sábado, 18 de agosto de 2018

KUMLA KRISTO KUNAMAANISHA KUINGIZWA NAYE



Kutafakari kutoka su Mit 9, 1-6; Waef 5, 15-20; Yoh 6, 51-58


     Yesu ndiye chakula ambacho Mungu alitupa na kuendelea kutupa ili tuwe na maisha kamili. Kutoka Umwilisho wa Neno mpaka msalaba na Ufufuko, maisha ya Yesu yalikuwa kujitolea daima kama chakula cha Mungu kwa ajili ya maisha ya watu wake. Ekaristi takatifu tunayosherehekea inatuhakikishia kwamba ukarimu wa Mungu haumaliziki, kweli utaendelea hata milele. Kila siku Kristo hufanya upya ishara yake ya upendo kwa ajili ya wokovu wetu. Yeye mwenyewe anatualika kwa karamu ya uzima, anajitoa kama chakula na kututumikia kama yule ya pekee ambaye anaweza kujaza moyo wetu unaomtamani Mungu na uhai wake sawa. Lengo la Ekaristi ni kufananisha maisha yetu kidogo kidogo kulingana na maisha ya Yule tunayepokea.

     Andiko la kwanza linaongea kwamba hekima ya Mungu imewakaribia wanadamu ili kuingizwa nao. Mwenye hekima ni yule anayekaribisha hekima hii na kuishi kulingana na msukumo wake. Kwa hekima ya kimungu tuko na nafasi kamili, chakula kamili ili tubadilishe mawazo yetu na kutembea kuelekea kwake. Hekima hii ndiye Mwana aliyefanyika mwili na kujitoa ili tumle kwa ajili ya kuishi kama wenye hekima sio wajinga, kulingana na yale anayosema Mtakatifu Paulo katika andiko la pili. Mapenzi ya Bwana ni tuweze kutumia vizuri wakati ambao tumepewa tukitafuta kula hii “Hekima iliyofanyika mwili” kwa ajili yetu ili tuishi kwa sababu yake.

        Katika injili Kristo aliwaalika wasikilizaji wake kuukaribisha ufunuo juu ya utambulisho wake kama chakula kilichoshuka kutoka mbinguni si kwa binadamu tu bali kwa ajili ya uhai wa ulimwengu wote. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata alimtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele (Jo 3, 16)”. Mwana anajitoa kama chakula kinachodumu hadi uzima wa milele kwa sababu ya mapenzi ya Baba aliye chemchemi ya uzima. Yeye ndiye anayesababisha uzima ndani ya kila mtu anayempokea Mwanawe. Tunaongea hapa kuhusu kiini cha mafundisho ya Yesu kama mwokozi na mkombozi wa ulimwengu, lakini wasikilizaji wa Yesu hawakuweza kuelewa kwa sababu walijua hali ya Yesu ya kibinadamu. Kweli alikuwa na ugumu wa kukubali kwamba mwenzao huyu alishuka mbinguni wala kuwa chakula kwao. Lakini ugumu wao haukumzuia Yesu ya kufunua njia iliyojaa maana kwa maisha yao.

     Yesu anaongea kuhusu uzima bila mwisho unaopatikana kwa wote. Inawezekana kuupokea uzima huu kwa kuula mwili wake na kuinywa damu yake, kwa sababu yeye ndiye uhai na huishi ndani ya wale wanaompokea. Yesu anatenda ishara hii ya upendo kwa uhuru kabisa na kulenga kukaa miongoni mwa wanadamu na ndani ya kila mtu. Hiki ndicho kipimo cha kupata uzima. Hilo ndilo fumbo la Ekaristi takatifu. Ndiyo zawadi kutoka kwa Mungu ambaye hataki kuishi mbali na binadamu. Ekaristi ni hazina ya kanisa na kiini cha uzoefu wake. Ekaristi inalifanya Kanisa na Kanisa linaishi kwa Ekaristi. Kulingana na Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa pili, “matendo yote ya Kanisa yatoka kwa Ekaristi na kulenga Ekaristi”. Ndivyo hivyo kwa sisi sote tunaoumega mkate mmoja na kunywa kikombe kimoja. Uzoefu huu ni ukamilifu wa ushirika wetu na Mungu na msukumo kwa ahadi yetu ya kindugu.

      “Tunapokula chakula cha kawaida mwili wetu unaingiza chakula hiki ili uwe na afya nzuri. Hivyo, chakula kinaingizwa na mwili wetu. Kuhusu Ekaristi, chakula cha uzima, matokeo ni tofauti: wakati tunampokea Yesu, ni sisi tunaoingizwa naye”. Kwa maneno mengine, Yesu anatuingiza, anatuchukua kwake ili tuishi naye na kwa sababu yake. Yeye anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Yeye anatuunganisha naye, kutuhusisha katika ushirika sawa anaoishi na Baba. Katika uzoefu huu tunabadilika kuwa yule tunayempokea kwa ajili ya ukuaji wa mwili mmoja. Hivyo, wakati tunaposherehekea Ekaristi kwa kina mahusiano kati yetu yabadilika na sisi tunakuwa vyombo vya umoja, upatanisho na amani kulingana na hisia za Kristo.

Fr Ndega


Nenhum comentário: