quinta-feira, 26 de janeiro de 2023

UTABIRI WA WAKATI MPYA

 

Sf 2,3;3,12-13; 1Cor 1, 26-31; Mt 5, 1-12




 

Maisha kamili yanaitegemea furaha ya kweli ambayo Yesu pekee yake anaweza kutuletea. Yeye alifanya hivyo kupitia kuhudhuria hali yetu ya kibinadamu akianzisha njia kamili ya kuishi. Njia hii inamhusu Mungu nayo inapitia unyenyekevu na haki. Mungu mwenyewe hana macho kwa waliotenda udhalimu wala kwa wanafiki bali kwa wanyenyekevu. Yeye yu makini sana kwa kilio chao naye yuko tayari kuwatendea mema kwa maana maisha yao yanathamini sana kwake. Kupitia Yesu anaonyesha upendo maalum kwao ambao wanamtumainia yeye peke yake.  

Katika andiko la Kwanza, nabii Sefania anatambua ndani ya maskini na wanyenyekevu uwezo mkubwa wa kumtafuta Mungu na kumtegemea yeye katika mambo yote. Mungu anaijua hali ya maskini na ya wanyenyekevu naye anaguswa na mahitaji yao. Maisha ya maskini na ya wanyenyekevu yanashuhudia kwamba kimbilio ambalo linatuhakikishia usalama sio pesa wala ulaji, bali ni Mungu peke yake. Kweli Mungu anapatikana kwa wanaotaka kukutana naye, lakini ni wanyenyekevu wa moyo tu wanaoweza kuuona uso wake, yaani kufanya uzoefu wa uwepo wake.  

Mtakatifu Paulo anasisitiza kuhusu tofauti kati ya mawazo ya Mungu na ya mawazo ya kidunia. Kulingana na mawazo ya kidunia ndio wenye umaarufu, wenye nguvu na matajiri waliotambuliwa kama watu wenye thamani. Badala yake, Mungu anawathamini na kuwasaidia waliodharauliwa na dunia hii yetu, yaani maskini na wanyenekevu. Kama wafuasi wa Kikristo, hatujaitwa kuifuata hekima ya kibinadamu wala kuutafuta umaarufu wa kidunia. Wito wetu unatoka kwa Mungu na kupaswa kuyafuata mawazo yake na njia zake kama Kristo alivyo.    

Andiko la injili ni mwanzo wa ile iliyojulikana kama “Hotuba ya mlimani” iliyotangazwa na Yesu. Hotuba hii kabisa inajumuisha sura tatu, yaani kutoka 5 mpaka 7. Kwanza kabisa ni muhimu sana kuifahamu nia ya Mathayo alipoandika toleo lake. Yeye aliandika kwa Wayahudi na kwa hivyo, alimjulisha Yesu kama “Musa Mpya” na aliye utimilifu. Mambo yote ambayo yanamhusu Kristo yanaileta hali mpya. Hivyo, Mlima wa “heri nane” unatukumbusha hali ya Mlima wa Sinai; ujumbe huu wa “Heri nane” ni mafundisho mapya kuhusu Amri za zamani; upendo wa kindugu ni haki mpya ambayo inashinda haki ya walimu wa Sheria na Mafarisayo, n.k.

Katika biblia, mlima ni mahali muhimu sana. Huko Mungu anajifunua mwenyewe na kufanya agano na Israeli. Tena huko baadhi ya viongozi waliweza kukutana na Mungu na kupokea kutoka kwake miongozo kwa maisha yao na ya watu waliokabidhiwa kwao. Yesu alichagua mahali huko kwa hotuba yake ya kuuanzisha ufalme wa mbinguni, yaani mapendekezo ya kupata furaha ya kweli kulingana na matarajio ya Mungu. Huu ni mpango wa maisha ambao Yesu aliishi kwanza kabla ya kupendekeza kwa wote. Kwa kifupi, ndani ya Heri nane tunaweza kukuta nafsi ya Yesu mwenyewe katika uhusiano wake na Mungu. Katika yeye na kwa sababu yake sisi tu wenye heri. 

Wakati Yesu alipotangaza Ufalme wa Mungu kwa mara ya kwanza, aliamua kuhubiri maneno ya faraja kwa wale waliokuwa na mahitaji na mateso mengi na kumtumainia Mungu, yaani walio kipaumbele katika Ufalme. Kweli, huko hawakwako wenye nguvu ama matajiri, bali maskini kwa aina mbalimbali. Tunahitaji kuchukua andiko hili la Mathayo pamoja na lile la Luka (6, 20-26) linalofanana zaidi na yale aliyofundisha Yesu. Hali ya maskini inagusa sana moyo wa Yesu naye alifanyika mwili akikubali hali hii ili kuonyesha ukaribu wa ufalme wa Mungu hasa kwa ajili ya wanaofunguliwa kwa mpango wa Mungu kuyahusu maisha yao. Ufalme wa Mungu ni wao.

Watu Hawa walionyeshwa na nyuso nyingi, yaani, “walio maskini wa roho ndio wasio na tamaa ya makuu bali wanaweza kuyasalimisha maisha yao mikononi mwa Mungu; wenye huzuni ndio wanaoguswa na uchungu wa wenzao; wenye upole ndio wanaoishi kwa ushirika na moyo wa Mungu; wenye njaa na kiu ya haki ndio wanaojitolea kwa kujenga jamii nzuri; wenye rehema ndio wanaoguswa na huruma ya Mungu ili wawe chombo cha huruma hii; wenye moyo safi ndio wanaoweza kumjua Mungu; wapatanishi ndio wanaosaidia uzoefu wa kindugu katika jumuiya zetu; wanaoteswa kwa ajili ya haki na kwa jina la Yesu ndio walio mashahidi wa wema wa Mungu kati yetu. Ufalme wa mbinguni ni tuzo yao.  

Sisi, tulio wafuasi wa Yesu, tunaalikwa kuchukua ujumbe wa “Heri nane” kama mpango wa maisha. Hatuhitaji njia nyingine ya kuishi kwa ajili ya kupata furaha ya kweli. Mambo yote Yesu aliyotaka kusema kwa wanaotaka kumfuata yapo hapa. Mungu anataka tuwe wenye furaha, lakini njia zake zina masharti yaliyo Heri nane yanayotualika tuweze kubadilisha njia ya kuona na ya kuishi. Hii ni njia ngumu, lakini hatuko pekee yetu. Mungu yu pamoja nasi kwa sababu hawaachi wale wanaomtumainia yeye. Maisha yetu yana thamani kubwa kwake. Jibu linalompendeza ni tuweze kuishi kwa uaminifu yale aliyoishi na kuyafundisha Yesu. Huu ni utabiri wa wakati mpya. Ingawa ufalme upo katika Yesu, yeye mwenyewe anatambua thamani za ufalme huu duniani na katika hali ya jumuiya zetu. Neema yake ituimarishe tuwe vyombo vya thamani za ufalme huu.


Fr Ndega

Nenhum comentário: