Tafakari tarehe 1 Sam 16,1b, 6-7,10-13a; Eph 5,8-14; Jo 9,1-41
Mungu ambaye Yesu ulionyesha ndiye Mungu wa
huruma, Mungu aliyeshughulika na maisha ya binadamu, Mungu wa upendo, Mungu
aliye Baba. Lakini mara nyingi tumesikia kwamba “Mungu anaadhibu;” au “Mungu
analazimisha kwamba jambo lifanyike kwa njia moja na siyo ya nyingine; au kwamba
mtu alimwua mwingine “kwa jina la Mungu;” au mbele ya hali mbaya, mtu anasema
“ndiyo mapenzi ya Mungu,” n.k. Je, Mungu huyo tunayezungumzia ni Mungu mmoja aliyefunua
Yesu Kristo? Nadhani wakati wa kupata kumjua Mungu vizuri umefika. Hakika
“tunajua” mambo mengi kumhusu Mungu kwa njia ya akili; lakini ni lazima “kumjua”
hasa kwa njia ya imani. Ninaongea juu ya kitenzi kujua kulingana na hali ya
kibiblia, yaani uhusiano wa upendo. Baadhi ya namna za “mapepo” - picha za
Mungu – tunaweza kufukuza kwa sala nyingi peke yake.
Andiko la kwanza anaongea juu ya uchaguzi na
upako wa Daudi kama mfalme. Vipimo Vilivyotumika kwa ajili ya jambo hili ni
kinyume na matarajio yote ya kibinadamu. Kwa kawaida sisi tunapomtazama mtu
tunaangalia hali ya nje ya mwili na kuzingatia nguvu zake; tena tunafikiria
uwezo wa kuongea na mambo mengine ambayo yanasababisha mshangao kwetu – hayo ni
mambo ya nje tu. Macho ya Bwana yanalenga yule aliye mdogo, asiye na umaarufu
na yule mnyenyekevu. Mungu anaona vizuri kwa sababu anaweza kuona linalotokea moyoni
mwa watu. Kwa hiyo, mtu anaweza kuona vizuri ikiwa anaweza kuona kama Mungu
anavyoona na kisha, tena anaweza kutenda kulingana na moyo wake Mungu. Tunajua
kwamba moyo ni mahali muhimu pa maamuzi yetu. Hivyo, ndipo moyoni tunapoamua
kuishi kama watoto wa mwanga au watoto wa giza.
Lakini kabla ya uamuzi wowote, Mt. Paulo
anataka tufikirie kwamba tumeangazwa na Kristo ili tuwe na kuisha kama watoto
wa mwanga. kwa upande wake, Mungu anatuhakikishia hali ya mwanga, lakini
mwendelezo wa hali hii unalitegemea jibu la kila siku. Mimi najiguswa sana na
maneno ya Mtakatifu fulani ambaye anasema, “Je, sisi tu ni nani? Sisi tu watoto
wa Mungu; na tena, Je, tunakuwa nini? Hili ni jibu letu kwake.” Bila shaka
kwamba katika majibu yetu haiwezekani kukosa matunda ya wema, haki na ukweli.
Ni vizuri kujua kwamba Mungu ana mpango wa upendo kwa maisha yetu na tena anatupa
zawadi zote kwa kutimiza mpango huu. “Yeye anatuambia kwa nabii Yeremia: Je, Efraimu si mwanangu mpendwa, mtoto ninayependezwa naye?
Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake, bado ninamkumbuka. Kwa hiyo moyo
wangu unamwonea shauku, nina huruma kubwa kwa ajili yake (Yer 31.20).”
Katika Yesu, Mungu ana njia maalum ya
kuangalia. Yesu anaona mtu aliyezaliwa kipofu na mtazamo wake umejaa upole na
huruma. Wakati wengine waliangalia na kumwona mtu aliye na hatia na kuadhibiwa
na Mungu, Yesu alimwona mtoto mpendwa wa Mungu, ambaye ana hamu kubwa ya
kushiriki kikamilifu katika jumuiya na kuwatambua wengine kama ndugu na dada wa
kweli. Swali la wanafunzi linaonyesha mawazo ya mazingira yale ambayo
yalifikiria upofu na magonjwa mengine kama adhabu ya Mungu. Yesu hakujibu nini
iliyousababisha upofu. Yeye alipendelea kufunua picha ya kweli ya Mungu akiwatunza
watu kwa njia ya pekee. Akimponya mtu aliyezaliwa kipofu, Yesu alidhihirisha
pia utambulisho wake kama Masihi, kwa sababu kulingana na utabiri wa nabii
Isaya Masiha aliyetarajiwa peke yake aliweza kufanya tendo kama hilo (Isa
29:18). Hivyo, maana ya maswali ya Mafarisayo na upinzani wao wa kukubali
kwamba tendo hili litoke kwa Yesu.
Yesu anajifunua kama mwanga wa ulimwengu na
kuhakikisha kwamba wale wanaomfuata hawatembei gizani, bali watakuwa na mwanga
wa uzima. Kumfuata Yesu ni kutembea katika mwanga. Na kufuata huku hufanyika
katika mwendo wa kuangazwa kama ilivyotokea kwa uponyaji wa kipofu yule. Mate
ya Yesu yalichanganywa na ardhi yalisababisha hali mpya. Ndio uumbaji mpya kwa
yule kipofu kama ilivyotokea katika mwanzo wakati Mungu Alipomwumba mtu kwa
udongo na kwa pumzi yake alimletea binadamu uhai. Mate ya Yesu ni ishara ya
Neno lake linalotupa mtazamo mpya na hamu ya kutembea. Lakini kutambua kazi hii
ya neno lake haitoshi kuwa mwanafunzi wake. Tunapaswa kumtambua yeye kama mtu aliye
zaidi ya “binadamu aliyeitwa Yesu” na zaidi ya “nabii.” Yeye ni Kristo wa Mungu
naye anataka kujifunua mwenyewe anapokutana na kila mmoja wetu kwa njia ya kibinafsi
ili tuweze kumtambua na kumshuhudia. Ndiyo katika sala daima ambayo inatokea utambulisho
wa mwanafunzi na Mwalimu wake.
Kutokana na mwendo huu tunaweza kuchukua mambo
matatu muhimu kwa safari yetu. Kwanza, ni kuhusu mtazamo wetu juu ya Mungu. Tunahitaji
kurekebisha picha zetu za Mungu. Ndilo kosa kubwa kufikiri kwamba tunaweza
kudhibiti Mungu na vipimo vyetu vidogo vidogo. Hatuwezi kuweka mipaka kwa
ukarimu wake na huruma yake. Kile tunachohitaji kwa kweli ni kuruhusu Mungu awe
Mungu na kutufunulia kwa nguvu zote za upendo wake. Pili, ni kuhusu maono yetu juu
ya wengine. Tunapaswa kujifunza kuangalia kwa “mtazamo” wa Mungu, kwa sababu
tuna maono yenye upungufu. Wakati tunapoangalia watu sisi huwahukumu na hata
tunawaadhibu. Mtazamo wa Mungu hauhukumu wala hauadhibu, bali unamsukuma mtu
aende mbele kwa sababu huu ni mtazamo wa upole na huruma. Tatu, ni kuhusu haja
ya ushirika kati ya tamani yetu na mapenzi ya Mungu. Mapenzi yake ni “kutubadilisha
ili tuwe kama Mwana wake Yesu.” Huu ni mwendo wa muda mrefu unaotokea kila siku
kwa kusikiliza Neno lake ambalo linatuita kutubu, linagusa mioyo yetu na kutuimarisha
tutende mema.” Hivyo, hatua kwa hatua, tutaponywa juu ya mtazamo wetu wenye
upungufu kuhusu Mungu, kuhusu sisi wenyewe na kuhusu wengine.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário