Kutafakari kuhusu Kutoka 17, 3-7; Yohane 4, 5-42
Maji ni zawadi ya thamani kubwa mno. Mara
nyingi hatuitumii zawadi hii kama ipasavyo. Tunatambua tu umuhimu wa maji
wakati tuko bila maji. Maisha ya viumbe vyote yanayategemea maji[1]. Tunajua umuhimu wa kunywa
maji mazuri kwa ajili ya kiu na ya afya yetu, sio ukweli? Ingawa maji ni muhimu
sana kwa ajili ya kuizima kiu yetu ya kimwili, maji haya hayatoshi kwa ajili ya
kiu zingine zinazouhusu mwelekeo wetu wa ndani na wa kiroho, yaani kiu ya
upendo, ya haki, ya furaha, ya heshima, na ya ukamilifu. Kwa namna hii ya kiu tunahitaji
maji tofauti yaliyo maji hai. Tujiulize maswali, ‘ni nani anaweza kututolea
maji haya’ na ‘tunawezaje kuyapata maji haya?’
Kama tulivyotafakari, nyika ni mahali maalum
pa mkutano na Mungu. Wakati huo huo nyikani ndipo mahali pa kujaribiwa. Watu wa
biblia walivutiwa jangwani kwa ajili ya uzoefu wa Mungu aliye na uhusiano wa
upendo na watu wake. Tukumbuke maneno ya Mungu mwenyewe katika kitabu cha nabii
Hosea: “Kwa hiyo angalia, mimi nitamvutia, na kumleta nyikani, na kusema naye
maneno ya kumtuliza moyo (Hos 2,14).” Vivyo hivyo Yesu alipojifunua kwa
mwanamke Msamaria jangwani alimwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye (Yoh 4,26).”
Mungu wetu ni “Mungu wa neno” na kuongea na
watu wake moyo kwa moyo kwa sababu moyo ndio mahali pa uamuzi. Ndipo moyoni mwao
ambapo Mungu aliweka kiu na njaa ya kulisikiliza Neno lake (cf. Am 8,11). Mara
nyingi, kosa la utambuzi liliwaongoza kumwacha Mungu ili kuifuata “miungu
mingine”. Mungu aliwatolea maji kwa ajili ya kiu ya mwili, lakini alitaka kuonyesha
kwamba kuwepo kiu ya ndani kabisa waliyopaswa kugundua pole pole, yaani kiu ya
kumjua Mungu vizuri na ya kuiamini riziki yake. Ufundishaji wa jangwa ulikuwa
nafasi pia ya kutambua kuwa ndiye Mungu peke yake chemchemi ya maji hai kwa
ajili ya kiu yao na sio miungu.
Ufundishaji huu wa kimungu ni wazi sana pia katika
mkutano wa Yesu na mwanamke Msamaria. Mwanamke huyo alifika kisimani katika saa
sita mchana, yaani saa isiyo ya kawaida. Labda aliepuka kukutana na wengine
ambao walimkosoa na kumdharau kwa sababu ya maisha yake yenye makosa mengi. Huu
ni mkutano wa ajabu kwa maana Yesu ni Myahudi na, kulingana na andiko hili Wayahudi
hawachangamani na Wasamaria[2]. Kweli, “Yesu amevunja
ukuta uliokuwepo na uliomtenga yeye na yule mwanamke Msamaria. Anataka
kutuonyesha kuwa Mungu hatumii vipimo vya wanadamu.”
Yesu anapatikana kwa mkutano huu kwa ajili ya
kumsaidia mwanamke huyo kugundua tena furaha ya kuishi. Kweli, mwanamke huyo
hakuwa na mume wala heshima wala furaha. Kwanza kabisa, Yesu anamwomba maji,
bali sio kwa ajili ya kiu ya kimwili. Je, ilikuwa kwa kiu gani? Kulingana na Mt Agustino, “Yule ambaye aliomba
maji alikuwa na kiu ya imani ya mwanamke Msamaria.” Yesu alimwomba maji kwa
sababu alitaka kutoa maji tofauti na mazuri zaidi, ndiye yeye mwenyewe. Basi, kwa
njia maalum na kwa uvumilivu, Yeye alimwongoza mwanamke atofautishe kati ya
‘kiu ya mwili’ na ‘kiu ya uzima.’
Yesu aliyajua makosa mengi ya mwanamke
Msamaria, lakini hakumhukumu kwa maana ya hayo. Yeye alipendekeza maisha mapya
ambayo yanaanza moyoni. Kama mwanamke huyo hakumjua Yesu, alihitaji mwendo pole
pole na hatua kwa hatua ili kumwamini na kuruhusu kuongozwa naye. “Kwanza
alimwita Yesu Myahudi (Yoh 4:9); pili alimwita Yesu Bwana (Yoh 4:11.15); tatu, nabii
(Yoh 4,19), nne, Kristo (Yoh 4, 25-26.28-29)[3].” Mwanamke Msamaria
alifanya ugunduzi mkubwa wa maisha yake. Haraka ya kutangaza habari hii njema
ilimfanya aache mtungi wake ulio mfano wa kuacha shida zake, vidonda vyake,
ukabila, hofu, uasherati, aibu. yule mwanamke ambaye hakuwa mkweli aliweza kuwa
shahidi wa ukweli. Maisha yake yaliyokuwa maana ya kashfa, kutoka hapo yalikuwa
msaada kwa ajili ya kuwasaidia wengine katika imani.
Mkutano wa Yesu na mwanamke Msamaria ni mfano
wa uzoefu wetu wa Mungu. Huu ndio mkutano na huruma ambayo inamzaa mtu tena ili
awe shahidi wa huruma huu. Kama tulivyotafakari, sisi tu “watafuta wa Mungu”
tangu kuzaliwa kwetu kwa sababu Yeye mwenyewe aliweka moyoni mwetu tamani (kiu)
kwa ajili yake. “Ikiwa tunamtafuta Mungu ni kwa sababu yeye alitutafuta kwanza
(Kitabu cha Wimbo Ulio Bora).” Kwa maneno mengine, tamani yetu ya Mungu ndiye
Mungu mwenyewe anayetamani ndani yetu. Hivyo, mwanamke Msamaria ambaye hana
jina ni sisi sote tunayovutiwa kukutana na Mungu katika saa na mahali
pasipotarajiwa. Anakuja kukutana nasi katika hali ya maisha yetu - yenye haja
na udhaifu - na kutaka kuongea nasi moyo kwa moyo.
Anatutafuta tunapopotea (tukumbuke pia uzoefu
wa “mwana mpotevu”) naye hatuhukumu kwa sababu ya makosa yetu, bali anataka
tukubali pendekezo lake la maisha mapya. Mwendo huu ni wa muda mrefu lakini
ndio ufanisi hasa tunapokiri ukweli wa maisha yetu na kukubali ukweli wa Yesu. Ikiwa
ninabaki kufungwa bila kukiri udhaifu wangu tena itakuwa ngumu kufanya uzoefu
wa kweli wa Mungu. Yeye anapatikana kama chanzo cha “maji hai” ambayo yanazizima
kiu zote. Kwa hivyo, tukubali maji haya yametolewa na Kristo ili sisi pia
tuweze kuwa chanzo cha maji yanayobubujika kwa uzima wa milele.
Fr Ndega
[1] Katika sayari yetu maji yako zaidi kuliko ardhi (71%). Maisha ya sayari unayategemea maji. Kuna maji
misituni, katika wanyama, mwilini mwetu na kadhalika. Maji yanarudisha upya,
yanasafisha, yanatakasa na kutoa uhai.
[2] “Tunayo historia ndefu ya chuki na uadui kati ya Wayahudi na Wasamaria
ambayo imedumu hata leo. Wote wanamkiri mhenga mmoja katika Imani yaani
Ibrahimu, na wote wana vitabu vitano vya kwanza katika Biblia takatifu ambavyo
vinaitwa ‘Torati’… Baada ya kifo cha mfalme Sulemani, palitokea ugaidi mnamo
mwaka 933 K.K uliosababisha kutengana kwa falme za kaskazini-Israeli na ufalme
wa kusini-Yudea. Mji mkuu wa ufalme wa kaskazini ulikuwa Samaria na ule wa
ufalme wa kusini ulikuwa Yerusalemu. Ufalme wa kaskazini ulistawi Zaidi ya
ufalme wa kusini. Mwaka 722 K.K Wasiria waliuteka nyara. Waliwachukua mateka
viongozi muhimu wa ufalme huo na kuwateua wageni kuwa viongozi wa watu.
Hatimaye, wageni hao walioana na wenyeji wa Samaria. Kizazi Kilichofuata
kilikuwa si kizazi halisi cha Wasamaria. Ndiyo maana Wasamaria wanadharauliwa
na Wayahudi wa Yudea (R. BAAWOBR. Injili
ya Mathayo: kwa ajili ya jumuiya ya Kikristu. Nairobi: Paulines, p.
38-39).”
[3] Id. Ibid., p. 39.
Nenhum comentário:
Postar um comentário