quarta-feira, 18 de novembro de 2015

WAKATI WA MAZINGIRA MAGUMU

Kutafakari kuhusu Dan 12: 1-3; Heb 10: 11-14; Mk 13: 24-32

Tunaweza kuanza kutafakari huku kujiuliza maswali sisi wenyewe: “Je, wakristo wanapaswa kuwa na tabia gani wakati wa mazingira magumu? Liturgia hii ni hamasa Kwetu ambao tunaalikwa kuishi imani yetu katika Kristo kama maana ya utambulisho. Kwa sisi ujumbe kuhusu miisho ya nyakati si ishara kwa kukata tamaa, bali mwaliko kwa tumaini. 

Somo la kwanza kutokana na kitabu cha nabii Danieli ni ufunuo kuhusu hukumu na ufufuko. Ni mara ya kwanza ambayo tangazo la ufufuko linaonekana katika biblia kabla ya Kristo. Watu wa Israeli walitumwa na wagiriki na kuteseka sana. Wengi miongoni mwao waliacha kumwamini Mungu, lakini wengine waliendelea katika imani yao kwa uvumilivu. Kwao Mungu alituma malaika Mikaeli awalinde na kuwahamasisha wakabili wakati wa taabu bila kukata tamaa. Uwepo wa malaika Mikaeli ni dhamana ya ukombozi na ufufuko kwa wale ambao walikuwa waaminifu kutenda mema hadi upeo. Kulingana na somo la pili sadaka ya Kristo ilishinda sadaka za makuhani wa Agano la Kale kwa sababu sadaka zao zilikuwa hafifu, haba na hazikuweza kuondolea dhambi za watu wote. Lakini sadaka ya Kristo iliyotolewa mara moja tu iliweza kuwatakasa watu wote kwa nyakati zote. Katika kila misa takatifu tunasherehekea fumbo la sadaka hii, kuuhisi na kuusaidia wokovu wa Kristo kwa wote. Ni Kristo mwenyewe ambaye anatuhusisha katika mwendo huu.

         Mwanzoni mwa sura ya kumi na tatu ya injili hii ya leo Yesu anasema kuhusu uharibifu wa Yerusalemu. Ufunuo huu uliwahamasisha baadhi ya wanafunzi wake wamwulize swali kuhusu ishara gani, siku na saa gani ya uharibifu huu. Yesu anatumia nafasi hii kuongelea mambo mengi ambayo yatatokea baadaye ili kuiandaa mioyo ya wafuasi wake, ni kwamba, ishara nyingi mbinguni, taabu, mateso, dhiki kuu na kuja kwake kulingana na unabii wa Danieli, yaani, juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. Kanisa katoliki hutafsiri tukio hili kama kuja kwake Yesu mara ya Pili ili kuwahukumia wazima na wafu. Hiyo ndiyo imani yetu ambayo sisi hutangaza kila jumapili. Kuhusu “Siku ya Bwana”, katika Agano la Kale manabii walikwisha wajulisha Waisraeli kuwa siku hii haingekuwa ya adhabu kwa mataifa mengine tu, bali pia kwa Waisraeli kwa kutokuwa waaminifu katika agano walilolifanya na Mungu. Kuhusu siku na saa hii hakuna mtu ajuaye. Hii ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Kwa hivyo huu ni pia mwaliko kwa kukesha. Kwa wale ambao wanamfuata Yesu, kukesha lazima kuwa tabia daima kwa sababu ikiwa tunamjua mwalimu wetu, tutakuwa tayari daima ili kumkaribisha.


    Katika utume wake, Yesu aliwaonya wafuasi wake kuwa, mwisho wa nyakati utatanguliwa na matukio mengi magumu, lakini Yesu hataki kutuogopesha. Anatuambia tutarajie kuja kwa pili kwa mwana wa mtu atayekuja kuwachukua wana wa Mungu. Lengo ni kuimarisha imani yetu na kufufua tumaini letu kwa tendo la Mungu ndiye mkuu katika nyakati zote, zilizopita na zijazo. Anatufundisha kuishi wito wetu wa wafuasi kwa uaminifu katika wakati zote pia, hata wakati wa mateso makali. Ushuhuda wa Yesu ni kwamba Mungu huingia katika historia yetu kwa upendo na anajionyesha tofauti kabisa nasi na hata historia yake ni tofauti na yetu.  Baada ya majaribu yote Mungu atakuwa ndiye mshindi. Ni mwaliko tuwe na imani kwa Mungu na kuacha kutabiri mambo, kushinda hofu na mashaka yote. Kulingana na mithali fulani, “hakuna usiku hata wa muda mrefu pasipo mapambazuko”. Basi, kwa wale ambao wanamfuata Kristo, mazingira magumu si ishara za mwisho wa nyakati bali ni wakati mpya, wakati wa kuishi wito wetu kwa shauku zaidi, furaha na tumaini, kuushuhudia kwa uaminifu uwepo wa Bwana miongoni mwetu. Anakuja kwa upendo na kutuokoa. Tukaribishe ishara za nyakati kama msaada tutambue uwepo wa Bwana na kuishi mafundisho yake kwa njia mpya. 

Fr Ndega
Mapitio: Sara

Nenhum comentário: