domingo, 2 de junho de 2019

YESU ANATENDA PAMOJA NA WANAFUNZI WAKE KUPITIA ROHO WAKE



Kutafakari kuhusu Mdo 1, 1-11; Waef 1, 17-23; Lk 24, 46-53



     Siku ya leo tunasherehekea kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alifanya kazi miongoni mwa wanadamu kwa miaka mitatu. Kupaa ni hitimisho ya kazi yake, lakini anaendelea kuwepo ulimwenguni kupitia Roho wake. Basi, sikukuu hii inatufafanulia fumbo la kuaga na uwepo wa Yesu kwa sababu yeye hakumwacha Baba alipokuja kwetu wala hakutuacha alipomrudia Baba. Kupaa kwake kunaongea kuhusu njia mpya ya uwepo wake miongoni mwetu kwa kutangaza hatua mpya ya kazi yake. Huu ni wakati wa Kanisa lililo jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Ujumbe muhimu kuhusu hali hii ni wazi sana hasa katika maandiko mawili ya Luka, yaani, Injili na kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika Injili yeye anajulisha vitendo vya Yesu, na katika Matendo ya Mitume anajulisha vitendo vya wanafunzi wake waliosaidiwa na Roho wake Mtakatifu.    

     Kuonekana kwa Yesu kwa muda fulani kuwaimarisha wanafunzi wake kugundua tena maana ya uanafunzi, wakishinda hofu na mashaka kuhusu hali ya ufufuko wake. Uzoefu huo ulikuwa mpya sana kwao naye Yesu alifahamu kwamba alipaswa kuwa na utulivu kwa sababu ya imani yao ndogo. Mwendo ulikuwa wa muda mrefu, lakini wenye ufanisi sana, ukisababisha mabadiliko makubwa maishani mwa wanafunzi, yaani, kutokana na uzoefu wa wanaume wenye hofu kuwa mashahidi wenye ujasiri.

    Katika maneno yake ya mwisho, Yesu aliwasaidia kufahamu uhusiano kati ya yale aliyoyatenda na kufundisha na yale yaliyoandikwa na manabii wa zamani. Habari ya toba na ondoleo la dhambi linapaswa kuwa umuhimu wa ujumbe wa waliotumwa kwa jina la Yesu aliye uso wa huruma ya Mungu Asiyeonekana. Uzoefu wao na Yesu uliwawezesha kuwa wanafunzi wa kweli, lakini walipaswa kuingoja nguvu kutoka juu ili waweze kuwa mashahidi wa Bwana Yesu tangu Yerusalemu mpaka mwisho wa nchi. Roho mmoja aliyekuwepo katika mwanzo wa uumbaji na wakati wa utume wa Yesu ataiongoza kazi ya wanafunzi wake.

       Yesu aliyashiriki mamlaka yake na wanafunzi wake ili wawatumikie watu, wakiwatendea mema. Kutokana na mfano wa kujisalimisha kwa Kristo ushuhuda wao wa kwanza ni kujitolea bila kipimo. Wanafunzi  walitumwa kama wajumbe wa habari njema kwa mataifa yote kwa sababu injili haina mpaka. Yesu alikuwa amewaahidia kuandamana nao mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa kimwili hauwezi kuonekana tena, Roho wake anawahakikishia kwamba hawatendi peke yao katika kazi. Uwepo wa Roho wa Yesu ulifanya maneno yao yawe ufanisi kupitia ishara nyingi na matendo mazuri.

      Kulingana na Mtakatifu Paulo, Roho ambaye aliwapewa kwa jumuiya ya kwanza ni Roho wa umoja. Kupitia Roho huyo tunaweza kumjua Mungu vizuri na kuishi katika umoja miongoni mwetu kama anavyotarajia Bwana wetu. Kila mtu anaitwa kuchukua ahadi hii ya umoja kama maana ya utambulisho. Katika jumuiya ya Kikristo tumezipokea zawadi nyingi kutoka kwa Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi, na kusaidia kujenga mwili mmoja, ambao ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake. Hili ni fumbo la uwepo wa Yesu katika kanisa lake ambalo ni mwili wake mwenyewe naye yu kichwa cha mwili huu.

    Malaika waliwaambia wanafunzi wa kwanza na kutuambia pia siku ya leo: “mbona mmesimama mkitazama mbinguni?” Hakika kama Wakristo tunahitaji kurudisha mtazamo wetu kwa Yesu aliye mfano wetu na kichwa chetu ili tuendelee kazi yake kwa uaminifu, lakini hatuwezi Kubaki wamesimama kutazama mbinguni kama ishara ya uvivu na utazamaji na kipooza. Bwana anatutaka tuwe waangalifu na wenye ufanisi kama ilivyoandikwa: “Wabarikiwa watumishi wale ambao watakuwa wakitumikia Bwana wao atakaporudi”. Maisha ya Kikristu ni kutafakari na kitendo, imani na matendo. Ishara za uwepo ufanisi wa Yesu zinaonyeshwa kupitia mapendo ya wale wanaomwamini na kuzifuata nyayo zake. Roho Mtakatifu afanye uwepo wa Yesu uwe ufanisi katika maisha yetu na kazi zetu ili tuendelee utume wake kwa uaminifu.  

Fr Ndega

Nenhum comentário: