domingo, 26 de novembro de 2017

HUKUMU IMEKWISHA ANZA


           Tafakari kutoka Ezekieli 14: 11-12.15-17; 1Kor 15: 20-26.28; Mt 25: 31-46




        Maandiko haya yasema kwamba Mungu ni kama Mfalme Mchungaji ambaye anawajali wana kondoo wake na kuwa na upendo maalum hasa kwa ajili ya wasio na nguvu. Tabia yake ni kipimo cha matendo yetu. Upendo na huruma kwa wenzetu walio na shida ya kimwili ndio kipimo ili tuweze kuingia katika ufalme wake. Tutafakari kuhusu fumbo la Ufalme huu na kukaribisha mifano ya huruma ya Kristo kama msukumo ili tufanye vivyo hivyo.

    Kwa jina la Mungu, Nabii Ezekieli anawashutumu viongozi wa Watu wa Israeli kwa sababu tabia yao ya kutowajibika ilisababisha uhamisho wa Babeli, yaani, kipindi cha huzuni na mateso kwa watu hawa. Lakini katika ujumbe wake, nabii anatangaza pia utunzaji wa Mungu kwa ajili ya watu hawa. Yeye atawaongoza kwenye hali mpya kama vile mchungaji kwa ajili wa wana kondoo wake. Unabii huu unapata mafanikio yake kwa ukombozi toka uhamisho. Unabii huu ndio pia tangazo la kazi ya Yesu Kristo kama Mchungaji Mwema aliyesalimisha ili wanadamu wote wapate maisha mengi. Kulingana na Mtakatifu Paulo, Yesu alishinda nguvu zote duniani, kupitia kifo chake na ufufuo wake, akiwaokoa wanadamu wote na kuanzisha Ufalme wa Mungu Baba yake. Wanadamu wote wanaalikwa kuingia katika ufalme huu. Lakini ni lazima kuungana na Kristo na kutenda kulingana na mapendekezo yake ili Mungu awe yote katika wote.  

    Andiko hili ya Injili linajulikana kama “Hukumu ya mwisho” na wengi kati yetu wanapendelea kumfikiria Yesu kama “hakimu” atakayekaa kitini chake akiwahukumu wanadamu, kuwatuza wengi na kuwaadhibu wengine kama wafalme wa ulimwengu walivyo. Lakini hatuwezi kusahau yale aliyosema, yaani “Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili kuwa hakimu wake, lakini kwa kuwa mkombozi wake” (Yohane 3, 17). Hivyo, lengo lake sio kuhukumu bali kuokoa kwa sababu ya upendo na huruma yake. Basi, inawezekanaje kufahamu andiko hili la Mathayo linaloongea kuhusu hukumu? Kwanza kabisa aina hii ya andiko ndiyo ya kifunuo ambayo inatumia ishara nyingi ili kuongea kuhusu hali iliyokuwa ikitokea katika wakati ule.

      Wainjilisti wanaonyesha kwamba Yesu alikataa cheo cha mfalme katika wakati wa utukufu, na kukubali katika wakati wa kushindwa, mfano msalaba. Upinzani wake kwa cheo hiki ulikuwa kwa sababu ya mawazo ya kisiasa ya watu kuhusu suala hili. Yeye anatumia mfano wa mfalme katika andiko hili ili kuelea maana kamili ya Ufalme na lengo lake kama Mfalme. Ufalme wake sio kutoka ulimwengu huu nao hauwezi kuonekana (kama ndipo huko au ndipo hapa). Yesu hakufafanua Ufalme wa Mungu ni nini, lakini alisema kwamba ndio tayari kati yetu nasi tunaweza kuhisi tukio lake kwa kupitia matendo mema kwa ajili ya wengine. Yesu ndiye mfalme aliyekubali msalaba kama kiti chake cha enzi alipoonyesha ishara kubwa ya upendo kwa ulimwengu. Hukumu imekwisha anza kwa sababu mfano wake wa kupenda na kuwa na huruma ni kipimo cha kutenda. 


        Mfalme huyo anataka kuwakusanya watu wote kuzunguka naye katika ufalme wake kama mchungaji anavyofanya kwa kundi lake. Yeye anajitambulisha na ndugu wadogo na kuyaanzisha matendo ya upendo na huruma kwa ajili yao kama kipimo cha wokovu. Maneno yake yanatusaidia tufanye utambuzi na chaguzi zetu zinatuhukumu. Aina ya mahusiano yetu na wale walio na shida na wadogo inatuhukumu. Sehemu ya mwisho ya hukumu itakuja kwa wote nayo inapaswa kuwa ukamilifu wa maisha yetu kwa sababu mambo yote ambayo tumeishi ndiyo maandalizi kwa wakati huu. Tutakapokutana na Mungu, hatutaulizwa ikiwa tumeshiriki katika dini fulani wala mara ngapi tulienda kanisani, bali kiasi gani tuliweza kupenda. Kwa hivyo tuko na ishara za Kristo kwa ajili ya wadogo kama mfano. Mambo yote ambayo tunaweza kufanya kwa ajili yao ndiyo kwa Kristo tunayofanya. Hatuhitaji kuacha ubinadamu wetu ili kukutana na Mungu. Yeye mwenyewe anajiruhusu kukuta katika ubinadamu wetu, hasa wakati ubinadamu huu unateseka. Ndizo chaguo zetu zitakazoamua mwelekeo wa maisha yetu. Tusisahau kwamba mapenzi ya Mungu ni kwamba maisha yetu yapate ukamilifu na kwa hivyo anakaa ndani yetu kwa njia ya Roho wake. Tumpe nafasi ya kutenda kwa sababu, “Ikiwa Mungu yumo ndani yetu, tutafanya yale mema hata kwa kupita kwetu tu”.

Fr Ndega

Nenhum comentário: