sábado, 8 de setembro de 2018

TUFANYE MAMBO YOTE VEMA



Kutafakari kutoka Isaya 35:4-7; Yak 2:1-5; Mk 7: 31-37


       Katika andiko la kwanza, nabii Isaya anatangaza wakati ujao umejaa tumaini kwa sababu Mungu atatembelea watu wake kama mwokozi na kuwatendea mambo makuu. Hali yote kandokando yao na miongoni mwao itabadilika kuwa ni nzuri, hasa hali ya maskini na wengine walio na shida ya afya. Ahadi hii ya kimasiya, Mungu alitimiza duniani kupitia Mwanawe Yesu Kristo ambaye aliwapa wote uwezo wa kuishi maisha mapya na mazuri.

      Katika andiko la pili Yakobo anawaalika Wakristo kushinda tabia ya ubaguzi katika jumuiya kwa kuthamini uwepo wa kila mtu bila kufikiria msimamo wake katika jamii. Kipaumbele ya jumuiya inapaswa kuwa maskini kwa sababu ndio wenye heri wa Mungu nao watapokea ufalme. Jumuiya za Kikristo haziko ili kufuata mawazo wa jamii bali kutenda kwa njia ya kinabii kulingana na injili. Utabiri wao utaonyeshwa wakati zinapopata kuwakaribisha na kuwanganisha katika uzoefu wake wote hasa wale ambao wanakataliwa.

        Katika injili, matendo ya Yesu yanatambuliwa na watu ambao walitangaza, “amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema”. Uwepo wa Yesu umeleta wakati mpya ulimwenguni. Katika Yeye ufalme wa Mungu umekuwa hali halisi, ilipatikana kwa wote. Wakati Yesu aliutangaza ujumbe wake katika sinagogi ya Nazareti, mahali alipolelewa, alikataliwa. Lakini alikaribishwa sana katika upande wa ziwa Galilaya, mahali panapoitwa Dekapoli - yaani miji kumi. Kulingana na toleo la Mathayo, Galilaya lilifikiriwa “nchi ya watu wa mataifa”. Uwepo wa Yesu uliwafanya watu waliokaa “gizani” waone mwanga mkubwa.

        Basi, ingawa watu hawa walikuwa na lugha na desturi tofauti na Wayahudi wa Yudea, walimtarajia na kumkaribisha Masiya kwa hamu sana. Injili ya Marko inasisitiza kipengele hiki kwa sababu iliandikwa kwa Wakristu wa huko Roma na lengo la injili hii ni kujibu kwa swali “Yesu ni nani?”. Jibu kwa swali hili tunakuta katika wakati wa mwisho wa maisha ya Yesu msalabani kutoka midomo ya jemadari mmoja wa Roma: “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

        Kama Mwana wa Mungu, lengo la Yesu ni kutangaza wokovu wa Mungu si kwa watu fulani tu, bali kwa wote. Yesu alikuwa Myahudi, bali hakuwa mali ya Wayahudi. Ishara zilizotumiwa na Yesu zilidhihirisha kwamba wokovu wa Mungu si mpango kwa wakati ujao tu, bali umekwisha anza katika historia kwa wote. Wakati tunaongea kuhusu “watu waliochaguliwa” tunamaanisha mpango wa hekima ya Mungu ambaye anatumia baadhi ya watu ili kufikia wengine kwa urahisi.

     Hivyo, kutoka Waisraeli Yesu na washirika wake walifikia wasio na Wayahudi pia wakitangaza habari njema ya injili. Mtu yule aliletwa kwa Yesu alikuwa na matatizo mawili, yaani, alikuwa bubu na kiziwi. Aliteseka sana na mara nyingi alikuwa mpweke kwa sababu hakuweza kuwasiliana na wenzake kila alichofikiri au kutamani, na wengine pia hawakuweza kuzungumza naye. Alitamani kukutana na Yesu na kupata maisha mapya ili kuishi uhusiano mwema na wengine. Kabla ya kufanya mwujiza Yesu alimwalika kuenda mahali pa faragha kwa sababu hakutafuta kuwa maarufu wala watafsiri muujiza wake kwa njia siyo kweli. Muujiza wa kwanza Yesu anaotaka kutenda katika maisha ya yeyote ndio kuwa na uhusiano wa ndani nawe. Yesu anatazama juu mbinguni kwa maana ya ushirika wake na Baba aliye wa pekee aliyemwezesha kumponya Bubu kiziwi. Hivyo, mkutano na Yesu kwa uhusiano wa ndani unaleta maisha mapya.

        Kazi ya Yesu ilikuwa kumwalika binadamu kutoka upweke na kutengwa kwa ushirika, yaani ushirika na Mungu na wenzake. Kama wafuasi wa Yesu tunaimarishwa na mfano wake na ishara zake. Ujumbe wetu unapaswa kuwa ni mwendelezo wa ujumbe wake na kama vile yeye tunaalikwa kufanya mambo yote vyema, yaani matendo yetu na mahusiano yetu yapaswa kufanya watu waishi maisha mapya. Yesu anatualika kwa uhusiano naye kwa faragha ili kutuponya kwa maana sisi tu kama mtu bubu na kiziwi, yaani tuna ugumu wa kusikiliza Neno la Mungu vizuri na kulitangaza kwa uaminifu. Matokeo wa uhusiano wetu na Bwana yatakuwa ni matunda mazuri kwa ajili ya utukufu wa Mungu na manufaa ya ndugu zetu. Ndiyo neema ya Mungu inayotenda ndani yetu ili tuweze kutenda kwa jina lake. Kama injili haina mpaka, tunaalikwa kushinda vikwazo ambavyo vinatuzuia kuwakaribisha wengine na kuwa na hisia mbele ya mahitaji yao. Ikiwa ni kweli uhusiano wetu na Bwana, tulime hisia na tabia kama yeye ili wengine wapate maisha mapya na sisi tuwe na furaha kamili.

Fr Ndega


Nenhum comentário: