domingo, 9 de julho de 2017

ANAYAPINGA MATARAJIO YA WAKUBWA NA KUYATIMIZA MATUMAINI YA WADOGO


Kutafakari kuhusu Zc 9,9-10; War 8,9.11-13; Mt 11,25-30


       Ni muhimu sana kutafakari tena kuhusu jambo la picha za Mungu kwa sababu mtazamo wetu, mawazo yetu na misimamo yetu mbele ya mambo yote ulimwenguni yategemea picha yetu ya Mungu. Maandiko haya yanatualika kufikiria picha kamili za Mungu ambazo ni muhimu sana katika safari yetu ya imani, yaani Mungu Mnyenyekevu, Mungu wa amani, Mungu Emanueli, Mungu wa Uhai, Mungu Aliyeguswa na hisia, Mungu Baba, Mungu Mpole na Mnyenyekevu wa moyo, Mungu wa wadogo, n.k. Tunaalikwa kumwacha Mungu awe Mungu mwenyewe. 
  
        Ingawa andiko la somo la kwanza liliandikwa baada ya utumwa wa Babeli, nabii Zakaria alitangaza habari ya wakati mpya ujao ambao Watu watafanywa wapya na mfano wa upole wa Mungu. Yeye anatangaza kwamba Mungu anakuja kwao na wakati huo huo yeye anakwisha kuwepo miongoni mwa watu kama Mungu wa amani. Watu ambao wanaweza kumtambua ni wale ambao Yesu atataja katika injili kama “wadogo”. Mfano wa upole wa Mungu unayapinga matarajio ya wale wanaojiona wenye nguvu na kutafuta masuluhisho kwa matatizo kupitia ukatili. Habari njema ambayo tuko nayo ya kutangaza ni kwamba Mungu ni tofauti na zile picha ambazo zinawaogopesha watu. Kulingana na somo la pili, Roho wa Mungu anakaa ndani yetu na kutaka kuongoza matendo yetu ili yamhusu Mungu aliye uhai na kutufanya kuishi kutokana na njia yake.

          Katika injili Yesu anasali kwa shukrani akimwita Mungu kama Baba. Katika injili ya Matayo Yesu anazungumza na Mungu kama Baba kuliko injili nyingine. Akitumia neno hili Yesu anaonyesha kwamba alikuwa na uhusiano wa pekee na Mungu. Ilikuwa kama mtoto mdogo na baba yake. Kwa Kibantu na Kiswahili, neno ambalo Yesu alitumia (Abba) linamaanisha “Tata”. Hakuna Myahudi ambaye aliweza kuwa na uhusiano na Mungu kama hivi kwa sababu hao walimheshimu sana kama mwenye nguvu kuliko kitu kingine chochote. Yesu alijiona kitu kimoja na Baba na kwa hivyo alimtegemea yeye katika mambo yote. Uhusiano wa ndani anaoishi na Baba yake sio umefungwa, bali ni mwaliko ili wanadamu wote washiriki. Ndiyo mapenzi ya Baba jambo hili nayo Mwana peke yake anaweza kulisaidia hilo.

            Uwezo wa maskini wa kuyakaribisha yale ambayo yalifunuliwa na njia ya Mungu ya kutenda inayosababisha sifa na shukrani moyoni mwa Yesu. kweli Mungu “anajifunua kwa wafuasi duni, wasiyo na vyeo vya juu wala sifa kubwa katika jamii. Wao walifanana kama watoto wadogo, katika unyofu na moyo ulio tayari kupokea. Hao ndiyo watakaoweza kutii na kuieneza Injili ulimwenguni kote.” Hivyo, katika kazi yake ya kufunua mpango wa Mungu, Yesu aliyapinga matarajio ya wenye elimu na kuyatimiza matumaini ya maskini. Kweli watu wenye hekima na wenye elimu hawakusadiki kwamba Yesu alikuwa Masiya wala kukaribisha ujumbe wake kama ufunuo wa Mungu kwa watu wake. Kwa upande wa wadogo, Yesu ndiye yule ambaye walimtarajia kwa hamu sana. Watu hawa waliweza kukaribisha mafundisho ya Yesu kama yaliyotoka kwa Mungu kwa sababu mafundisho hayo yaliihusu hali yao ya walio heri wa Mungu.  


           Yesu anatualika kuenda kwake ili tuweze kujifunza na kuishi maisha ya upendo, ya unyenyekevu na upole. Yeye mwenyewe anajijulisha kama rejeo la fadhila hizi kwa sababu alipata kuishi fadhila hizi kabisa. Kama ilivyotokea katika hotuba ya milimani, alipopendekeza heri nane, yeye alipendekeza njia yake mwenyewe ya kuishi kwa sababu ndiye yeye Heri wa pekee. Hivyo, ni rahisi kwa wadogo wajitambulishe naye. Maisha yake ni tangazo ya upole na unyenyekevu wa Mungu. Fadhila hizi ni kipimo ili tuweze kuwa kama wadogo na kuwa na moyo kama yeye alivyo navyo. Yeye peke yake anaweza kutupa fadhila hizi. Yeye anajua kuhusu uzito wetu hasa wakati hatuwezi kuchagua ama kuamua kwa uhuru kabisa hali nzuri kwa maisha yetu ama kwa nchi yetu na kupendelea kutumia ukatili badala ya amani. Masharti ya Yesu hayatufanyi kubeba uzito ulio zaidi kuliko nguvu zetu maana yeye mwenyewe anatusaidia kuchukua hayo. Mfano wake utufaye tayari ya kumkabidhi Mungu maisha yetu badala ya kuutegemea uwezo wetu peke yake.   

Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine Githui

Nenhum comentário: