sexta-feira, 13 de setembro de 2019

FURAHA YA KUSAMEHE NA KUSAMEHEWA



Kutafakari kuhusu Lk 15, 1-32




Sura ya kumi na tano ya toleo la Luka inajulikana sana miongoni mwa mifano ya Yesu. Hii inaitwa sura ya Mifano ya huruma. Tuko na mifano mitatu, yaani mfano wa Kondoo aliyepotea (4-7), wa Sarafu iliyopotea (8-10) na Mwana mpotevu (11-32). Mifano hii inaonyesha tabia ya huruma ya Mungu kwa wenye dhambi na furaha ya kupata tena kitu kilichopotea. Kwa kufahamu nia ya Yesu alipoisimulia mifano hii tunahitaji kutafakari kwanza kuhusu mazingira ambayo Yesu aliishi.

Katika muktadha ule, baadhi ya watu walijiona waliostahili wokovu wa Mungu kuliko wengine kwa sababu ya uaminifu wao kwa Sheria. Walichukua mamlaka ya kuwatenganisha watu, wakiwapanga kama wema au wabaya. Mamlaka haya hayatoki kwa Mungu kwa sababu kipimo ni ubaguzi. Walisahau kwamba mbele ya Mungu hakuna yeyote aliye na haki kuliko mwingine. katika njia yake ya kupenda Mungu hakuna ubaguzi. Kwa upande wake watoza ushuru na wenye dhambi ni watoto wake kama vile ndio Mafarisayo na Waandishi. Kipimo cha kuishi kwa ushirika na Mungu sio sheria bali uzoefu wa undugu.
        
         Ingawa yako matukio mengi katika Agano la Kale, ambayo yanaonyesha njia maalum ya Mungu ya kutenda, ni “katika Yesu Kristo kwamba huruma ya Mungu imepata kuwa hai na yenye kuonekana, na hata ilifikia kilele chake katika Yeye... Yesu ni uso wa huruma ya Baba. Kila kitu ndani yake kinaongelea huruma. Hakuna chochote kwake kinachopungukiwa na huruma (Baba Mt Francisco).”  Kama alama ya huruma ya Mungu, Yesu ana chaguo wazi sana, kulingana na maneno ya waliompinga yeye, yaani “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao”.

       Kweli, Yesu alikuwa na njia maalum ya kuongelea huruma ya Mungu, yaani katika Yesu jambo la huruma lilionyeshwa “kwa neno lake, matendo yake na kwa nafsi yake yote.” Yeye alitumia ishara nyingi za makaribisho, akithibitisha lengo la ujumbe wake na ukweli wa mafundisho yake. Kwa kweli, watozaushuru wengi, makahaba na wengine waliokataliwa na jamii, walijiona kukaribishwa na Yesu na tena kubadilishwa kwa sababu ya mkutano na huruma ya Mungu.

      Mfano wa mchungaji anayepoteza kondoo wake tuko na ishara ya Mungu Baba ambaye ana macho maalum kwa kila mtu naye hapumziki mpaka kukutana na aliyepotea na kumhusisha tena katika ushirika wake. Katika mfano wa sarafu iliyopotea Mungu ni kama mama mmoja anayetumia juhudi na nguvu zote ili kukuta kitu alichopoteza naye anapopata hiki anafanya sikukuu. Katika mfano wa mwana mpotevu, macho yetu yamlenga baba aliye mhusika mkuu wakati wote. Uhusiano wake wa mapendo kwa vijana wake ndio umuhimu wa tukio hili. Kulingana na Yesu, Mungu ni kama baba mmoja aliye na watoto wawili na kushiriki nao zawadi zake kwa njia sawa. Yeye anawapenda wote na kutaka wajione katika uzoefu  wa familia kwa kushiriki katika furaha yake ya baba. Utunzaji na ulinzi wake ni maana nzuri ili wabaki pamoja naye daima.

    Yule ndogo alichukua nafasi ya kuenda zake akiacha ushirika wa baba yake. Yeye alifanya hivyo sio kwa sababu hajihisi kupendwa bali kwa sababu alihisi mwenye uhuru. Ndio hivyo uzoefu ya upendo wa Mungu Baba, yaani unaheshimu kila mtu na kumruhusu kuchagua kwa uhuru kabisa njia yenyewe ya maisha yake. Tunapotenda dhidi ya Mungu kupitia dhambi, Yeye anajihisi ameachwa na kusalitiwa, lakini hashindwi kutupenda. Yeye anashughulika sana kwa ajili ya maisha yetu kwa kutupa ulinzi na utunzaji wake. Kwa hivyo kwa kufikiria upendo wake kwetu tunahisi majuto na hamu ya kurudi tena kwake. Ingawa tunashindwa kuishi kama wana, Mungu hashindi kuishi na kutenda kama Baba mwema kamwe.

       Katika mfano huu yuko pia mwana mkubwa ambaye hajihisi mwana wala ndugu. Kosa la utoto ni kwa sababu anajiona kuwa ni mfanyakazi; kosa la undugu ni kwa sababu anamkataa ndugu yake mdogo. Tabia ya huyo mwana mkubwa inaizuia furaha kamili ya baba na ukamilifu wa sikukuu. Kumrudia Mungu ni maana ya furaha kubwa kwake. Lakini furaha yake itakuwa kubwa zaidi ikiwa wale ambao wanajiona watoto wake waweze kushiriki katika hisia zake kuwahusu wengine. Hataki kwamba tuwe na wivu kuhusu njia yake ya kupenda bali tutende kama yeye alivyo. Kwa hivyo Yesu alisema, “Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo.” Upatanisho na wengine ni kipimo ili uhusiano wetu na Mungu uwe kweli. Hii ni njia ya kweli ya toba iliyo mwendo wa muda mrefu na huanza mioyoni mwetu. Turuhusu kuguswa na huruma ya Mungu ili tuweze kuwa vyombo vya huruma hii kwa wale wanaohitaji msamaha wetu.

Nenhum comentário: