Kutafakari kuhusu Mwanzo 12: 1-4a; Mathayo 17:1-9
Safari ya wale wanaomwamini
Mungu ina maana kwa sababu wanatembea kwa tumaini la kuishi milele. Binadamu ni
“mtafuta wa Mungu” tangu kuzaliwa kwake. Baada ya kila hatua, tunaalikwa kuendelea
kwenye nyingine maana hamu fulani ndani yetu inatuimarisha kusonga mbele na
kutuambia, “upeo wa macho bado”, lakini ni lazima kuendelea kutembea. Kuna
mambo mengi ya kuacha kwa sababu kila hatua mpya ya maisha yetu inatuongoza
kuchukua mambo mapya.
Ili tufikie lengo kamili
la maisha yetu hatuhitaji haraka bali uamuzi ulioandamana na imani unakuta
mwelekeo wake kamili kwa sababu yule anayetualika kwa “tukio la kuishi”
anatuvutia kwake kweli, kulingana na Mt. Augustine anayesema, “Ee Mungu,
umetufanya kwa ajili yako na mioyo yetu inahangaika hadi ikapumzike kwako”. Tukimwangalia
Yesu anayegeuka sura ni rahisi kuelewa maana ya kweli ya maisha yetu. Hivyo
ndivyo tunaalikwa kuelewa mwaliko wa Mungu kwa Ibrahimu kwenye hali
isiyojulikana na mwaliko wa Yesu kwa wanafunzi wake waandamane naye kwenye
mlimani.
Ibrahimu
anafahamika kama “baba yetu katika imani” kwa sababu alikuwa wa kwanza aliyesadiki
tofauti kabisa na matarajio ya kibinadamu. Yeye alialikwa kuacha yote na
kufunga safari. Hakujua mahali ambapo alipaswa kufika, hata hivyo aliamua kumwamini
Mungu na kuzikubali ahadi zake kama kipimo katika safari yake. Mambo yote
yaliyosemwa na Mungu yalitimia kwa sababu ni mwaminifu yule aliyeahidi. Ibrahimu
alisonga mbele sio kwa ajili ya kutimiza mpango wake wa kibinafsi tu bali pia kwa
kufanya mapenzi ya yule aliyemwalika kufunga safari. Safari yetu siyo tofauti
na ile ya Ibrahimu. Labda tunahitaji imani kama vile yake.
Tukio la kugeuka
sura kwa Yesu kulitokea baada ya siku sita ya ufunuo kuhusu mateso, kufa na
kufufuka kwake. Wakati huo huo aliwaalika wanafunzi wamfuate kwa “kujikana wenyewe,
kuuchukua msalaba wao na kumfuata Yesu.” Kweli mambo hayo yalikuwa dhidi ya
matarajio yao yote kuhusu mtu huyo waliyetambua kama Kristo wa Mungu. Hata yeye
aliongea kuhusu kufufuka kwake, lakini mioyo yao ilikwisha sumbuliwa nao
hawakuweza kuelewa vizuri. Basi, Yesu aliwaalikwa baadhi ya wanafunzi waandamane
naye kwenye Mlima Tabor. Safari hii ilibadilisha mtazamo wao. Huko mlimani Yesu
aligeuka sura mbele yao. Yesu aliwaonyesha kidogo utukufu wake na hali ijayo ya
maisha ya wale wanaomfuata kwa uaminifu. Yesu aliwaalika kwa uzoefu wa juu ili
waone kwa mtazamo wa juu na kuweza kuona vizuri hali ya kujisalimisha kwake na
hali ambayo waliakwa kuichukua kama ahadi na Mwalimu wao.
Uwepo wa Musa na
Elia unaeleza kuhusu rejeo la ufunuo katika Agano la Kale. Wote wawili waliongea
na Yesu wakionyesha kwamba hakuna kupasuka kati ya mafundisho yao na yale ya
Yesu, bali uhusiano na mwendelezo. Lakini kulingana na sauti iliyosikika kutoka
kwenye wingu, ingawa mafundisho ya Yesu ni mwendelezo, ndiye yeye kwa uwezo wa
kufundisha na kutafsiri kamili yale yaliyosemwa na mababu wa zamani. Baba alishuhudia
kuhusu Mwana wake, akimuweka kama rejeo la maisha yetu, yaani, “Huyu ni
Mwanangu mpendwa, msikilizeni”. Wote wanaalikwa kumsikiliza[1].
Kusikiliza katika Biblia ni kitenzi chenye nguvu sana. Hii ni tabia kamili ya Myahudi
mbele ya Neno la Mungu, akifanya mazoezi kuhusu yale aliyosikia. Basi, kusikiliza
kuna uhusiano wa kidani na kushika/kutenda.
“Wanatamani kubaki
mlimani, lakini sauti inatoka mbinguni iliwaalika kumsikiliza na kumtii Yesu.” Mara
nyingi Mungu anatualika kufanya uzoefu wa uwepo wake kama ilivyotokea na
Ibrahimu ama kama vile wale kwenye mlimani. Mfano, tunaposhiriki katika sherehe
fulani ama siku za maombi na kadhalika. Uzoefu kama huu unaiimarisha imani yetu
na hamu yetu kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kwa kawaida tunataka uzoefu huu uwe wa
muda mrefu. Lakini safari yetu yapaswa kutendeka kati ya “kupanda mlimani” (mfano
wa uzoefu wa Mungu wa kibinafsi) na “kushuka milimani” (mfano wa changamoto za undugu
na kazi). Kila siku tunaalikwa kufanya uzoefu wa “kugeuka sura” kwa kusikiliza
Neno la Yesu na kufanya mazoezi kuhusu Neno hili. Uzoefu huu unatusaidia
kutambua nyuso bila heshima za ndugu wengi kandokando yetu na kuona hisia na
tabia za Kristo kwa ajili yao. “Kusikiliza neno lake kunatupatia nguvu ya
kumfuata mpaka mwisho.” Hii ni njia kamili ili tuwe pia “wana wapendwa” wa
Mungu.
Fr Ndega
[1] Yesu ni ufunuo wa kipekee wa Mungu. Hakuna mwingine ambaye aweze
kumdhihirisha Mungu kama Yesu alivyo. Kweli Mungu aliongea wakati wa zamani kwa
mababu zetu. Lakini “siku hizi” mambo yote ambayo Mungu anaendelea kudhihirisha
kwa watu anafanya kwa Mwanawe Yesu Kristo. Hata wale ambao hawamjui Yesu wanapokea
ufunuo wa Mungu kwa njia yake. Katika kila ndugu ambaye wanamsaidia wanaweza
kukutana na Kristo ambaye alijitambulisha na walio na mahitaji mengi (cf. Mt
25,31-46). Kipimo ni upendo/huruma. Matendo yao ya huruma yanaongelea Kristo.
Nenhum comentário:
Postar um comentário