sábado, 11 de janeiro de 2020

KATIKA MWANA MPENDWA SISI TU WAPENDWA PIA



Kutafakari kuhusu Isa. 42:1-4, 6-7; Mdo. 10:34-38; Mt 13: 13-17




      Tunasherehekea sikukuu ya ubatizo wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Hii ni mwisho wa Wakati wa Krismasi na mwanzo wa Wakati wa Kawaida. Kama ubatizo ni mwanzo wa maisha yake hadharani, katika liturjia hii ni nafasi ili tuandamane naye katika kazi yake ya kawaida huko Palestina. Hii ni nafasi maalum pia ya kuukumbuka ubatizo wetu na kuweka upya ahadi ya kuwa Wakristo, kwa kuishi wito wetu wa wana wa Mungu kama Kristo alivyo.

     Yesu ndiye mtumishi wa Bwana, aliyetabiri na Isaya, kulingana na somo la kwanza. Mungu mwenyewe anajulisha mtumishi wake kama yule ambaye anatenda kulingana na mapenzi yake kwa sababu hatumii mamlaka yake kwa manufaa yake mwenyewe bali anapenda kuishi kama “agano la watu na nuru ya mataifa.” Hivyo uwepo wake duniani ni mafanikio ya wokovu  wa Mungu  kwa wote hasa kwa ajili ya walio na shida nyingi.

       Kulingana na kitabu cha Matendo, Petro anatangaza amani kwa kupitia Yesu aliyefanya kazi njema kwa maisha ya watu kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. Vivyo hivyo kwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo, yaani tunaalikwa kuishi kama Kristo kwa kuendelea utume wake kwa manufaa ya Kanisa na wokovu wa binadamu kwa sababu yeye yuko pamoja nasi. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya ubatizo wetu ulio ushiriki katika uhai wake wenyewe.

      Katika Injili tuko na mkutano maalum kati ya Yesu na Yohana ambaye alikuwa akibatiza. katika wakati wa kwanza Yohane alikataa kumbatiza Yesu kwa sababu alijifikiria mwenyewe kama sauti tu wala asiyestahili kufungua ukanda wa viatu vyake. Baadaye Yesu mwenyewe atatambua ukuu wa Yohane akiweka unyenyekevu wake kama mfano kwa safari yetu. Yohana aliwabatiza watu kwa maji kama ishara ya kugeuka kwao kutoka dhambi. Lakini Yesu hakuwa na dhambi, basi, kwa nini alikubali kubatizwa?

    Kwa Yesu ilikuwa nafasi ya kuonyesha mshikamano wake kuhusu kazi ya ajabu ya Yohana, kuthibitisha kwamba Mungu anatarajia watu wake warudi kwake. Wakati wa ubatizo wa Yesu Mungu mwenyewe alimjulisha akisema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe”. Sauti hii itasikika tena katika tukio la milima. Huko milimani Mungu Baba alionyesha pendo lake kumhusu Mwanawe akiwaalika wote wamsikilize na kuishi kama wapendwa kama Yesu. Matukio mawili yalenga kutuhusisha katika ushirika wake na Baba.

       Yesu alionyesha pia unyenyekevu akijifananisha na binadamu ambaye ana udhaifu na kuhitaji kuishi katika ushirika na Mungu. Yesu alikuja si kuishi kujitengwa na watu bali aishi kuhusishwa katika safari yao. Kabla ya Yesu maji yalikuwa na nguvu ya kutakasa mwili pekee yake. Kutokana na uzoefu huu Yesu aliyatakasa maji ili yawe na nguvu ya kutakasa pia roho ya watu, yaani maji ya ubatizo.

      Baada ya kupokea ubatizo wa Yohana na kujulishwa kama Mwana mpendwa wa Mungu Yesu aliwezeshwa na Roho Mtakatifu ili aanze kazi yake akipendekeza uzoefu huu kwa wote ambao wanataka kuwa watoto wapendwa wa Mungu. Tunaweza kusema kwamba ubatizo ambao Yesu anapendekeza ni uwezo wa kushiriki katika uzoefu wake wa Mwana wa Mungu. Ubatizo huu ni ishara ya utambulisho wa Kikristo, yaani Ubatizo wa Roho Mtakatifu na kwa moto, kulingana na maneno ya Yohane Mbatizaji.

      Ubatizo huu una nguvu ya kufanya mabadiliko katika maisha ya mtu yeyote kwa sababu unamfanya kuzaliwa katika familia ya Mungu. Alama yetu kama watoto wa Mungu haiwezi kufutika. Ipo daima! Tunaweza kuishi maisha mapya ambayo ni zawadi ya Kristo mwenyewe na matokeo ya utume wake. Ubatizo wetu, pamoja na maondoleo ya dhambi, unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe.

      Kupitia alama hii ya nje tunakufa kweli kwa maisha ya dhambi, na pia tunapitia ufufuko wa maisha mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga wa kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Yeyote akimfuata hatatembea gizani bali atakuwa na nuru ya milele. Kupitia mwendo huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika mwanga wa Mungu kila siku ya maisha yetu. Ekaristi hii itusaidie kuishi lengo hili la safari yetu ya Kikristo, walio wana wapendwa wa Mungu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: