domingo, 4 de junho de 2017

WATU WENGI KWA LUGHA MOJA PEKE YAKE


Kutafakari kuhusu Mdo. 2,1-11; 1Kor. 12,3b-7.12-13; Yoh 20,19-23


          Siku ya leo tunasherehekea ujio wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wa kwanza na mwanzo wa utume wa Kanisa, lililo Jumuiya ya Agano Jipya. Sherehe hii inatuhakikishia kwamba Roho Mtakatifu ndiye kuwepo kanisani na ndani ya kila mmoja wetu. Huyo ndiye Roho wa Yesu na Baba aliye Roho wa faraja kwa wale wanaohisi kutokuwepo kwa Yesu kwa kimwili. Huyo ndiye Roho wa nguvu kwa wale wanaohitaji ujasiri ili wawe mashahidi wa makuu ya Mungu kwa wote. Huyo ndiye Roho wa umoja ili ushahidi wetu kwa Yesu uwe wa kuaminika.

      Kulingana na somo la kwanza, wafuasi walikusanyika kusali wakishiriki pamoja matarajio yao kuhusu ahadi ya Yesu pamoja na mama yake na wanawake wengine, lakini walikuwa wamejawa na hofu kwa sababu ya upinzani wa jamii ya Wayahudi dhidi ya mafundisho ya Yesu na wafuasi wake. Yesu aliahidi kuandamana nao siku zote, lakini walikuwa hawajafahamu bado maana ya uwepo huu. Walihitaji nguvu kutoka juu kwa uelewa kabisa kuhusu maneno ya Yesu. Hao walisubiri wakimwomba Mungu kwa uvumilivu na imani ili wapate nguvu hii. Ghafla, Roho aliwashukia wote kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Ndimi hizi za moto zilizo mfano wa zawadi za Roho Mtakatifu, zilichoma hofu ambayo iliwazuia kuongea na kuwafanya kuwa mashahidi jasiri.

        Mwinjilisti Luka anasema kwamba Roho Mtakatifu alikuja katika Sikukuu ya Pentekoste ambayo Wayahudi walisherehekea Sikukuu ya Majuma ama ya mavuno. Tena walikumbuka utoaji wa Amri kumi Mlimani Sinai. Kwa wanafunzi wa Yesu hii imekuwa Sikukuu ya uumbaji mpya kwa tendo la Roho wa Yesu. Mungu alifanya Agano jipya na watu wapya. Kwa hivyo ishara nyingi za ajabu zilionyeshwa kama zilitokea katika Agano la kwanza, yaani moto, tetemeko la ardhi, upepo wa nguvu na kadhalika. Hivyo, Kanisa lililo jumuiya ya Agano Jipya, lilianza safari yake kwa nguvu ambayo ikalifungua kwa dunia nzima. Zawadi ya lugha mbalimbali inaonyesha kwamba Kanisa linatumwa kwa wote na kuongea nao kwa lugha rahisi ili iwafanye watu wote wawe familia moja.

            Kwa upande wa injili ya Yohane, Roho Mtakatifu ndiye zawadi iliyotolewa katika siku ile ya Ufufuko kama alama ya maisha mapya ya Yesu Mfufuka kwa wote. Yeye aliingia katika mahali ambapo wanafunzi walikusanyika ili kuwasaidia kushinda hofu na kugundua tena msukumo katika safari yao. Yesu aliwavuvia akiwapa Roho Mtakatifu. Lakini kabla ya kuwapa zawadi hii kubwa Yesu alisimama katikati yao na kuwahakikishia hali nzuri kama maandalizi ya kupokea Roho yake Mtakatifu. 

           Kwanza kabisa, aliwapa zawadi ya amani nao walifurahia uwepo wa Bwana Mfufuka. Yesu aliwashirikisha katika kazi yake akiwatuma kama mashahidi wa furaha ili watangaze mambo makuu ya Mungu. Watapaswa kutangaza huruma ya Mungu na upatanisho kati ya watu. Kazi hii muhimu haiwezekani kufanya bila msaada wa Roho Mtakatifu. Kwa hivyo, Yesu aliwapa Roho yake kwa hiari.  ‘Roho waliyempokea kutoka kwa Yesu anawafanya wapya na kuwapa nguvu ya kufanya maajabu kwa jina la Yesu.’


          Hili ndilo tendo la Roho Mtakatifu maishani mwetu tulio wanafunzi wapya wa Yesu. Ikiwa katika tukio la pentekoste Roho Mtakatifu aliwakalia kila mmoja wa wanafunzi wa kwanza, yeye anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya wanaomfuata Yesu kwa vizazi vyote. Sisi tumepokea Roho Mtakatifu huyo tangu ubatizo wetu. Makaribisho ni ya kibinafsi lakini uzoefu huu tunaishi katika jumuiya na kwa ajili ya jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Kwa kifupi, “kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho Mtakatifu kwa kufaidiana.” 

          Ingawa hatutambui, sisi tumeongozwa na Roho Mtakatifu kila wakati. Hivyo, hatuwezi kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Tena hatuwezi kutenda mema ama kumwomba Mungu kama ipasavyo isipokuwa katika Roho huyo. Ingawa sisi ni wa tamaduni mbalimbali na kuongea lugha nyingi, tunaweza kupanga pamoja kwa ajili ya wote kwa sababu ya Roho huyo ambaye anaongea lugha moja peke yake, yaani lugha ya upendo iliyo lugha ya msamaha na ya amani. Roho Mtakatifu atupatie lugha hii.

Fr Ndega
Kiswahili review: Christine Githui

Nenhum comentário: