domingo, 25 de junho de 2017

MAANA YA KUISHI KWA TUMAINI


Kutafakari kutoka Yer 20,10-13; War 5, 12-15; Mt 10: 24-33


       Mazingira magumu ni sehemu ya maisha yetu ya binadamu. Katika safari tunakabiliana na changamoto nyingi. Mara nyingi tunaogopa kwa sababu tunafikiri kwamba tunaweza kushinda magumu kwa nguvu zetu peke yake nasi tunashindwa. Hapa ni muhimu kugundua tena kiini cha ujumbe wa Kikristo, yaani ubaba na utunzaji wa Mungu kwa watoto wake. Ujumbe huu ni habari njema inayotupa maana ya kuishi kwa tumaini na kusadiki kwamba mambo yote ulimwenguni ni sehemu ya mpango wa hekima ya wema wa Mungu ambaye anatenda makuu hata mbele ya udhaifu na maovu ya kibinadamu. Mazingira ni magumu lakini tuko na Mungu aliye Baba.

       Nabii Yeremia ni mfano wa hali hii. Yeye alikabiliana na mazingira magumu na kuteseka kwa sababu ya uaminifu wake kwa Mungu aliyemwita kuwa nabii tangu tumbo la mama yake. Uhakika kuhusu ulinzi na utunzaji wa Mungu ulimwimarisha wakati wote wa safari yake. Katika maneno ya Yeremia tunaweza kutambua kwamba alikuwa na uhusiano wa ndani na Mungu. Uhusiano huu ndio maana ya uvumilivu wake na kuwaaibisha maadui yake. Yule anayemtumainia Mungu hakati tamaa kwa sababu Mungu hawaachi waliomtumainia yeye. Kulingana na somo la pili, tuko na maana za kuamini kuliko kukata tamaa kwa sababu, ingawa wanadamu wote waliguswa na dhambi ya Adamu nao walitenda dhambi, neema ya msamaha ambayo ilikuja kwetu kwa Yesu ilishinda mno hali ya dhambi. “Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima” (Papa Francisco).

      Katika injili, Yesu aliwaambia wanafunzi wake “Msiogope." Je, kwa nini alisema hivyo kwa mara tatu? Alisisitiza kwa neno “Msiogope" kwa sababu alitaka wawe mashahidi jasiri wa uzoefu ambao ulibadilisha ulimwengu ukishinda giza na kuzifukuza hofu zote. Yesu alijua kwamba wataonja mateso kama yeye na kwamba imani yao ni haba kwa kubaki imara. Kwa hivyo, aliwahakikishia uwepo wake maishani mwao na kuongea kuhusu utunzaji wa Mungu kwao. Kwa Mungu maisha yao yanathamani sana. Mungu anaweza kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri. Anafanya hivyo kwa sababu anawapenda na kuwatunza wale ambao aliwachagua. Maneno haya ya Yesu yaliwaimarisha ili waiendeleze kazi ambayo yeye aliwakabidhi.

      Wakati Yesu alishiriki mamlaka yake na wanafunzi wake alilenga waweze kutangaza kwa wote. Hii ni maana ya habari inayopaswa kutangazika hadharani. Kiini cha ujumbe wao ni utunzaji wa Mungu anayeshughulika hata kwa mambo madogo ya maisha. Kwa kutangaza ujumbe huu wanafunzi wanapaswa kushinda hofu kwa sababu hali ya hofu inaonekana kukana ukweli wa ujumbe huu. Tunajua kwamba ukatili dhidi ya wajumbe wa Mungu ulikuwepo zamani na unaendelea siku hizi. Lakini wameutendea mbaya mwili tu. Shida inaanza wakati wanaochaguliwa sio waaminifu na kusababisha kashfa, wakivuruga wale wanaotaka kusadiki. Hali  hii ni kifo cha mwili na roho pamoja.

      Tunataka kukumbuka Waathirika wa ukatili kwa sababu ya Imani katika nyakati zote. Kama mwalimu wao, walibaki imara katika ahadi yake. Njia yao ya kuishi mbele ya ukatili imewaaibisha maadui zao na kuwasaidia kutafakari. Siku moja Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Mtu akikupigia kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili”, yaani njia tofauti iliyo njia kamili ya kutenda. Ukatili hauwezi kushinda ukatili bali ndio wema wa moyo unaoweza kufanya hivyo.


       Hata sisi tunapoona hali mbaya tunajaribiwa kuwa na hofu, kukata tamaa, kufa moyo na kuacha ahadi yetu. Lakini uhakika wa uwepo wa Yesu na utunzaji wa Mungu unatuimarisha kuendelea na safari. Kwa hivyo maneno haya ya Yesu ni faraja pia kwetu: “Msiogope”! Mwe na imani tu! Mungu anajua jinsi ya kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri. Yeye anajua analofanya. Matarajio yake, kulingana na mafundisho ya Yesu, ni kwamba tujione watoto wake na kwa hivyo, tumruhusu kutenda maishani mwetu kulingana na mapenzi yake. Tusiogope kwa maana tuna thamani kuliko shomoro wengi na Mungu hawaachi wanaomwamini na kumtumainia yeye.

Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Ghitui

Nenhum comentário: