Kutafakari kutoka Mt
13, 1-23
Tunataka kutafakari juu ya ufanisi wa Neno la Mungu katika maisha yetu
na majibu yetu mbalimbali mbele ya tendo la neno hili. Kulingana na maneno ya
nabii Isaya, neno la Mungu ni kama mvua na theluji ambazo hazimrudii Mungu bila
kuipandishia ardhi na kuifanya kuota (angalia Isaya 55:10). Hivi ndivyo Neno la
Mungu katika maisha yetu liko. Mungu anapoongea, yeye huumba na kuumba tena,
yaani, anatoa uhai kulingana na mapenzi yake. Picha nyingine ambayo tunataka
kutafakari kwa kina ndiyo “mbegu”, ambayo huleta nguvu kubwa ndani yake
yenyewe, lakini inahitaji mazingira mazuri ya kuzaa matunda. Lengo la Neno ndilo
kuyatimiza mambo yanayompendeza Mungu, yaani, mabadiliko ya maisha yetu.
Katika mwanzo wa injili, watu walikusanyika ili wasikilize Neno la Mungu
kwa kinywa cha Yesu. Tunajua kwamba Katika tangazo la Ufalme wa Mungu, Yesu
alipendelea kutumia lugha rahisi ili watu waweze kuyakaribisha mafundisho yake
vizuri sana. Yeye aliitumia mifano kuihusu hali ya kimungu na hali ya
kibinadamu. Alianza akitumia ishara ambazo watu walizijua na baadaye hatua kwa
hatua aliwafunulia upya wa hali ijayo. Hivyo, Yesu aliwafanya watu waone, kwa
matarajio, uzima ambao anaahidi, akiongeza matumaini ya wokovu moyoni mwao.
Yule ambaye anaongea maneno ya uzima wa milele anataka kusikika, lakini
makaribisho hayakuwa sawa kwa upande wa wasikilizaji wake. Kama matokeo, maneno
ya Yesu hayakuweza kusababisha mabadiliko aliyotarajia. Haya ndiyo mazingira
ambayo mfano wa mpanzi ulizaliwa.
Kuhusu watu
ambao walisikia mifano yake, Yesu alisema, “Mtasikia, lakini hamtaelewa.
Mtatazama, lakini hamtaona.” Kwa upande wa wanafunzi wake, Yesu alisema: “Heri
yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia”. Basi, ikiwa
lengo la mifano ni kuwa lugha rahisi ili watu wafahamu siri za Ufalme, kwa nini
Yesu alianzisha tofauti kati ya wanafunzi wake na watu wengine? Ndiyo kwa maana
wanafunzi wake walikubali mafundisho yake kwa moyo ambao umefunguliwa na kuishi
kulingana na mapenzi ya Mungu. Wengine walikuwa na tabia tofauti. Hao
walimpinga Yesu tangu mwanzo. Katika Yesu hali ya ufalme imekuwa halisi
kupatikana; upinzani dhidi yake ni upinzani kwa mafanikio ya ufalme huu.
Tufikirie sasa mfano wa mpanzi.
Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake nyingi na mbegu zile zilianguka
katika mahali mbalimbali. Kama mpanzi huyo, ndivyo Mungu anavyofanya kwa midomo
ya Yesu. Yeye ameongea sana na Neno
lake lina nguvu ya kuumba na kuzaa maisha mapya. Kwa upande wa Mungu anaona
furaha kubwa kuwaambia watu wake kitu. Kila mazungumzo na Yesu ni mwaliko wa
kufikiri na kutenda tofauti. Mbegu ni Neno la Mungu. Nia ya Yesu ilikuwa
kuongea kuhusu nguvu ya neno lenyewe na kwamba ni lazima kulisikiliza kwa
uangalifu ili neno hili liweze kutimiza mapenzi ya Mungu maishani mwa watu.
Katika Biblia neno kusikiliza linamaanisha vitendo viwili, yaani, kusikia na
kuishi/kushika. Kuhusu mahali pengi, tunafikiria tabia mbalimbali za watu mbele
ya Neno la Mungu na tena matokeo mbalimbali katika hali ya kawaida.
Mbegu zilizoanguka njiani zinaonyesha kwamba mara nyingi tunaposikia
Neno la Mungu, bila ahadi kwa Neno hili tunaruhusu ibilisi aliondoe neno
lililopandwa mioyoni mwetu. Tendo letu hili linaiondoa maana ya Neno. Mbegu
zile zilizoanguka penye mawe zinaonesha kwamba tunaposikia Neno la Mungu
tunapokea kwa furaha, lakini kwa sababu ya imani ndogo sisi husadiki kwa muda
mfupi tu, na tunapojaribiwa sisi hukata tamaa. Zile zilizoanguka kwenye miti ya
miiba ni tunaposikia neno la Mungu, lakini wasiwasi, mali na anasa za maisha
zinatuzuia tubadilishe tabia zetu. Zile
zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni tunapolisikia Neno la Mungu na
kulikaribisha vizuri kwa kuyafananisha maisha yetu kulingana na neno hili. Lakini
hali hii ni tendo la Neno lenyewe kwa neema ya Mungu kwa sababu neno la Mungu
“ni ufanisi na halimrudii yeye tupu.”
Kulingana na andiko hilo, kuna tofauti kati ya moyo wa
wanaomfuata Yesu na wengine wanaomsikiliza tu. Njia ya kupanda mbegu ni mfano
wa ukarimu wa Mungu. Kwa upande wake hakuna mipaka; ni ukarimu tu. Kutoka
ukarimu wake tumepokea neema juu ya neema, lakini uwezo wetu wa kuipokea neema
yake ni mdogo sana. Hata hivyo, ikiwa tuko tayari kulisikiliza na kulishika
neno la Mwanawe, Mungu mwenyewe anazidisha uwezo na ukarimu wetu ili tuweze
kusonga mbele kwa matendo mema mengi kulingana na matarajio yake. Tena na tena
tunahitaji kufahamu kwamba Mungu anatarajia mafanikio yetu, lakini uamuzi ndio
wetu. Tukaribishe pendekezo la Yesu kwa utayarisho wa moyo ili tuweze kupata
maisha mapya ambayo Neno lake linatoa.
Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Githui
Nenhum comentário:
Postar um comentário