domingo, 25 de dezembro de 2022

MUNGU ALIYAJENGA MAKAO YAKE KATI YETU

 

Kutafakari kuhusu Is 52. 7-10; Eb 1. 1-6; Yoh 1. 1-18




 

    Sisi tunaishi wakati wa furaha na shukrani, yaani wakati wa Krisimasi. Kila kitu kinaonekana kuwa na rangi zaidi, mwanga zaidi na maana zaidi. Haya ndiyo matokeo ya uwepo wa Mungu miongoni mwetu; yeye aliyachukua mazingira yetu na kutualika kujifunza kutoka kwake ili tuweze kuishi vizuri. Tumshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa sisi nafasi ya kuwa watu wapya. Ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu ni ujumbe wa furaha kubwa kwa wote, kwa sababu Mwokozi alizaliwa kwa wote. Tufurahi kwa sababu Mungu aliamua kuyajenga makao yake kati yetu na kutuletea wokovu.

    Kulingana na somo la kwanza, baada ya uzoefu wa utumwa Watu wa Israeli waliishi hali mpya na kugundua tena wito wao kama watu wa Mungu. Wito huu sio kutumia kisasi dhidi ya maadui yao, bali kutangaza habari njema ndiyo habari ya amani. Habari hii ni ujumbe wa faraja unaotoka kwa Mungu na kutia moyo wa watu. Kwa hivyo unapaswa kutangazika kwa wote. Miguu yetu ni ishara ya upatikanaji wetu, hamu yetu kwa ajili ya mpango wa Mungu. Yote ambayo Mungu amefanya maishani mwetu ni lazima kutangazika. Furaha iliyo matokeo ya tendo hili itakuwa kamili maishani mwetu tu ikiwa tunatangaza kwa wengine.

  Somo la pili linatuanzisha kwenye siri ya neno la Mungu kwa kushuhudia kwamba Mungu wetu ndiye Mungu wa neno. Aliviumba vyote kwa nguvu ya neno lake. Yeye aliongea zamani kwa kupitia mababu zetu, anaongea leo na kuendelea kuongea kwa sababu huyo Neno alikuwako kwake milele. Neno hili ni Mwanawe Yesu Kristo aliye mpatanishi wa Agano Jipya. Yeye ni utimizaji wa ahadi zote za Mungu kwa watu wa Agano la Kale. Mambo yote yalifanyika kwa sababu yake na kwa ajili yake. Tena mambo yote yanazunguka kandokando yake na kuikuta maana katika yeye. Hivyo hakuna yeyote ambaye anaweza kutupatia wokovu ila yeye peke yake aliye Neno la milele la Baba.   

    Kuhusu injili tuko na mwendelezo wa ujumbe huu lakini kwa kiini zaidi. Neno la Mungu ambaye alikuwako milele ni Mwana wa Mungu. Huyo ni maana ya vyote vilivyofanyika. Huyo Neno alifanyika mwili tumboni kwa Bikira Maria akija ulimwenguni amejaa neema na ukweli akifunua sura ya Mungu kama Baba aliyejaa wema na huruma. Mwana Yesu alitufanya watoto wa Mungu na kutuangaza kwa mwanga wake ili tuwe mashahidi wa nuru na ukweli kama vile Yohana Mbatizaji. Mambo yote ambayo Mungu anafanya ni mazuri na kamili kwa sababu hii ni njia yake ya kutenda.

    Basi, “Neno alifanyika mwili na akakaa kwetu”. Katika Yesu, Mungu ni mmoja wetu. Yeye ni huruma ambaye alijiruhusu kukuta na kuguswa akituletea pendekezo mpya la maisha. Kwa hivyo, haitoshi kuitambua huruma ya Mungu katika Yesu; ni muhimu pia tujiruhusu kuguswa na huruma hii na tena kuongozwa na ujumbe wake wa amani na upendo. Kuzaliwa kwake Yesu kuliwafanya wanadamu wote wawe familia moja ya kipekee. Kweli, Mungu alijidhihirisha kama jirani, maskini na aliyekataliwa, akitualika sisi sote tutambue thamani ya ishara ndogo na mipango midogo. Bila shaka chaguo hili la Mungu linatualika kufikiri na kutenda kwa njia tofauti, yaani kuwa wanadamu bora.

Mungu Mwenyezi anakubali hali ya mtoto mdogo, kwa utegemezi kabisa wa utunzaji na upendo wa binadamu, kwa mfano Mariamu na Yusufu. Ndiyo imani inayotuongoza kutambua mtoto huyu mdogo wa Bethlehemu katika kila mtoto ambaye sisi hukutana katika safari yetu ya kawaida. Kila mtoto anaomba upendo wetu. “Tufikiri kuhusu watoto ambao hawana uzoefu wa upendo wa wazazi wao; pia kuhusu watoto wa barabara ambao hawana mahali pa kuishi; tena kuhusu watoto wanaotumika kama askari, wakibadilishwa kuwa vyombo vya ukatili badala ya kuwa vyombo vya amani; pia kuhusu watoto ambao ni waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia, na kuhusu watoto waliolazimishwa kuacha ndoto zao kwa sababu ya hali ya kiuchumi siyo nzuri”. Mtoto ndogo ya Bethlehemu ni mwaliko ili tuweze kusaidia kwa hali tofauti maishani mwa watoto wetu.

Ingawa tunaishi katika jamii ya ulaji, inayotuzuia kulenga muhimu katika maisha yetu, tunapaswa kuwa macho. Krismasi ni zaidi ya ulaji. Ni sikukuu ya ufunuo wa fumbo la upendo wa Mungu unaobadilisha moyo wa binadamu kuwa makao ya thamani za kweli. Mungu anatupenda kwa hiari na ukarimu, bila astahili kwa upande wetu. Uzoefu huu unatuongoza kutenda vivyo hivyo ili Krismasi iwe zaidi ya wakati mmoja tu kwa mwaka. Itakuwa Krismasi daima ikiwa tuweze kujifunza jinsi ya kupenda kwa kweli na kuweka juhudi kwa kujenga jamii ya undugu na ya haki kwa wema wa wote.


Fr Ndega

Nenhum comentário: