sexta-feira, 23 de fevereiro de 2018

NI VIZURI KUWA HAPA NA KUJIFUNZA KUISHI KAMA WAPENDWA



Kutafakari kuhusu Mk 9, 2-10


           Nafasi hii injili inajulisha kugeuka sura kwa Yesu na mwaliko wa kugeuka sura kwetu wenyewe, hasa katika wakati huu wa Kwaresima. Tunaweza kukuta tukio hili tena katika wainjilisti wengine, yaani Mathayo e Luka, kwa tofauti fulani, kulingana na mwinjilisti mwenyewe. Kwa mfano, mara mwanzoni mwa andiko hili la Marco, tunakuta maneno “baada ya siku sita”. Tena tunakuta maneno haya katika Mathayo lakini katika Luka ni tofauti kidogo, yaani “takriban baada ya siku ya nane”. Basi, tuanze kutoka tukio lililotokea siku sita ama ya nane ya injili ya leo, yaani Yesu alitangaza kujisalimisha kwake na kujulisha mahitaji ya kumfuata. Kisha, Yesu alichukua wanafunzi wa tatu na kupanda mlima mrefu. Mlima una maana kubwa katika biblia. Kama jangwa, tuliyotafakari mara iliyopita, mlima ni pia mahali maalum pa uzoefu wa Mungu. Yesu alipanda mlimani mara nyingi na matendo yake mengi yalitokea huko.

      Kulingana na desturi ya Kikristo, mlima wa kugeuka sura unaitwa Tabor, wengine watalaam wa Biblia wanasema kwamba huko ni mlima Hermon. Hata hivyo, ni muhimu kujua kwamba ulikuwa mlima mrefu na huko Yesu aligeuka sura mbele ya wanafunzi wake. Mwinjilisti Marko anaongea kuhusu mavazi ya Yesu lakini haongei kuhusu uso wake kama tunavyokuta katika injili ya Mathayo. Yesu aliwaonyesha kidogo utukufu wake na hali ijayo ya maisha ya wale wanaomfuata kwa uaminifu. Yesu aliwaalika kwa uzoefu wa juu ili waone vizuri hali ya kujisalimisha kwake na hali wanayoalikwa kuichukua kama ushiriki katika kazi ya Mwalimu wao. Basi, sio Yesu peke yake aligeuka sura bali wanafunzi pia walivyo kwa sababu waliweza kuona tofauti.

         Uwepo wa Musa na Elia unaeleza kuhusu rejeo la ufunuo katika Agano la Kale. Wote wawili waliongea na Yesu wakionyesha kwamba hakuna kupasuka kati ya mafundisho yao na yale ya Yesu, bali uhusiano na mwendelezo. Lakini kulingana na sauti iliyosikika kutoka kwenye wingu ndiye yeye kwa uwezo wa kufundisha na kutafsiri kamili yale yaliyosemwa na mababu wa zamani. Baba alishuhudia kwa upendo kuhusu Mwana wake, akimweka kama rejeo la maisha yetu, yaani, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni”. Wote wanaalikwa kumsikiliza. Kusikiliza katika Biblia ni kitenzi chenye nguvu sana. Hii ni tabia kamili ya mtu mbele ya Neno la Mungu, akifanya mazoezi kuhusu yale aliyosikia. Basi, kusikiliza kuna uhusiano wa ndani na kushika/kutenda.

       Yesu ni ufunuo wa kipekee wa Mungu. Hakuna mwingine ambaye aweze kumdhihirisha Mungu kama Yesu alivyo. Kweli Mungu aliongea wakati wa zamani kwa mababu zetu. Lakini “siku hizi” mambo yote Mungu anayoendelea kudhihirisha kwa watu anafanya kwa njia ya Mwanawe Yesu. Hata wale ambao hawamjui Yesu wanapokea ufunuo wa Mungu kwa njia yake. Katika kila ndugu wanayemsaidia wanaweza kukutana na Kristo ambaye alijitambulisha na walio na mahitaji mengi (cf. Mt 25,31-46). Kipimo ni upendo/huruma. Matendo yao ya huruma yanaongelea Kristo.

   Wanafunzi walitamani kubaki mlimani, lakini sauti iliyotoka mbinguni ikawaalika kumsikiliza Yesu na kutoka nje ya uzoefu huu wamepatikana kuandamana naye mpaka upeo. Mara nyingi Mungu ametualika kufanya uzoefu wa uwepo wake kama ilivyotokea kwa wale mlimani, mfano, wakati tunaposhiriki katika sherehe fulani ama siku za maombi, uzoefu wa undugu na kadhalika. Uzoefu kama huu unaiimarisha imani yetu na hamu yetu kwa ajili ya kazi ya Mungu. Lakini safari yetu yapaswa kutendeka kati ya “kupanda mlimani” (mfano wa uzoefu wa Mungu wa kibinafsi) na “kushuka mlimani” (mfano wa changamoto za undugu na kazi). Kila siku tunaalikwa kufanya uzoefu wa “kugeuka sura” kupya kwa kusikiliza Neno la Yesu na kufanya mazoezi kuhusu Neno hili. Uzoefu huu unatusaidia kutambua uso wa Yesu katika nyuso za ndugu wengi kandokando yetu na kuona hisia na tabia za yake kwa ajili yao. “Kusikiliza neno lake kunatupatia nguvu ya kumfuata mpaka mwisho.” Hii ni njia kamili ili tuweze pia kuishi kama “wana wapendwa” wa Mungu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: