sábado, 1 de abril de 2017

UKAMILIFU WA MAISHA YETU


Kutafakari kutoka Ez 37, 12-14; Rom 8, 8-11; Yoh 11: 1-45


         Maisha yetu ni fumbo kubwa. Ndiyo zawadi inayotoka kwa Mungu na kupata ukamilifu wake katika Kristo. hivyo, maisha hayafikii mwisho hapa duniani. Urithi wa maisha ya wale waliotuacha unathamini sana kwetu tunaoitwa kuendelea safari yetu ya imani tukiishi kwa maana. Ikiwa hatuwezi kuwaona tena wale ambao walitutangulia, yale maadili waliyoishi na kutuachia ndiyo yanashuhudia kwamba uwepo wao kati yetu haukuwa utupu. Mtakatifu Yohane Calabria alikuwa na mazoea ya kusema, “Ikiwa Mungu yumo ndani yetu, tutafanya yale mema hata kwa kupita kwetu tu”. Kusherehekea Mababu ni alama kubwa ya jinsi wanavyoendelea kuwepo maishani mwetu na kutuimarisha katika safari yetu. Katika fumbo la Yesu Kristo aliye ufufuko na uzima, tunapata kuelewa ushirika uliokuwepo kati yetu na waliotutangulia na kuona mbele kwa matumaini ya kupata mafanikio kabisa ya maisha yetu ambayo wakati yanapoonekana duniani yanaishi sehemu yake ya kwanza tu.

     Kulingana na andiko la kwanza, watu waliokuwako utumwani walionekana kuwa waliokufa na kukaa kaburini. Mungu anayewapenda watu wake hataki wakae katika hali hii wala hataki wawe waathirika wa nguvu yoyote inayozaa mauti. Akiwashirikisha roho wa uhai, Mungu alijifunua mwenyewe kama Chanzo cha uzima na kutaka kuwashirikisha watu uhai wake ili waishi milele. Hivyo, utukufu wake unatimiza kabisa kwa sababu “Utukufu wa Mungu unatendeka wakati binadamu anapoishi.” Kwa mtazamo huu, Mt. Paulo anatualika kufikiria kwamba watu walio wa Mungu ndio watu wamefunguliwa kwa uzima na kuusaidia uzima. Safari ya imani ndiyo safari ya maisha yanayofanywa upya daima na Roho wa Mungu. Roho huyo aliyemfufua Yesu amekaa ndani yetu akitufanya watu wa Kristo na watoto wa Mungu. Tumeitwa kuishi milele na kwa nguvu ya Roho huyo Mtakatifu tutatimiza kabisa wito wetu tukionja ufufuko sawa ambao Yesu Kristo alivyo.

       Mungu anataka tushiriki katika uhai wake kama ilivyotokea kwa uzoefu wa urafiki kati ya Yesu na marafiki wake watatu, yaani Martha, Maria e Lazaro. Dada walikuwa wawili, lakini uhakika ulikuwa mmoja, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa (Yoh 11,21).” Mtu anayeishi uhusiano wa upendo na Kristo anaweza kuutambua utambulisho wake wa kweli. Kweli mikutano mingi na Yesu iliwawezesha marafiki hawa watatu kumkaribisha Yesu na kumtambua kama Masiha wa Mungu ndiye Ufufuko na Uzima. Habari ambayo Martha alimpasha Maria, yaani “Mwalimu yuko hapa, anakuita,” ina nguvu sawa ya maneno “Lazaro! Toka nge!” Maneno haya yanaonyesha njia ya Mungu ya kupenda. Katika Kristo Mungu anaguswa na uchungu na mateso ya watu. Mwaliko wa Yesu kwa Maria akutane naye na kwa Lazaro aache kaburi, ulikuwa mwaliko wa kuacha uchungu ili kupata furaha, kuacha giza ili kupata mwanga, kuacha mauti ili kupata uhai.

      Ufufuko wa Lazaro ni tangazo la ufufuko wa Kristo na uhakika wa ufufuko wetu katika Kristo. Hali inaliimarisha tumaini letu na kutoa maana kwa imani yetu. Kwa hivyo, Mt. Paulo anasema, “Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure na tumaini letu ni pasipo maana”. Mungu ambaye tunamwamini ni Mungu wa uhai naye anapotupa uzima, hujiunganisha nasi na kutufanya wanawe wapendwa. Kwa kuwa mateso katika maisha haya, hayawezi kulinganishwa na furaha tutakayohisi na utukufu utakaotufunuliwa. Vilevile, tujifunze kujisalimisha kutoka kwa Yesu ambaye hata katika wakati wa uchungu na mateso aliilenga imani yake katika tendo la riziki ya Mungu, yaani “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”. Hili lazima kuwa kilio cha roho zetu ili tujihakikishie wenyewe kwamba Mungu hawezi kutuacha wala kunyamaza mbele ya kinachotokea nasi. Mbele ya kufa kwake Yesu, jibu la Mungu lilikuwa ufufuko wa Mwanawe. Hali hii inatupa tumaini kuhusu kufufuka kwetu na hivyo, inatuhakikishia maisha kamili kwani yeye si Mungu wa wafu bali ni wa wanaoishi. Hivyo tunapaswa kutangaza kwamba Mungu hataki kifo. Katika Yesu anajifunua kama ufufuko na uhai.

     Tunaalikwa kutangaza imani katika Yesu aliyeshinda mauti na kutambua kwamba ufufuko wake umetufanya watu wa milele. Mungu anatuvutia kwake kwa huruma yake na kukaa pamoja nasi kwa Roho wake. Kutangaza imani katika ufufuko wa mwili ni kutambua kwamba Mungu anaendelea kufanya makuu kwa ajili ya watu wake dhidi ya matarajio yote mabaya kuhusu maisha ya binadamu. Lengo la maisha yetu ni kupata ukamilifu nao ukamilifu wetu ndio Mungu, kama alivyosema Augustino, yaani “Ee Mungu ulituumba ili tuwe wako na mioyo yetu inahangaika hadi tunapopumzika kwako”. Kwa Yule aliye na imani, kifo ni pumziko tu katika Mungu, yaani kujisalimisha mikononi mwa yule ambaye anatujali kwa sababu anatupenda. Wakati muhimu sana wa maisha yetu  utakuja ambao tutakutana na Mungu kwa njia ya kipekee. Tutakapokuwa mbele yake hatutaulizwa ikiwa tumeshiriki katika dini fulani wala mara ngapi tulienda kanisani, bali kiasi gani tuliweza kupenda. Ingawa ndizo chaguo zetu ambazo zitadhihirisha mwelekeo wa maisha yetu, tusisahau kwamba mapenzi ya Mungu ni kwamba maisha yetu yapate ukamilifu ambao umekwisha kuanza.


Fr Ndega

Nenhum comentário: