sexta-feira, 2 de dezembro de 2022

TUTENGENEZENI NJIA YA BWANA

 

Kutafakari kuhusu Is 11: 1-10; Rm 15: 4-9; Mt 3: 1-12




     Liturgia hii inaendelea kutumwalika kumkaribisha Bwana anayekuja kutuletea wokovu. Tunaalikwa kujiandaa vizuri ili tuweze kumpokea Masiya wakati wowote. Wakati wa Majilio unatusaidia kutambua kwamba kwa matayarisho kamili ni lazima mabadiliko ya moyo, kwa njia mpya kabisa. Maneno ya nabii Isaya yanaijaza mioyo ya watu kwa matumaini makubwa kwa sababu yanatangaza hali ya ajabu ambayo Bwana wao anaandaa kwa maisha yao. Mungu anawaongoza watu wake katika mwangaza na utukufu wake. Anawaahidi mkombozi ambaye atawaletea amani na kutenda kwa haki na upendo hasa kuwahusu maskini na wanaoteseka. Mkombozi huyo ndiye Kristo, aliye Mungu pamoja nasi.

    Paulo akiwaandikia Waroma anathibitisha kwamba Kristo alitimia ahadi zilizowafanyiwa mababu kama mtumishi mwaminifu wa Mungu. Uwepo wake duniani umekuwa maonyesho ya huruma ya Mungu kwa wote hata kwa Wapagani ambao walichukuliwa kama wasio na nafasi ya wokovu. Yeyote anayejitambulisha na Kristo kama mfuasi wake anapaswa kuwa na hisia sawasawa na yeye. Hivyo imani na ushirika wa Waroma na Wakristo wote wakuwa uenezi wa habari njema kwa kuzaa mazao mazuri kwa utukufu wa Mungu. Huu ndio ukweli wa utambulisho wetu.  

    Injili inaongelea Yohane Mbatizaji anayeonekana jangwani kwa kutangaza Neno la Mungu. Uwezo wa Yohane unatokana na uzoefu wa Neno hili kwa maana hakuna mtu hata mmoja aweze kutoa ushahidi wa jambo fulani bila kupata nafasi ya kufanya uzoefu wa jambo hili. Yohane anaanza kazi yake jangwani. Katika biblia jangwa ni mahali maalum pa uzoefu wa Neno la Mungu. Katika mahali huko viongozi wengi waliishi uzoefu wa ndani wa Mungu ili kujiandaa kwa kazi ya kuwaongoza Watu wa Mungu kulingana na mwongozo wake na tena kwa matakwa wake. Yohane Mbatizaji ndiye nabii wa mwisho na kufikiriwa kama mkuu wa manabii wote.

Kuja kwake Yohane Mbatizaji kunaufuata mpango wa Mungu ambaye ana wakati kamili kwa kila kitu. Kama Yohane ni kiungo kati ya Agano la kale na la Jipya, kazi yake inatangaza kwamba nyakati za Masiya zimeanza. Yeye ni sauti tu ambayo inatayarisha njia za Bwana. Kwanza kabisa aliwatangazia watu watubu ili kuukaribisha ufalme wa Mungu ulio karibu nasi. Ufalme huu unamaanisha uwepo wa Mungu miongoni mwa watu wake kupitia nafsi ya Yesu na makaribisho kwa ufalme huu yatokea tunapotoa ruhusa kwa tendo la Mungu maishani mwetu.

Zaidi ya maneno, tena Yohane aliwatayarisha watu kumpokea Masiya kwa ubatizo. Kupitia ishara hii alitangaza huruma ya Mungu iliyopatikana kwa kila mtu kwa sababu ni mpango wa Mungu kwamba wokovu wake ufikie wote. Ubatizo wa Yohane haukuweza kuziondoa dhambi za watu naye Yohane alitambua hilo vizuri. Basi, je ikiwa ubatizo huu haukuwa na uwezo wa kuziondoa dhambi, kwa nini Yohane aliitumia ishara hii? Ni kwa sababu alitaka kuwasaidia watu kukiri dhambi zao na kufungua moyo kwa huruma ya Mungu. Ubatizo huu ulikuwa maandalizi kwa ubatizo mpya na kamili atakaotumia Masiya kama ishara inayoonekana mapito kutoka dhambi kwenye neema na kutoka mauti kwenye maisha mapya.

Ubatizo wa Yohane ni tofauti na ubatizo wa Yesu, lakini yote mbili ni nafasi ya kuishi maisha mapya. Kwa upande wetu maisha mapya ni zawadi ya Kristo na matokeo ya utume wake. Ubatizo wa Kikristo, pamoja na maondoleo ya dhambi, unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe. Ubatizo ni wa kwanza kati ya sakramenti tatu za mwanzo ukifuatiwa na Kipaimara na Ekaristi kwa uzoefu wa mwanzo katika safari ya kikristo. Ubatizo wetu ni ishara ya nje ya kufa kwa maisha ya dhambi, na ya kufufuka kwa maisha mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga wa kweli unaomfafanua kila mtu. Kupitia mwendo huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika nuru ya Mungu kila siku ya maisha yetu.

Kipindi cha Majilio kinatusaidia kujiandaa kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu. Maisha ya unyenyekevu ya Yohane ni mwaliko tutende kama yeye alivyo ili maisha yetu yaweze kumpendeza Mungu. Mambo Yohana aliyowaambia mafarisayo na masadukayo ni muhimu pia kwetu: kuhusu kutubu hayatoshi maneno; tunapaswa kuzionyesha ishara halisi za mabadiliko yetu, vinginevyo hatutapata kujitayarisha ipasavyo kwa kumkaribisha yesu. Kuna vikwazo vingi vya kuondoa katika maisha yetu kwa msaada wa huruma ya Mungu. Basi, tuchukue nafasi hii nzuri kuadhimisha sacramenti ya Upatanisho (na kitubio) na kuishi kwa njia mpya uhusiano wetu na Mungu na wengine.


Fr Ndega

Nenhum comentário: