segunda-feira, 20 de fevereiro de 2023

WAKATI MWAFAKA UMEANZA

 

Kutafakari kutoka  Yoe 2, 12-18; 2Kor 5, 20-6:2 Mt 6, 1-6; 16-18




 

    Kupitia sherehe hii ya Majivu tumeanza wakati wa kwaresima. Kwaresima ni siku arobaini za maandalizi kwa adhimisho la fumbo la Pasaka ya Kristo. Wakati huu unatukumbusha siku arobaini ambazo Musa alibaki milimani Sinai; pia miaka arobaini ya Wana wa Israeli jangwani; tena siku arobaini za Eliya akitembea mpaka milima Horebi na siku arobaini za Yesu jangwani aliyeongozwa na Roho Mtakatifu.

    Wakati wa kwaresima unalenga kuwa uzoefu wa jangwa. Kwa upande wa viongozi wengi katika biblia jangwa palikuwa mahali pa mkutano na Mungu kwa hamu na uzoefu wa utakaso. Walitafuta mahali huko kabla ya matukio muhimu maishani mwao ili waweze kuchukua ahadi kwa nguvu na uaminifu. Vivyo hivyo, ni Kwaresma kama maandalizi kwa tukio muhimu sana la imani yetu, yaani Ufufuko wa Yesu.   

    Huu ni wakati kwa kutafakari kwa njia ya ndani kuhusu huruma ya Mungu na hali yetu ya wenye dhambi. Dhamiri kuhusu matokeo ya dhambi katika maisha yetu inatuongoza kumwomba Mungu kulingana na somo la kwanza, yaani “Wahurumie watu wako ee Bwana!” nasi tunajua kwamba Mungu anawahurumia watu wake sio kwa sababu tunastahili, lakini kwa sababu hii ni tabia yake ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa rehema.

    Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “Mbele ya hali kubwa ya dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima.” Kwa hivyo tunaalikwa kumrudia yeye kwa imani kubwa na kuutumainia wokovu wake.

    Somo la pili linaongea kuhusu mahitaji ya upatanisho na Mungu kwa sababu yeye mwenyewe anatupa nafasi ya kufanya hivyo kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Huu ni wakati wa neema, nasi hatuwezi kuipokea neema ya Mungu bure. Hebo tuonyeshe tabia ya toba kutoka ndani! Tubuni na kuiamini injili”, asema Yesu. Wakati wa mabadiliko na wa wokovu ndio sasa.

    Katika dini ya kiyahudi, kuna hatua tatu muhimu sana ambazo zinadhihirisha utambulisho wa myahudi wa kweli, yaani sala, sadaka (itolewayo kwa maskini) na kufunga. Hasa wakati huu wa kwaresima tunaalikwa kuchukua hali hizi kama ishara ya toba yetu. Yesu alipopendekeza hatua hizi tatu, yeye aliwakumbusha wafuasi wake kuhusu tabia ya roho ambayo inapaswa kutoa maana kwa hatua hizi. Wakati wa Yesu, kufunga kulikuwa shughuli ya kawaida, naye pia alifunga kwa wakati wa siku arobaini jangwani kabla ya kuanza ujumbe wake kwa umma.

    Yesu alitaka kwamba wanafunzi watende kwa tabia ya kweli sio kama ile ya baadhi ya watu (wanafiki) ambao walipofunga wakaonyesha huzuni ili wapate kuonekana kwa watu kuwa wanafunga. Yesu alitokubali tabia hii na kusema kwamba wamekwisha pata tuzo lao. Kufunga kwetu tulio Wakristo ni tabia ya toba na ya ushirikiano na Kristo ambaye alifunga kwa siku arobaini na baadaye aliteseka kwa ajili yetu. Mtakatifu Agostino alisema kwamba “kufunga kwetu ni halali ikiwa kunachoma ndani yetu tamaa ya kumwona Kristo”. Kufunga kunalenga kutusaidia kujinyima wenyewe ili tuwe watu bora. Tunaweza kueneza ujumbe huu hasa kwa ajili ya kufunga baadhi ya maneno, ya matendo na ya mawazo ambayo si mazuri katika uhusiano wetu na wengine.  

    Kuhusu sala, ni vizuri pia kuufuata mfano wa Bwana wetu. Yeye alikuwa mtu wa sala na aliijulisha sala kama njia kamili ya kuwa mwaminifu kwa mpango wa Mungu. Sala yake ilikuwa maonyesho ya uhusiano wa ndani na Baba na mwaliko ili wanafunzi wake wafanye vivyo hivyo kama utambulisho naye. Kwaresima ni wakati wa sala kwa hamu zaidi, kwa kufungua akili zetu na mioyo yetu kwa tendo la wokovu wa Mungu. Huu ni wakati pia wa kutenda matendo ya huruma kwa wenzetu, kwa kuonyesha juhudi yetu ya kubadilisha hali yetu na kandokando yetu. Majivu usoni ni ishara ya udhaifu yetu na kukubalika kwetu kuhusu mwaliko wa Kanisa wa toba kwa sababu wakati wa kuukaribisha wokovu wa Mungu na kuiamini injili ndio sasa.   


Fr Nega

Nenhum comentário: