Kutafakari kuhusu 2Waf 4,8-11.14-16a; Mt 10: 37-42
Mungu anampenda binadamu kwa hiari na bure,
yaani halazimishwi kupenda wala anamlazimisha binadamu ampende yeye. Lakini
anatarajia tu upendo wa binadamu kwake ufuate njia yake ya kumpenda. Nabii
Elisha alitumwa kwenye Shunemu kutembelea wanandoa ambao hawakuwa na mtoto.
Mwanamke mwenye nyumba alimkaribisha vizuri akimtambua kama mtu mtakatifu wa
Mungu. Pamoja na mumewe walimtendea nabii mema kama mshiriki wa familia yao.
Kwa sababu ya ukarimu wake, nabii Elisha alimpatia zawadi ya kumzaa mtoto
mmoja. Kujitolea kwake mwanamke kwa ajili ya nabii Elisha ni kwa sababu aliweza
kutambua katika mtu huyo maonyesho ya upendo wa Mungu mwenyewe aliyepanga
kusababisha hali mpya maishani mwake.
Katika injili Yesu anaomba upendo kamili na wa
kipekee kutoka kwa wanafunzi wake, yaani “Ampendaye baba au mama yake kuliko
anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi,
hanistahili. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.” Kama
mwendelezo, yeye aliongeza haja ya kuyasalimisha maisha kwa ajili yake.
Inamaanisha kwamba kwa Yesu upendo ni kujisalimisha kwa ajili yake. Wazazi na
familia nzima ni zawadi ya Mungu, lakini hawawezi kuchukua nafasi ya Mungu
katika maisha ya wanafunzi. Hakuna upinzani kati ya upendo kwa Mungu na kwa
wazazi, lakini ni tofauti na tena Yesu anaomba kwamba upendo kwa ajili yake uwe
kipaumbele kwa sababu ndio upendo huu unaozaa upendo kwa ajili ya wazazi na ya
wengine.
Kabla ya andiko hili, Yesu alikwisha sema
kwamba hakuja kuleta amani bali kuleta upanga unaowaimarisha watu kuchukua
uamuzi katika familia na kumhusu Mungu. Upendo ambao Yesu anaomba kutoka
wanafunzi wake unatukumbusha mazungumzo ambayo Yeye alimwuliza Petro kwa mara
tatu kuhusu upendo wake, yaani “Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi
kuliko hawa?” Naye akajibu, “Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi
nakupenda.” Ingawa Yesu anajua udhaifu wa wanafunzi wake, anaomba upendo “mara
tatu”, yaani “kamili”, maana yeye mwenyewe anawawezesha wanafunzi kupenda
hivyo. Yeye anajitambulisha na wanafunzi wake na kwa hivyo anawaalika kuchukua
ahadi ya kumpenda hadi mwisho kama yeye alivyo.
Maneno yake yalikuwa nafasi ya kutafakari kwa
kweli maana ya safari yao. Yesu ni wazi sana akiwajulisha masharti ili wawe
wanafunzi wa kweli. Hivyo, alizuia kwamba wamfuate kwa njia yoyote. Ikiwa
wanataka kupata mafanikio katika safari yao wanapaswa kuchukua matokeo ya
uamuzi huu. Hapo tuko na jambo la msalaba ambao ni ishara ya upendo wa Yesu
mpaka upeo na tabia ya wanafunzi ambao wanajitambulisha na mwalimu wao.
Pendekezo la Yesu linajumuisha kujinyima, kwa sababu yeyote anayekutana na Yesu
kwa kweli amekwisha pata hazina ya kweli kwa maisha yake naye hawezi kubaki
alivyo, yaani mambo mengine hayana maana tena. Kwa maneno mengine, Yesu anataka
kuwa kipaumbele maishani mwa wanaoamua kumfuata. Hakuna jambo lingine ambalo
liweze kuitoa maana ya kweli kwa maisha yao ila Yesu mwenyewe.
Kama wanafunzi wapya wa Yesu sisi tunaalikwa
kumtegemea Mungu katika mambo yote na kumpenda juu ya yote kama Yesu alivyo.
Yeye anatukabidhi ufalme wake na kutujulisha njia ya msalaba ili tuweze kufanya
mapenzi ya Baba yake. Kupitia njia hii, tunatambua kwamba Kumfuata Yesu
hakuuleti upendeleo au hadhi, bali nafasi ya kujisalimisha kwa upendo kwa ajili
ya ufalme wa Mungu. Basi, yeyote ambaye anataka kuishi shwari na bila ahadi
hawezi kumfuata Yesu. Tena yeyote ambaye anatamani kumfuata Kristo bila msalaba
hatamfuata Yeye kwa kweli kamwe. Kuchukua msalaba ni ishara ya utayari wetu wa
kuyakaribisha mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu. Kwa kufikia lengo hili
tunapaswa kujikana ili Mungu aweze kujifunua kwa nguvu yote ya upendo wake.
Kuacha mahali muhimu ama nafasi ya kuwa rejeo ni njia kamili ili tuweze kuwapa
wengine nafasi zaidi. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuwafikiria wengine kuwa wa
muhimu kuliko sisi wenyewe. Tukifanya hivyo hakika tunaweza kumfuata Yesu kwa
upendo kamili na wa kipekee.
Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine Githui
Nenhum comentário:
Postar um comentário