sábado, 15 de junho de 2019

UMOJA WA UTATU MTAKATIFU NI CHEMCHEMI YA UMOJA WETU



Mit 8: 22-31; Rum 5: 1-5; Yoh 16,12-15



      Utatu Mtakatifu ni fumbo la Mungu aliye ushirika wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, yaani fumbo la upendo. Upendo ni utambulisho wa Mungu. Hivyo, “Mungu ni Utatu kwa sababu ndiye upendo”. Yeye ni Mungu wa kipekee lakini haishi peke yake kwa sababu alitaka kuwa ushirika wa upendo. Uumbaji wote ni uenezi wa nafsi yake na fumbo lake. Viumbe vyote vinaitwa kuingia katika ushirika huu wa upendo na kuwa maonyesho ya wema wake. Tunaposema ishara ya msalaba, yaani, “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu”, tunakiri kwamba nafsi yetu ndiyo makao ya uwepo maalum tangu ubatizo wetu. Ndio uwepo wa upendo na kutuomba uhusiano wa upendo nawe. Inawezekaje Mungu Mkubwa mno akae ndani yetu wadogo mno?

    Hilo ndilo fumbo kubwa kuliko yote ya imani yetu. Kutoka ufunuo wa Yesu tunapata kujifunza mengi na kuendelea kwa msaada wa Roho Mtakatifu ili tujihisi kuhusishwa katika fumbo hili hata bila kufahamu kamili. Kuna hadithi fulani inayoongea zaidi kuhusu hali hii: “Siku moja Mtakatifu Agostino alikuwa akitembea katika pwani ya bahari, akijiuliza swali kuhusu fumbo la Utatu Mtakatifu, akisema, “inawezekanaje Mungu kuwako kama Mmoja na Utatu wakati huo huo? Ghafla, alimwona mtoto mdogo aliyefanya shimo katika mchanga na kukimbia kwenye bahari, akichukua maji kidogo na kuyaweka shimoni. Baada ya kuangalia mchezo huu wa mtoto mdogo kwa mara nyingi, Agostino aliamua kumwuliza maana ya mchezo huo. Mtoto mdogo akamjibu akisema: “Najaribu kuweka maji yale yote ndani ya shimo hii”. Ameshangaa sana, Agostino akasema: “Hutapata kufanya hivyo kamwe!” Kisha, mtoto mdogo akamwambia akisema: “ni rahisi kwangu kuyaweka maji yale yote shimoni kuliko wewe ukapate kufahamu fumbo la Utatu Mtakatifu kwa akili yako. Mwishowe, mtoto mdogo alitoweka na Mtakatifu Agostino akajiambia mwenyewe: “Labda mtoto huyo alikuwa malaika fulani!”

      Hadithi hii inatufundisha hali muhimu sana, yaani, fumbo la Utatu Mtakatifu sio fumbo la kufahamika bali la kukaribishwa. Ikiwa tunajifungua zaidi kwa fumbo hili tunaweza kuhisi zaidi fumbo hili ndani yetu. Ujumbe wa masomo ya leo unatusaidia katika mwendo huu. Katika somo la kwanza hekima anajifunua kama nafsi ya Mungu. Hekima hii ni Mwana wa Mungu ambaye yuko pamoja na Mungu milele na kutenda naye kabla ya kuumbwa ulimwengu. Yeye ni Akili ya Mungu na viumbe vyote vilivyokuwako viliumbwa kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake. Yeye ni ukamilifu wa viumbe vyote. Somo la pili linatuambia kwamba Mwana alitushirikisha katika utukufu wake na Baba. Kupitia yeye tulipewa Roho Mtakatifu ili tuishi kama watoto. Tendo la Roho huyu limemimina mioyoni mwetu pendo la Mungu likithibitisha kwamba sisi ni watoto wake na hivyo tunaweza kumwita Baba yetu kwa uhuru kabisa. Ikiwa sisi ni watoto sisi pia ni warithi pamoja na Yesu kwa kupokea uhai wake wa kimungu. Ndiyo hali hii ambayo ubatizo wetu unatufanya kuishi.
    
      Umuhimu wa ujumbe ambao Yesu ametukabidhi ni kwamba yeye ndiye ukweli wa Baba na kutenda kwa Roho Mtakatifu. Mungu ndiye Utatu na hutenda pamoja kwa ushirikiano kamili. Yesu, aliyetumwa na Mungu Baba, alitangaza ukweli akiwahusisha watu katika ushirika sawasawa anaoishi Baba na Roho Mtakatifu. Utimizaji wa ahadi kuhusu ujio wa Roho huyo unatuhakikishia umoja wetu, kutuunganisha kama wana wa familia moja. Kupitia Roho huyo tunaangazika ili tuweze kukumbuka mafundisho ya Yesu na kuyatangaza kwa uaminifu. Wakati sisi hupendana tunaonyesha ukweli wa uhusiano wetu na Mungu na hali ya Mungu mwenyewe kama Utatu Mtakatifu. Tunapoishi uhusiano wa kweli na Yesu vivyo hivyo tunahisi ndani yetu tendo la Baba na Roho wake. Uzoefu wetu wa Yesu katika Ekaristi ni uzoefu wa Utatu Mtakatifu. Mungu anatumikia anakaa kati yetu na ndani yetu. Yeye anatuunganisha naye na miongoni mwetu. Hili ni fumbo la ushirika ambao Mungu ametuhusisha kwa maana anataka tuwe washiriki katika uhai wake mwenyewe. Kwa hivyo, tuombe atukuzwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu...

Fr Ndega

Nenhum comentário: