sábado, 14 de julho de 2018

NJIA KAMILI YA KUWA WANAFUNZI WA YESU


Amosi 7: 12-15; Waefeso 1: 3-14; Mk 6: 7-13



         Nabii Amosi alichaguliwa na Mungu ili kutabiri katika hali ngumu ya watu wa Israeli (Ufalme wa Kaskazini), yaani, kukosekana kwa usawa wa kijamii, udhalimu dhidi ya maskini na matumizi ya dini kulingana na mvuto binafsi wa mfalme. Wakati wa mfalme Yeroboamu wa II, pamoja na hekalu kuu la Yerusalemu (Ufalme Kusini) lilikuwako pia hekalu lingine lililoitwa Betheli (Kaskazini). Amosi alipoanza kazi yake katika mahali huko, alikutana na kuhani wa hekalu la Betheli, aliyeitwa Amazia, ambaye alifanya upinzani dhidi ya unabii wa Amosi. Amazia ni aina ya mtu aliyelipwa ili kudumisha mfumo wa hekalu na kuhalalisha mfumo wa kidhalimu wa mfalme. Ingawa Amosi alitendewa vibaya, tabia yake ni tofauti, yaani alipendelea kumwelezea Amazia maana ya wito wake. Ujumbe wa Amosi kama nabii hautegemei malipo, bali ni maonyesho ya ukarimu na mapenzi ya Mungu anayeruhusu kuguswa na hali ya maskini na ya wanaoteseka.

          Somo la pili ni wimbo wa shukrani kwa Mungu ambaye ametubariki sana katika Kristo tangu mwanzo wa ulimwengu ili tuwe watoto wake. Kwa ujumbe wa Yesu Kristu tumesamehewa dhambi zetu ili tuweze kuishi wito wetu kwa utakatifu. Wito huu ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Mungu ambaye katika Kristo ametuchagua ili tuwe watu wake mwenyewe. Roho wa Mungu anatusaidia kuishi wito wetu kwa uaminifu na kutupatia utimizaji wa ahadi yake. Kulingana na Baraza ya Vatikano ya II utakatifu ni wito wa wote tangu ubatizo wetu na Mt Yohana Calabria anasema kwamba “hatuhitaji kufanya mambo ya ajabu ili tuwe watakatifu. Tunaweza kuwa watakatifu kupitia hali ya kawaida. Yatosha nia zetu ziwe takatifu katika mambo yote.”    
   
       Baada ya kukataliwa kijijini chake, Yesu aliendelea na ujumbe wake vijijini vingine kandokando huko ambapo alikaribishwa vizuri sana. Aliweza kufanya kazi yake peke yake, bali hakutaka. Kwa hivyo aliwaita Mitume kumi na wawili kama washirika. Kabla ya kuwatuma kwa ujumbe, aliwaita ili kubaki naye, yaani aliwapendekezea uzoefu wa nafsi yake. Uzoefu huu ni wa msingi kwa mafanikio ya kazi. Wakati huu alishiriki nao hisia yake kuhusu hali ya watu walioteseka kwa sababu ya nguvu za maovu na ya magonjwa mengi. Mamlaka ambayo Yesu alishiriki nao yalilenga kuwaimarisha watu ili waweze kushiriki kikamilifu katika jamii. Hatimaye, aliwapa maelekezo hasa kuhusu mahitaji ya njia ya unyenyekevu wa maisha na kuwatuma wawiliwawili. 
   
          Ndiye Yesu aliyechukua nafasi ya kuwaalika wanafunzi. Hakuwatafuta wenye nguvu au wenye umaarufu katika jamii. Aliwachagua watu wanyenyekevu, wafanyakazi na walio makini kwa ufunuo wa Mungu kupitia Mwana wake. Yaliyomo ya maelekezo Yesu aliyowapa yanaufuata mwelekeo tofauti kabisa na matarajio ya binadamu. Kwa mafanikio katika kazi, mitume walipaswa kushinda baadhi ya tabia za binadamu ambazo zipo sana maishani mwetu: dhidi ya tabia ya kutenda kwa njia ya kibinafsi, tunaalikwa kutenda pamoja na kusaidiana katika jumuiya na kwa manufaa ya jumuiya. Kazi ya kuinjilisha sio kazi ambayo mtu anachukua peke yake bali ndiyo kazi ya kijumuiya. Dhidi ya tabia ya kutawala, Yesu anashiriki nasi uwezo wake ili tutumikie watu; dhidi ya tabia ya kuwa na mali, Yesu anatupendekezea kujinyima, unyenyekevu na ukarimu.

        Kama wanafunzi wa kwanza tunapaswa kufahamu kwamba tajiri yetu ndilo ujumbe ambao Mungu anatukabidhi. Siyo mali ambayo inaweza kutuhakikishia usalama, bali ndiye Yule ambaye aliyetualika, akatutuma na kuandamana nasi. Dhidi ya tabia ya kulazimisha, tangazo letu ni pendekezo, pendekezo la toba na la mabadiliko ya maisha. Ikiwa mtu fulani hataki kupokea ujumbe wetu, hatuwezi kumlazimisha bali kuheshimu uhuru wake kwa sababu ni kwa uhuru ambao mtu anaweza kukubali pendekezo la Yesu na kumfuata. Wakati tunapokabiliana na upinzani dhidi ya kazi yetu Yesu anatarajia tuweze kushinda hofu na kufanya upya imani yetu katika Riziki ya Mungu ambaye hawaachi wale wanaotumainia yeye. Njia yetu ya kuishi inaongea zaidi kuliko maneno yetu. Pendekezo la toba ambalo tunawatangazia wengine liwe maonyesho ya mabadiliko ambayo tumeona kwa kupitia uzoefu wetu wa huruma ya Mungu. Mungu anataka kuyapatia maisha mengi kwa watu wake na kuamua kututumia kama washirika wake. Tuko tayari?    

Fr Ndega

Nenhum comentário: