yeye anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Yeye anatuunganisha naye, kutuhusisha katika ushirika sawa anaoishi na Baba. Katika uzoefu huu tunabadilika kuwa yule tunayempokea kwa ajili ya ukuaji wa mwili mmoja. Hivyo, wakati tunaposherehekea Ekaristi kwa kina mahusiano kati yetu yabadilika na kupata nguvu na sisi tunakuwa vyombo vya umoja, upatanisho na amani kulingana na hisia za Kristo.

Fr Ndega


Nenhum comentário: