sexta-feira, 16 de dezembro de 2022

KUWA WASHIRIKA WA MUNGU

 

Tafakari kutoka Is 7: 10-14; Rm 1: 1-7; Mt 1: 18-24




 

    Katika safari yetu kuelekea Krismasi, ni muhimu sana kutafakari kuhusu Mtakatifu Yosefu aliyekuwa mtu mkimya bali alikuwa na ushiriki mkubwa katika kuhakikisha usalama na ulinzi kwa Mwana wa Mungu aliyekuja ulimwenguni, dhaifu na mhitaji. Ingawa Mungu angeweza kuwaokoa wanadamu peke yake, alitaka kuchagua washirika kwa kutekeleza mpango wake kama alivyosema Mtakatifu Augustino, “Mungu alituumba bila sisi lakini hakutaka kutuokoa bila sisi”.

    Katika somo la kwanza nabii Isaya halikukataa uamuzi wa mfalme wa Yuda, yaani Ahazi ambaye akihisi kutishwa na uvamizi unaowezekana na uliokuwa karibu, aliamua kufanya mapatano ya kisiasa na kijeshi pamoja na Ashuru badala ya kumwomba Bwana ishara kama maonyesho ya imani katika uwepo na ulinzi wake. Lakini Mungu, hata akikataliwa, hajiachi kuzuiwa kuhusu mpango wake wa kuwaokoa watu wake na kwa sababu hiyo anatoa kuzaliwa kwa mtoto ambaye ataufanya ufalme huu kuwa imara, na kutoa mustakabali wa tumaini kwa watu wote. Tunaona katika mtoto huyo sura ya Yesu, ambaye anatuletea wokovu, akihakikishia kwamba uthabiti wa kweli hautokani na ulinzi wa kibinadamu bali kwa kumtumaini Mungu.

    Katika somo la pili, Paulo anahutubia Wakristo wa Rumi kwa kujijulisha mwenywe si kwa kutumia data yake binafsi ya masjala bali kutokana na utambulisho wake mpya uliozaliwa kutokana na mkutano na Yesu Kristo aliyemfanya kuwa mtume wa Mataifa. Utambulisho wake huu hautokani na sifa zake bali ni uchaguzi unaofanywa kwa upendo, zawadi ya neema ya Mungu. Ufahamu huu wa Mtume Paolo unatuimarisha katika safari yetu na kutufanya tuelewe kwamba sisi pia tunapendwa na Mungu nasi tu watakatifu kwa wito kwa ajili ya kuwa washirika wake katika kazi ya wokovu kama mashahidi wa upendo wake na uhuru wake.

    Injili inatujulisha mfano wa Yusufu ambaye anaitwa mtu mwenye haki, yaani, “aliyekuwa na sheria yote ya Bwana moyoni mwake”. Kwa sababu ya pendekezo la Mungu lenye changamoto kwa Mariamu, anaongozwa kufanya uchaguzi wa ajabu. Maria anapomweleza kuhusu hali aliyokuwa akikabili, anamhakikishia kwamba ilikuwa ni uingiliaji wa kimungu. Kisha, Yosefu alikuwa mbele yake si tu sheria ya Mambo ya Walawi, ambayo iliamuru kushutumu wanawake kama kwahali hii ya Mariamu, bali pia upendo aliokuwa nao kwa msichana huyo na uaminifu wa maneno yake, akikubali kuweka maisha yake hatarini ili mpango wa Mungu ukatimize kwa ajili ya wokovu wa watu wake.

    ‘Ndiyo’ ya Maria aliye huru na mkarimu ilikuwa imesubiriwa na Mungu ambaye alimtaka awe mtumishi wake na alikuwa amemwandaa kwa hili, lakini tunapaswa kukubali kwamba ili aishi ndiyo hii yake, zaidi ya neema ya Mungu, Mariamu pia alisaidiwa na ndiyo ya Yusufu. Kwa busara na ukimya wake, anafanya ndoto ya wanandoa itimie kwa wakati zaidi na kumpa Mungu nafasi sahihi ya kutenda. Kwa hakika, pamoja na Yusufu Mungu hatoi Mariamu tu bali pia malaika wa kumsaidia “kuifuata njia ya upendo na kuiacha ile ya Sheria”. Hivyo toleo la Maria kuhusu ukweli wa lililotokea limethibitishwa. Wote wawili wameongozwa katika njia ifaayo ili kazi hii iliyozaliwa na mpango wa kimungu isishindwe kwa sababu ya magumu ya kibinadamu.

    Watu hawa wawili wanaotembelewa na Mungu, katika unyenyekevu na udogo wao hufanya maisha yao ya kila siku kuwa yenye kuzaa matunda, wanakuwa vyombo vya heshima vilivyotumiwa na Mungu kwa hiari katika kazi kuu ya wokovu. Ushuhuda wao unatusaidia kuelewa ni nini njia ya Mungu na ni nini hasa kinachompendeza. Hata kama hawakuelewa kazi yao ingekuwaje hapo mwanzo, hawakuweka vikwazo katika njia ya mipango ya Mungu.Vivyo hivyo lazima iwe mwitikio wetu wa kila siku kwa wito wa Mungu. Hatuhitaji kuelewa mara moja kazi yetu inapaswa kuwa nini. Tunahitaji kupatikana na kuwa tayari kwa kila kitu, tukimwaminia Mungu kama Mariamu, Yusufu na wengine wengi walivyofanya.


Fr Ndega

Nenhum comentário: