domingo, 26 de maio de 2019

KUWA MAKAO YA MUNGU



Kutafakari kutoka Mdo 15,1-2.22-29; Ufu 21, 10-14.22-23; Yoh 14, 23-29



       Ujumbe muhimu wa maandiko haya ni kuhusu uwepo na makao ya Mungu ulimwenguni na ndani ya kila mtu kupitia upendo. Hali hii inatualika kufanya upya ahadi zetu za waliobatizwa na kuboresha uhusiano wa kweli na yule ambaye anapendezwa kukaa ndani yetu.

      Hali ya somo la kwanza inaongea kwamba mwanzoni mwa kuinjilisha wanafunzi wa Yesu walihitaji utambuzi sana watangaze habari njema ya Yesu bila kipimo na masharti. Baadhi ya desturi za binadamu ni kama mzigo katika uhusiano wa watu na Mungu. Mazungumzo ya Paulo na Barnaba pamoja na mitume wengine wameongozwa na Roho Mtakatifu ni mfano wazi kuhusu njia ya Kanisa ya kutenda ili liweze kutatua shida na magumu miongoni mwa wana wake kwa sababu ya tofauti ya tamaduni, ya mawazo na kadhalika. Matokeo ya mwendo huu ni kutia moyo kupitia waraka wa mwongozo kwa ajili ya jumuiya na ya kujenga mwili mzima. Kulingana na mtazamo wa Yohana, Mungu alifanya makao duniani na kupitia Yesu, aliye hekalu la kipekee tunaloweza kukutana na Mungu kwa kweli. Lengo la safari yetu kama Watu wa Mungu ni kushiriki katika utukufu wake na kutia nuru kupitia Mwana wake aliye mwanga wa ulimwengu.

      Katika injili tuko na hotuba ya kuaga ya Yesu anayewashauri wafuasi wake walishike neno lake kama alama ya upendo wao kwake. Wanafunzi wana maana nzuri ya kufanya hivyo kwa maana hiyo ni njia maalum ya kuwa makao pa Mungu. Uhusiano wa ushirika kati ya Mwana na Baba na Roho Mtakatifu sio kufungwa bali ni mwaliko wa ushiriki wa wale watakaoendelea kazi ya Yesu ulimwenguni. Kipimo cha mwendo huu ni neno lake linalo asili katika Baba na linapatikana  kwa wote kupitia tendo la Roho Mtakatifu. Roho huyo ni Msaidizi anayeweza kubadilisha maisha ya yeyote anayejifungua kwa neno la Yesu. Wanafunzi wanaalikwa kuishi hatua mpya katika safari yao na maneno haya ya Yesu ni faraja inayotoa ujasiri ili wapate kushinda kila hofu.

      Yesu hakuwaacha kama walio yatima. Yeye atatoweka kwa kimwili lakini ataendelea kuwepo miongoni mwao kupitia upendo. Mahali ambapo Yesu yupo vivyo hivyo Baba na Roho Mtakatifu wapo. Ikiwa mara iliyopita (Yoh 13, 31-35) tulitafakari kuhusu haja ya kupendana kama Yesu alivyopenda, sasa muhimu ndio upendo wao kwa Yesu aliye njia ya kweli ya kumkutana na Mungu. Yeye, pamoja na Baba na Roho Mtakatifu wanakuja daima kwetu na kutarajia kukaribishwa vizuri. Ujio wao maishani mwetu ni ufanisi sana, kulingana na Baba wa Kanisa Gregori, yaani, “wanakuja kwetu twende kwao; wanakuja kusaidia wakati wa dhiki; tunakwenda kwao kwa kutii; wanakuja kwa kutuelimisha, tunawaendea kwa kutafakari; wanakuja kwa kutujaza, tunawaendea kwa kushikilia; ufunuo wao si wa nje bali wa ndani; makao yao kwetu si ya muda bali ya milele. Imesemwa tutakuja kwake na kufanya makao kwake.”  

       Yesu anaongea kuhusu Baba kwa hamu na kutambua sana msaada wa Roho Mtakatifu katika kazi yake. Huu ni mwaliko wa tuishi uhusiano mpya miongoni mwetu hata tufikirie wengine muhimu kuliko sisi wenyewe na tena kutambua kazi yao muhimu kuliko zetu. Ufunuo wa Yesu unaleta changamoto kwetu tulioalikwa kuendeleza kazi yake. Anataka kwamba kupitia maneno na matendo yetu dunia ikamjue. Bila shaka kwamba tunapaswa kuwa waaminifu na mwendo huu ni matokeo ya kulisikia na kulishika neno lake. Tendo hili ni kipimo cha upendo wetu kwake. Tunaweza kufanya hili kwa sababu alikuwa yeye aliyetupenda kwanza na kuja kwetu. Wakati tunalishika neno lake Yesu tunaruhusu kuingia kwa Utatu Mtakatifu ndani yetu. Tunajua kwamba hali hii ni kweli tangu ubatizo wetu, lakini sio daima tumeishi kulingana na uwepo huu. Tuchukue nafasi hii ili kufanya mpya urafiki wetu na uwepo huu maalum ndani yetu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: