quarta-feira, 25 de novembro de 2015

UFALME WA YESU NI TOFAUTI KABISA


Kutafakari kuhusu Yoh 18, 33-37

            Tunasherehekea sikuku ya Bwana Wetu Yesu Kristu Mfalme. Yeye ni Mfalme wa mbingu na dunia; enzi na utawala wote ni wake. Liturjia hii inatualika kumfuata Mfalme huyo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Kuutafuta kwanza ufalme wake ni maana ya kweli ya maisha yetu.

Mbele ya Pilato, Yesu hakukanusha juu ya ufalme wake,  bali anafafanua zaidi maana ya ufalme huo. Swali la Pilato kwa Yesu ya kwamba: “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”, lilikuwa limewaza kuwa Yesu alikuwa mmoja wa wazalendo ambaye alitaka kuupindua utawala wa Roma na kuanzisha utawala mpya wa kisiasa kwa wayahudi. Wayahudi wengine walitumaini kuwa Masiha angewarudishia tena utawala wa Daudi. Wote, Pilato na Wayahudi, wana wazo ambalo sio kamili kuhusu ufalme wa mbinguni na kuhusu pia Yule aliyechaguliwa na Mungu adhihirishe ufalme huu. Yesu anakubali kuwa yeye ni mfalme, lakini siyo mfalme wa wayahudi tu. Yeye ni Mfalme wa wote na Ufalme wake ni tofauti. Kumbe ufalme wa Yesu si wa dunia hii lakini unawahusu wote waishio hapa duniani.

      Ufalme ni mapenzi ya Mungu ambayo Yesu aliishi na ufalme huu ni pia hali mpya aliyoanzisha ulimwenguni. Uwepo wake unaanzisha wakati mpya, yaani, wakati wa wokovu wa Mungu. Msingi wa ujumbe wa Yesu ni tangazo la wokovu wa Mungu ambalo ni sawa na tangazo la ufalme pia. Kwa kweli Yesu hajitangazi mwenyewe, bali anautangaza Ufalme. Katika Yesu mwenywe ufalme ulikuwa hali halisi ukisababisha mabadiliko ulimwenguni kwa wema wa wote hasa kwa walio na mahitaji mengi, yaani, wagonjwa wanapona, bubu wanaongea tena, vipofu wanapata kuona tena, maskini wanaipokea habari njema na wenye dhambi wanaondolewa dhambi zao. Kuna wengi ambao wanalitambua tendo la wokovu wa Mungu katika ishara za ukombozi za Yesu na wanajiruhusu kubadilishwa, lakini kuna wengine pia ambao wanajifunga wenyewe na hawawezi kutambua kile ambacho kinatokea kandokando yao. Upinzani dhidi ya Yesu ni upinzani dhidi ya mafanikio ya Ufalme wa Mungu. Katika maana hii ni ngumu sana kumfuata nyayo zake na kutangaza ufalme wake.

        Sio kwa Pilato tu, bali kwa wengine pia ilikuwa ngumu kufahamu kwamba Ufalme wa Yesu ni tofauti na wa dunia hii. Ufalme wake ni wa kuushuhudia ukweli na kuwaongoza watu katika njia ya kweli. Ufalme ambao Yesu anatangaza upo ndani yake na unaonyeshwa kupitia matendo yake miongoni mwa watu. Yesu hakufasili Ufalme lakini aliuonyesha upo ulimwenguni kupitia ishara nyingi. Hii si hali kwa kutazama bali kwa kuhisi na kutangaza. Hili ni fumbo la imani. Ingawa hatuna ufafanuzi kuhusu ufalme kutokana na injili, ibada ya Ekaristi ya siku hii inatujulisha baadhi ya thamani ambazo zina uhusiano wa ndani na ufalme ambao Yesu alikuja kutangaza, yaani, “Huu ni ufalme wa milele na ulimwengu wote, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani.”


        Ni lazima kuwa makini sana kwa ishara za ufalme huu, kwa sababu, ingawa ufalme huu ni hali inayochanganyika na hali za binadamu, zipo ishara nyingi zinazoonekana kuwa wa Ufalme wa Mungu, lakini zinaweza kutudanganya. Yesu ni ishara ya ufalme kwa namna ya ajabu. Hatuhitaji nyingine. Msingi wa ufalme wa Yesu ni ushuhuda katika kweli unaoweza kubadili maisha ya watu, ikiwa tumkubali. Tunapomkubali Yesu na kumsikiliza na kisha kumruhusu awe kiongozi wa maisha yetu, tutakuwa tukiishi katika kweli. Kila aliye wa hiyo kweli humsikia sauti ya Yesu anayesema kuamba ndiye njia, ukweli na uzima. Ukweli huu utawapeni uhuru. Ufalme wa Yesu hupingana na uongo, uonevu na ukandamizaji na kila namna. Ufalme wa Yesu hautokani na nguvu au vita. Hivyo kila mmoja wetu ni budi aisikie sauti ya ukweli na kuamua kwa hiari yake kuifuata. Tuchukue pamoja na Mtakatifu Yohana Calabria ahadi ya kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu kuiimarisha imani duniani katika Mungu Baba Mtoaji.

Fr Ndega
Mapitio: Sara

Nenhum comentário: