Kutafakari kuhusu Is 60. 1-6; Waef 3, 2-3a.5-6; Mt 2, 1-12
Kidogo kidogo, liturjia imetusaidia kuelewa maana ya kuzaliwa kwa Yesu. Yeye alizaliwa huko Bethlehemu ulio mji wa Wayahudi, lakini si kwao tu; alikuja kwa ajili ya wanadamu wote. Kwa fupi, kuzaliwa kwake kunatuhakikishia kwamba sisi sote ni watoto wa Mungu na kwamba ni mapenzi yake kuokoa kila mtu.
Somo
la kwanza ni wimbo uliofanywa baada ya uzoefu wa uhamishoni. Nabii anaona
wakati ujao wa mji Yerusalemu kama rejeo la hija kwa watu wengi. Lakini maana
ya hali hii ni ya imani kuliko ya kijiografia. Katika jiji hili, Yesu
alikamilisha kazi yake, akihakikishia wokovu wa Mungu kwa wote kwa kuuondoa
(wokovu) kutoka kwa mipaka ya dini na utamaduni wa Kiyahudi. Hapo rejeo letu ni
Yesu.
Katika
waraka wake Mtakatifu Paulo anafunua kwamba Yesu ndiye ufunuo wa siri iliyokuwa
imefichwa kwa muda mrefu. Kulingana na ufunuo huu, watu wengine pia wanakuwa
warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Wayahudi. Uwepo wa Yesu unatafsiri
kikamilifu kila jambo ambalo Mungu aliwaambia manabii wa kale. “Mungu alichagua
taifa moja kama rejeo ili kuyafikia mengine yote kwa urahisi zaidi”.
Habari
za kuzaliwa kwa Yesu ni nzuri, lakini sio wote waliipokea vizuri. Kwa Mamajusi,
habari hii ilileta maana kwa maisha yao; kwa hiyo wakamtafuta mfalme mpya bila
woga wa kuziacha nchi zao na usalama wao. Kwa bahati mbaya serikali ya Kiyahudi
ilifadhaika sana kwa sababu ya hofu ya kupoteza fahari, mapendeleo na mamlaka
yao.
Mamajusi
walipendelea kuiacha hali ya usalama katika nchi zao ili kukitafuta kile
kilichokuwa zaidi ya nyota. “Waliifuata mioyo yao. Je? Nasi huifuata mioyo
yetu? Moyo unatambulikana kama mbegu ya tamaa zetu. Katika moyo ndimo
tunamohifadhi ndoto zetu na mambo tunayoyatamani maishani”.
“Mamajusi nao pia wanatamani kutafuta kile ambacho mioyo yao ilitamani. Walijua vyema hakuna jingine la kutamanika lililo zaidi ya Mungu. Na ndipo wakatoka kwenda kutafuta, huku wakiongozwa na nyota. Hawakuitafuta nyota bali kile kilichokuwa kikiwakilishwa na nyota. Sote tunapaswa kuwa na ndoto, tutoke tuifuate mioyo yetu tukitafute kilicho chema. Hapo ndipo Mungu atajidhihirisha kwetu”.
Basi,
siku hii ya leo Mungu anatualika tuwe macho kuhusu nyota anayotumia kutuongoza.
Je, umegundua nyota inayokuongoza kupata maana ya kweli kwa maisha yako? Kwa mfano
wa Mamajusi, maisha yetu ni safari ya imani kukutana na Mungu tukiongozwa na
nuru yake na kumruhusu abadilishe njia zetu. Tukikutana naye tumtolee zawadi
muhimu zaidi za maisha yetu kwa manufaa ya wote!
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário