Kutafakari kuhusu Is 52. 7-10; Eb 1. 1-6; Yoh 1. 1-18
Sisi tunaishi wakati wa
furaha na shukrani, yaani wakati wa Krisimasi. Kila kitu kinaonekana kuwa na
rangi zaidi, mwanga zaidi na maana zaidi. Haya ndiyo matokeo ya uwepo wa Mungu
miongoni mwetu; yeye aliyachukua mazingira yetu na kutualika kujifunza kutoka kwake
ili tuweze kuishi vizuri. Tumshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa sisi nafasi ya
kuwa watu wapya. Ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu
ni ujumbe wa furaha kubwa kwa wote, kwa sababu Mwokozi alizaliwa kwa
wote. Tufurahi kwa sababu Mungu
aliamua kuyajenga makao yake kati yetu na kutuletea wokovu.
Kulingana na somo la kwanza,
baada ya uzoefu wa utumwa Watu wa Israeli waliishi hali mpya na kugundua tena
wito wao kama watu wa Mungu. Wito huu sio kutumia kisasi dhidi ya maadui yao,
bali kutangaza habari njema ndiyo habari ya amani. Habari hii ni ujumbe wa
faraja unaotoka kwa Mungu na kutia moyo wa watu. Kwa hivyo unapaswa kutangazika
kwa wote. Miguu yetu ni ishara ya upatikanaji wetu, hamu yetu kwa ajili ya
mpango wa Mungu. Yote ambayo Mungu amefanya maishani mwetu ni lazima
kutangazika. Furaha iliyo matokeo ya tendo hili itakuwa kamili maishani mwetu tu
ikiwa tunatangaza kwa wengine.
Somo la
pili linatuanzisha kwenye siri ya neno la Mungu kwa kushuhudia kwamba Mungu wetu
ndiye Mungu wa neno. Aliviumba vyote kwa nguvu ya neno lake. Yeye aliongea
zamani kwa kupitia mababu zetu, anaongea leo na kuendelea kuongea kwa sababu huyo
Neno alikuwako kwake milele. Neno hili ni Mwanawe Yesu Kristo aliye mpatanishi wa
Agano Jipya. Yeye ni utimizaji wa ahadi zote za Mungu kwa watu wa Agano la
Kale. Mambo yote yalifanyika kwa sababu yake na kwa ajili yake. Tena mambo yote
yanazunguka kandokando yake na kuikuta maana katika yeye. Hivyo hakuna yeyote
ambaye anaweza kutupatia wokovu ila yeye peke yake aliye Neno la milele la
Baba.
Kuhusu injili tuko na
mwendelezo wa ujumbe huu lakini kwa kiini zaidi. Neno la Mungu ambaye alikuwako
milele ni Mwana wa Mungu. Huyo ni maana ya vyote vilivyofanyika. Huyo Neno
alifanyika mwili tumboni kwa Bikira Maria akija ulimwenguni amejaa neema na
ukweli akifunua sura ya Mungu kama Baba aliyejaa wema na huruma. Mwana Yesu alitufanya
watoto wa Mungu na kutuangaza kwa mwanga wake ili tuwe mashahidi wa nuru na ukweli
kama vile Yohana Mbatizaji. Mambo yote ambayo Mungu anafanya ni mazuri na
kamili kwa sababu hii ni njia yake ya kutenda.
Basi, “Neno alifanyika mwili
na akakaa kwetu”. Katika Yesu, Mungu ni mmoja
wetu. Yeye ni huruma ambaye alijiruhusu kukuta na kuguswa akituletea pendekezo
mpya la maisha. Kwa hivyo, haitoshi
kuitambua huruma ya Mungu katika Yesu; ni muhimu pia tujiruhusu kuguswa
na huruma hii na tena kuongozwa na ujumbe
wake wa amani na upendo. Kuzaliwa
kwake Yesu kuliwafanya wanadamu
wote wawe familia moja ya kipekee.
Kweli, Mungu alijidhihirisha kama
jirani, maskini na
aliyekataliwa, akitualika sisi sote tutambue thamani
ya ishara ndogo na mipango midogo.
Bila shaka chaguo hili la Mungu linatualika kufikiri na kutenda kwa njia tofauti, yaani kuwa
wanadamu bora.
Mungu Mwenyezi anakubali hali
ya mtoto mdogo, kwa utegemezi
kabisa wa utunzaji na upendo wa binadamu, kwa mfano Mariamu na Yusufu. Ndiyo imani inayotuongoza kutambua mtoto huyu mdogo wa Bethlehemu
katika kila mtoto ambaye sisi hukutana katika safari
yetu ya kawaida. Kila mtoto
anaomba upendo wetu. “Tufikiri kuhusu watoto ambao hawana uzoefu
wa upendo wa wazazi wao; pia kuhusu watoto wa barabara ambao hawana mahali pa kuishi; tena
kuhusu watoto wanaotumika kama askari, wakibadilishwa kuwa vyombo vya ukatili badala ya kuwa vyombo
vya amani; pia kuhusu watoto ambao
ni waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia,
na kuhusu watoto waliolazimishwa kuacha
ndoto zao kwa sababu ya hali ya kiuchumi siyo nzuri”. Mtoto ndogo ya Bethlehemu
ni mwaliko ili tuweze kusaidia kwa hali tofauti maishani mwa watoto wetu.
Ingawa
tunaishi katika jamii ya ulaji,
inayotuzuia kulenga muhimu katika maisha yetu, tunapaswa kuwa macho. Krismasi ni zaidi ya ulaji. Ni
sikukuu ya ufunuo wa fumbo la upendo wa Mungu unaobadilisha moyo wa binadamu kuwa makao ya thamani za kweli. Mungu anatupenda kwa
hiari na ukarimu, bila astahili kwa upande wetu. Uzoefu huu unatuongoza kutenda vivyo hivyo ili
Krismasi iwe zaidi ya wakati mmoja
tu kwa mwaka. Itakuwa Krismasi daima ikiwa tuweze kujifunza jinsi ya kupenda kwa kweli na kuweka juhudi kwa kujenga jamii ya
undugu na ya haki
kwa wema wa wote.
Fr Ndega