sábado, 18 de maio de 2019

MAMBO YOTE YAWEZEKANA KWA SABABU YA UPENDO



Kutafakari kuhusu Yoh 13, 31-35



      Umuhimu wa andiko hili ni amri ya upendo kama Yesu alivyofundisha. Kila kitu ambacho tunatenda kinapaswa kuwa alama ya upendo. Tendo bila upendo halina maana. Mtume Paulo aliliweka wazi jambo hilo: “Pia nikiwa na unabii, na kujua mafumbo yote na maarifa yote, na kuwa na imani yote hata kuhamisha milima, nikikosa upendo, sina maana” (1 Wakorintho 13:2).

       Mazingira ya andiko la siku ya leo ni ya karamu ya mwisho ambayo Yesu alianzisha Ekaristi iliyo sakramenti ya upendo na ya utumishi. Yesu alijua wazi kwamba Saa yake ilikuwa imefika. Katika injili ya Yohane, kila ishara ambayo Yesu anatenda ni tangazo la Saa hii ambayo inajumuisha mateso, kifo na kufufuka kwake. Kupitia Saa hii atamtukuza Baba na kutimiza utume wake. Kwa upande wa wanafunzi wa Yesu, Saa hii ni kipindi cha uamuzi, yaani, wanapaswa kuamua ikiwa wanataka kuendelea kazi ya mwalimu au la. Mwinjilisti Yohane alitaja wakati kamili ambao Yuda alitoka mahali pa mkutano na tena wakati wa kumtukuzwa kwa Yesu na Baba yake: “Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake”.

      Mazungumzo ya Yesu na Yuda na kuondoka kwake kulikwa maandalizi kwa kipindi kifuatacho cha zawadi kubwa ya amri mpya kama urithi wa Yesu kwa watoto wadogo wake. Yesu alikuwa akizungumza nao kama vile mama na baba wanavyofanya na watoto wao. Yeye alishiriki nao hisia zake na kitu muhimu sana, yaani, amri mpya ya upendo. Kwa upande wa wanafunzi amri hii siyo amri mpya kwa sababu imekwepo tangu Agano la Kale. Lakini wanaalikwa kuiishi kwa njia mpya, kulingana na njia aliyowafundisha Yesu. Basi, pamoja na zawadi ya amri hiyo Yesu aliwaonyesha jinsi ya kuishi zawadi hii. Kipimo cha upendo wao kinapaswa kufuata upendo wa Bwana wao, yaani njia yao ya kupendana inapaswa kufuata njia aliyochagua Yesu.

      Yesu anawapenda wanafunzi wake mpaka upeo, kwa sababu hajui kupenda kwa njia nyingine. Ilikuwa kwa upendo kwamba Mungu alimtoa Mwanawe pekee kwa wokovu wa ulimwengu. Upendo tu uliimarisha kazi yake katika nyakati zote. Ilikuwa kwa upendo kwamba Mwana wa Mungu aliutoa uhai wake. Umuhimu wa mafundisho yake ni upendo kama amri mpya na kama maana ya utambulisho wa wanafunzi wake. kupitia kupendana wao kwa wao kama Yesu alivyowapenda watu wote watawatambua kama wafuasi wa Yesu. Upendo wa Yesu ndio msingi wa furaha yake, yaani, furaha ya ushirika wake na Baba, furaha ya kuishi miongoni mwa binadamu, furaha ya kuwachagua baadhi ya wanadamu kama washirika kwa ajili ya kazi yake na furaha ya kuutoa uhai kwa ajili yao. Akiushiriki upendo na wafuasi wake, Yesu aliyajaa maisha yao kwa furaha kubwa, kwa maana kuna uhusiano wa ndani kati ya upendo na furaha. Mtu anayependa kwa kweli yu mwenye furaha ya kweli.

       Kwa kupitia mfano wa unyenyekevu na utumishi Yesu aliwapa wafuasi wake amri yake mpya. Basi, mfano huu unakuwa ushuhuda wetu wa kwanza kwa ajili ya kutangaza Yesu na mafundisho yake. Uzoefu wetu wa undugu unapaswa kuwa maonyesho ya imani yetu, kama ilivyotokea na uzoefu wa Wakristo wa kwanza ambao watu walisema, “Mwone kama wanavyopendana!” Upendo wao ulionyeshwa kupitia makaribisho wao kwa wao, kushiriki pamoja, ishara za mshikamano, uvumilivu katika maombi pamoja na unyenyekevu wa moyo. Tunaalikwa kuchukua hayo kama mpango wa maisha. Upendo unapaswa kuwa umuhimu kati yetu na maana ya kazi zetu. Kupitia kupendana tu tunaweza kujitolea kama vile Kristo na kuwafanya wanafunzi wapya kwake. Kupitia kupendana tu tunakuwa wajumbe wa habari njema kwa wote. Kupitia upendo tu twatambua kwamba sio sisi ambao tunaofanya kazi wala hatutendi peke yetu bali ndiye Mungu ambaye kupitia sisi anafanya yote na kwa upendo.

Fr Ndega                                                                                                                                                                                                                                                                                               

Nenhum comentário: