domingo, 4 de outubro de 2015

MWANZO MUNGU ALIWAUMBA MWANAMKE NA MWANAMUME


Kutafakari kutoka Marko 10:2-16

     Mwanzoni mwa injili ya leo Yesu alikuwa akiwafundisha watu kama ilivyokuwa desturi yake. Ghafla baadhi ya Mafarisayo walimwendea wakimjaribu. Jambo lilikuwa kuhusu talaka. Yesu aliitambua nia yao mbaya, lakini aliwatendea mema, akiwasikiliza kwa utulivu na kuthamini juhudi zao za kumwuliza maswali. Katika mazungumzo na Yesu shida yao ya pekee ilikuwa mtazamo pungufu kuhusu ndoa na familia. Yesu alisahihisha mtazamo huo, akiwakumbusha mpango asili wa Mungu kwa mwanamume na mwanamke. Aliongea pia kuhusu uzinzi kama matokeo ya talaka na kuonyesha uhusiano maalum na watoto wadogo ambao wanastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa ili wakue kwa usalama na furaha.

      Baadhi ya Mafarisayo wanatumia sheria ya Musa kumjaribu Yesu. Kulingana na mawazo yao, Sheria hiyo inaruhusu talaka, lakini Yesu anayakataa hayo. Kwa nini Yesu ana msimamo tofauti kwa uhusiano na jambo hili la Sheria? Kulingana na Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria, sura 24, mwanamume aliweza kumpatia mkewe talaka ikiwa hakupendezwa naye kwa sababu ameona kwake kitu kisichofaa. Mwanamke alikuwa na nafasi chache za kutoa talaka kwa mmewe, mfano mwanaume akiugua ukoma. Katika mazingira haya hali ya mwanamke ilikuwa ngumu sana kwa sababu daima alionewa na daima alitegemea huruma tu ya mwanamume. Lakini Yesu aliwasaidia kufikiri vizuri kwa sababu Sheria zimewekwa kwa manufaa ya watu na si watu kwa ajili ya sheria.

      Msimamo wa Yesu ni wazi sana. Yeye alikuja kudhihirisha mpango asili wa Mungu na kulingana na mpango huu, wote mme na mke wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu ameweka upendo asili unaowafanya watamaniane na hatimaye kuwaacha wazazi wao, kuungana na kuwa mwili mmoja. Jambo hili linaonyesha kuwa mwanaume hana haki ya kuamua atakavyo kwa mkewe, mfano kumwacha mke wake kwa muda wowote anaotaka. Hivyo kuungana kwao kunamaanisha kuwa hawawezi kuachana au kutenganishwa. Lengo kuu la Yesu, ni kukarabati nafasi na utu wa mwanamke ulioharibiwa na sheria. Kulingana na Yesu Mwanamke ana haki ya kuheshimiwa katika maisha ya ndoa na si kutendewa na kumilikiwa kama chombo tu. Nia ya Mungu ni kuwa mume na mke waendelee kukua katika pendo na kupata uzima wa milele. Nasi tunaweza kuushiriki mpango huu wa kuishi maisha ya umoja katika familia na jumuiya zetu.

     Thamani ya kibinadamu ya kupenda na kupendwa ni maana ya uzoefu wa ndoa na familia. Familia ni msingi wa uzoefu wa kibinadamu na yoyote ambayo ni dhidi ya kanuni hii ni marufuku katika biblia. Kwa hiyo “Usizini” ni moja miongoni mwa Amri Kumi. Kwa nini uzinzi hutishia familia? Uzinzi unaweza kuharibu familia kwa sababu unaweza kusababisha ujauzito na kuzaliwa kwa mtoto. Mtoto huyo ataanza safari ya maisha pasipo familia. Ikiwa uzinzi hauharibu familia, mara nyingi unasababisha madhara ya kutisha ndoa, kama hisia ya usaliti na upotevu wa itibari ambayo inamaanisha kwamba uzinzi unasababisha maisha ya ulaghai. Ni lazima kuwa macho kwa baadhi ya aina za urafiki. Wakati mume au mke ana urafiki fulani ambao anaanzisha uhusiano wa nguvu zaidi kuliko ule anaoishi na mke au mume, ni ngumu sana kuuepuka uzinzi. Wakati mume au mke ana ngono na mwingine kuliko mkewe/mumewe, mawazo kuhusu yule mtu ni daima na mawazo kuhusu jinsi ya kumdanganya mume au mke ni daima pia. Uzinzi haulindi familia na tena hauwalindi wanandoa dhidi ya maumivu ya hisia. 

        Maana ya Amri “Usizini” ni ulinzi kwa familia. Kwa nini familia ni muhimu sana? Kwa sababu pasipo familia uimara wa jamii hauwezekani. Kwa sababu bila familia mawasiliano ya thamani ya jamii kizazi kwa kizazi hayawezekani. Kwa maana uhusiano kati ya wazazi na watoto unawafanya kuwajibika na kukomaa zaidi. Kwa sababu bora kuliko chochote, familia inayaridhisha mahitaji ya hisia na fizikia/mwili, kuwapa watoto utoto salama na imara.

Fr Ndega

Mapitio: Sara 

Nenhum comentário: